Baada ya mteja tarajiwa kugeuzwa kuwa kamili kwa kukubali kulipia. Kinachofuata baada ya hapo ni mteja mwanachama.
Huyu ni mteja ambaye amenunua kwako zaidi ya mara mbili. Kwa lugha rahisi anakuwa amerudi tena kununua bidhaa au huduma baada ya manunuzi ya kwanza na ya pili.
Neno hili la uanachama tumekuwa tukilisikia mara nyingi zaidi kwenye maeneo tofauti kama mpira na siasa.
Unasikia fulani ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi au Chama Cha Demokrasia na Maendeleo au vyama vingine. Ni mwanachama wa timu fulani Simba au Yanga na anakuwa na kadi na kutoa michango yote. Hapo naamini umepata picha nzuri ya uanachama.
Sehemu zingine kama siasa na michezo wanachama wanalipa ada na kupewa kadi ya uanachama. Lakini kwenye mauzo ada ya mteja ni manunuzi anayokuwa anafanya mara kwa mara. Na kadi ni bidhaa anazochukua. Na ndiyo hufanya arudi tena.
Sifa za mteja mwanachama;
Moja; Ni lazima awe amefanya malipo katika biashara yako zaidi ya mara moja.
Mbili; Ni mteja anayekupa ushirikiano wa kibiashara kwa namna moja au nyingine. Inaweza kuwa kupokea simu au kutembelea.
Tatu; Ameridhika na biashara ndiyo maana anaendelea kurudi kununua.
Mambo ya kuzingatia kutengeneza wateja wanachama;
Moja. Mpe thamani
Kitendo cha wateja kurudi tena kununua maana yake wamepata thamani waliyokuwa wanatarajia. Unaweza kuona hii ni ngazi rahisi kufikia, lakini utashangazwa jinsi ambavyo kwenye biashara nyingi wateja wananunua mara moja tu na hawarudi tena.
Mbili. Timiza ahadi
Lazima utimize yale uliyowaahidi kwenye manunuzi yao ya kwanza. Kitu kinachohitaji kazi ya ziada kuweza kuwashawishi wateja warudi tena kununua baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza.
Tatu; Kumfanya ajisikie vizuri
Mteja anapojisikia vizuri ni rahisi kuridhika. Anaporidhika ni rahisi kununua kwenye biashara yako mara kwa mara.
Muhimu; Wateja wanachama huwa ni rahisi kuendelea kuwauzia kwenye biashara maana tayari walishafanya maamuzi ya kuchukua bidhaa au huduma yako. Pia, ni rahisi kuwafanyia mauzo ya ziada kwa sababu unakuwa na baadhi ya taarifa zao.
Je, biashara yako inao wateja wangapi?
Ongea nasi hapa hapa kwa maoni na ushauri 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo.
Karibu tujifunze zaidi.