Habari muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Eneo la kukamilisha mauzo ndiyo eneo ambalo watu wengi huwa wanaliogopa. Usiogope kumwambia mteja kinachofuata baada ya hapa ni wewe kulipia bidhaa au huduma unayotoa.
Na ndiyo eneo ambalo ukilifanyia kazi basi utaweza kuongeza mauzo kwenye biashara yako.
Hakuna pesa inayoingia kwenye biashara pasipo muuzaji kumtenganisha mteja na pesa zake.
Pale mteja anapokulipa ndiyo ushindi hayo mengine yote ni chenga.
Ushindi kamili kwenye mauzo, ni wewe muuzaji kupata fedha na mteja kupata bidhaa au huduma.
Hapa ni sababu tano ambazo mtu akiweza kuzivuka, ataweza kuwa na mafanikio makubwa kwenye ukamilishaji wa mauzo.
Soma hapa makala iliyopita kupata sababu nyingine tano; Sababu Kumi (10) Zinazopelekea Wakamilisha -1https://www.mauzo.tz/sababu-kumi-10-zinazopelekea-wakamilishaji-kushindwa-1/
6. Kuiga wengine.
Bindamu ni viumbe vya hisia, huwa tunapenda kufuata mkumbo kwa kuangalia wengine wanafanya nini.
Licha ya wewe kupata mafunzo, lakini kulingana na mazoea ya kijamii, bado unajilinganisha na wengine na kuona yale mazoea ambayo yanafanywa na wengi huenda ndiyo sahihi na kile unachoishi wewe siyo sahihi.
Changamoto kubwa ni kwamba watu wengi wanaotuzunguka hawana malengo yoyote makubwa, hivyo hawaweki juhudi kubwa. Wakiona mtu anaweka juhudi kubwa wanamkatisha tamaa.
Kwa kuzungukwa na watu wa aina hiyo na kuwaiga, huwezi kukamilisha mauzo makubwa.
Hatua ya kuchukua hapa; Epuka kutumia muda wako na watu ambao hawana malengo makubwa. Epuka kuchukua ushauri wa watu ambao hawana mafanikio na wala hawaelekei kwenye mafanikio. Simamia ndoto zako na weka juhudi kubwa bila kujali wengine wanasemaje au kukuchukuliaje.
7. Kukosa mpango wa kifedha.
Watu wengi wanaishi lakini hawana mipango ya kifedha. Wengi wanasukumwa na hela ya kula, wanafanya kazi wakipata hela ya kula wanaridhika na kushindwa kuweka juhudi kubwa.
Watu ambao hawana mpango wa kifedha kwenye maisha yao, huwa hawana msukumo mkubwa wa kukamilisha mauzo. Chochote wanachopata wanaridhika nacho kwa sababu hakuna kikubwa wanachotaka kupata.
Hatua ya kuchukua hapa; kuwa na mipango mikubwa ya fedha ili uweze kufikia mafanikio makubwa na tumia mauzo Kama njia ya kukusukuma wewe kuuza zaidi na kupata mafanikio unayotaka.
Malengo madogo ya fedha yanakufanya uridhike mapema na kuwa mtu wa kawaida. Jitoe ili uuze zaidi na upate fedha zaidi.
8. Kuchukua malalamiko kama mapingamizi.
Siyo kila mteja malalamiko yake ni mapingamizi. Mwingine anataka tu asikilizwe.
Wakati mwingine waache wateja wajielezee kwa njia ya kulalamika, wewe kaa kimya wasikilize huku ukiwaangalia machoni na baada ya hapo watajisikia vizuri baada ya kulalamika.
Wako wateja ambao desturi yao ni kulalamika, na hakuna kitu ambacho watu wanapenda kama ukiungana nao kwenye malalamiko yao wanayopitia.
Unapaswa kuchukulia kila wanachosema wateja kama malalamiko tu, mpaka pale utakapojiridhisha kwamba ni mapingamizi ya kweli.
Na kwa malalamiko, usijisumbue kuyajibu, mteja hataki uyajibu, anataka tu kuonyesha maumivu yake. Kwa malalamiko ambayo wateja wanayatoa, wajibu unawaelewa, kisha endelea na mchakato wa kukamilisha mauzo.
Hupaswi kutumia nguvu na muda mwingi kwenye kitu kisichokuwa na nguvu kwenye mchakato mzima wa mauzo.
9. Upungufu wa zana za kukamilisha.
Kama huna njia na zana za kutosha kuweza kukamilisha mauzo, hutaweza kukamilisha mauzo. Utafanya mauzo kuwa magumu kwako, lakini ukiwa na mbinu mbali mbali zitakusaidia kufanya mauzo kuwa rahisi kwako.
Unahitaji kuwa na silaha nyingi ili pale mteja anapoleta pingamizi lolote unakuwa na njia ya kulikabili hilo pingamizi.
Kwa kuwa uko kwenye mafunzo ya mauzo, usiwe na wasiwasi kwa sababu utaendelea kujifunza mbinu hizo.
10. Kikwazo kisicho sahihi
Wauzaji wengi huwa wanaona wateja ni kikwazo pale wanaposhindwa kukamilisha mauzo. Lakini hiyo sahihi, kikwazo cha mauzo kamwe huwa siyo mteja, bali muuzaji mwenyewe.
Hiyo ina maana kwamba kama unashindwa kukamilisha mauzo, tatizo siyo wateja, tatizo ni wewe muuzaji.
Kubali hilo haraka na jitafakari nini unafanya kukwamisha ukamilishaji wa mauzo. Chukua hatua kwa vikwazo unavyoweka kwenye ukamilishaji wa mauzo ili uweze kukamilisha mauzo makubwa zaidi. Kwa kukubali wewe ndiye kikwazo utaweza kuona maeneo unayokwamisha ukamilishaji wa mauzo.
Kwa mfano, kama huzingatii mambo 16 ya kuzingatia wakati wa mazungumzo ya mauzo kama vile kusifia wateja, kutoa ushuhuda, kujali maslahi ya wateja wako lazima yatapelekea mauzo kuwa magumu kwako.
Pale unapokuwa unashindwa kukamilisha mauzo, jiweke kitimoto wewe mwenyewe, pitia yale mazungumzo yako na mteja na kisha utaona wapi unakosea.
Mwisho, umeshazijua sababu zinazopelekea watu kushindwa kukamilisha mauzo. Hivyo unapokutana nazo jua namna ya kukabiliana nazo ili uweze kukamilisha lengo lako kuu ambalo ni kuuza.
Kauli mbiu yetu; ABC: ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz