Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Je, Mteja Yupo Sahihi Kila Wakati?

Hapana, mteja hayupo sahihi kila wakati. Kuna muda anakosea, ila kwa kuwa lengo lako kuu ni kukamilisha mauzo unachukulia yupo sahihi. Hii ni kutaka kuondoa hali ya kumuona msumbufu.

Naamini hapo ulipo, msemo wa mteja yupo sahihi mara zote sio neno geni kulisoma au kulisikia. Umekuwa unatumika sana. Ni msemo ulioanzishwa mwaka 1909 na Harry Gordon Selfridge, John Wanamaker na Marshall Field, mpaka leo unatumika katika biashara zetu.

Lengo lake kuu ni kushawishi wateja kwamba watapata huduma nzuri kila wakati na vile vile kushawishi wafanyakazi kutoa huduma nzuri kwa wateja.

Ipo hivi, mteja anapokuja katika biashara yako au unapokua unaongea naye kuna hitaji analo au kuna namna anaelewa jambo. Ikiwa na maana anapokuwa anakupatia maelezo ili baadaye umhudumie anachotarajia kutoka kwako ni kumsikiliza na kumpatia hitaji au huduma yake.

Kujaribu kupingana na anachosema mteja ni ugomvi mkubwa unataka kuanzisha. Maana hakuna mtu anayekubali kushindwa huku akitoa pesa yake. Atakachoweza kufanya ni kuendelea kukupinga ili kudhihirisha kuwa kipo kitu anakijua kuhusu bidhaa fulani. Mjadala huo lazima uwe mkubwa na ikiwa mmoja wapo hatoshuka basi hitimisho halitaweza kufikiwa mwishowe hakuna hitimisho litafikiwa.

Unapokuwa kwenye biashara wewe jua kwamba mteja yuko sahihi. Hii ni kauli unayopaswa kuielewa kwa kina sana. Kwamba mteja yupo sahihi mara zote. Hata kama kwa upande wako unaona hayupo sahihi, jua kwa upande wake anajiona yupo sahihi. Na yeye ndiye anayefanya maamuzi iwapo anunue au la, na anunue kwako au kwingine.

Katika mazingira yetu ya biashara tunakutana na changamoto nyingi sana kutoka kwa wateja. Wengine wanakutukana, wengine hawataki kufuata utaratibu fulani katika biashara yako. Wengine wanafanya fujo kama vile kupigana katika biashara yako, wanakugombeza bila sababu za msingi, vitu kama hivyo.

Kwa mantiki hiyo, lazima utaona changamoto. Lakini kwa kufuata maana kamili ya msemo huu “customer is always right”, unaamua kupotezea na kujishusha ili ukamilishe mauzo. Maana ndiyo kazi kubwa inayokuweka katika biashara.

Je, msemo huu “mteja mara zote/kila wakati yuko sahihi” ni sahihi kuendelea kuutumia?

Jibu ni ndiyo. Maana kazi yako kama mhudumiaji sio kumlazimisha mteja kufanya maamuzi. Bali unawajibu wa kumsaidia vema kufanya maamuzi. Hii ni pamoja na kumsikiliza vema juu ya kile anachohitaji.

Sababu Za Kwanini Mteja Yupo Sahihi Mara Zote?

Moja; Mteja ana haki ya kusikilizwa.
Bila kujali amekosea au hajakosea, wajibu wako mkuu kama mtu wa mauzo ni kumsikiliza mteja. Na hiki ndicho kitu anachohitaji kutoka kwako kama muuzaji.

Mbili; Wateja wanataka kuona tatizo lao limetatuliwa.
Tatizo ndilo huwaleta wateja katika eneo lako. Hivyo, ukimpa suluhu Atashawishika kununua kwako tena.

Tatu; Wateja wanapofurahia wanaleta wateja wengine.
Zaidi ya asilimia 60% ya wateja hufanya manunuzi katika biashara tofauti. Hivyo, unapowahudumia vema unawavutia zaidi.

Hivi vitu ukiweza kuvifanyia kazi itakuwa ni rahisi kukabiliana na wateja wako. Kwa sababu utakuwa unajua kupitia mteja ndipo unapata mahitaji yako pamoja na kuiendesha biashara yako.

Je, unawachukuliaje wateja wako?

Kwa hayo na mengine mengi karibu Chuo Cha Mauzo upate mafunzo zaidi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi.
Tufuatilie www.mauzo.tz

1 Comment

  • Faraji
    Posted December 21, 2023 at 6:00 am

    Mteja ni mfalme nn a mfalme hapingwi,.

Leave a comment