Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Njia Ya Kwanza Ya Kuwafanya Watu Wakukubali

Muuzaji bora kuwahi kutokea,

Kila mtu anapenda kukubalika na wengine, lakini wengi wamekuwa wanatumia njia zisizo sahihi ili kukubalika.

Ni kawaida watu kupenda kuwa na marafiki lakini wanapata marafiki wasio sahihi kwa sababu njia wanazotumia siyo sahihi.

Tunakwenda kujifunza ya kwanza kati ya sita za kutengeneza marafiki kwa kutumia njia hizi sita, tutawafanya watu watupende na kutukubali kutoka ndani ya mioyo yao.

Habari njema ni kwamba, njia ya kwanza ya kuwafanya watu wengine watukubali ni ; Wajali wengine kutoka ndani ya moyo wako.

Rafiki na muuzaji bora kuwahi kutokea,
Natumaini unamjua mbwa, sasa mbwa ndiye mnyama pekee anayefungwa na binadamu ambaye hana anachozalisha.
Kuku wanafugwa kwa sababu wanataga mayai na kutumika kama kitoweo.
Ng’ombe wanatoa maziwa na punda wanabeba mizigo.

Je, ulishawahi kujiuliza kwa nini mbwa hana anachozalisha lakini anapendwa, na kulishwa vizuri licha ya kuwa hana uzalishaji wowote.

Unajua ni kwa nini?

Hii ni kwa sababu mbwa, ana sifa moja, huwa anampenda na kumjali kweli anayemfuga.
Kwa mfano, mbwa akimuona mfugaji wake kwa mbali, hukimbilia na kumpokea vizuri.
Atamrukia rukia, atatikisa mkia atalialia vyote hivyo ni viashiria vya kuonesha anamjali na kumpenda ndani ya moyo wake.

Sisi kama wauzaji bora kuwahi kutokea, tunapaswa kujifunza kwa mbwa na itatusaidia sana kupata marafiki wengi zaidi.
Sifa hiyo tunajifunza kutoka kwa mbwa ni kuwajali wengine kutoka ndani ya moyo wako.

Wajali wateja wako, kutoka ndani kabisa ya moyo wako. Na wala usiigize kwani binadamu tuna mlango wa sita unaojua kama kile unachofanya kinatoka ndani au unaigiza kweli.

Kwa mfano, Yesu alikuwa ni muuzaji bora kuwahi kutokea.
Siku moja aliwahi kumuuliza mwanafunzi wake Petro, je, wanipenda, yale maswali yalimfanya Petro ashindwe kujizuia akalia na kumjibu bwana, wewe wajua yote.
Kitendo cha kulia kwa Petro, kinaashiria kwamba, Petro alimpenda bwana wake upeo na  ilitoka ndani ya moyo wake kabisa.

Mfano, mume au mke, wanaopenda kweli, kila mmoja atampenda mwenzake na kumjali kweli kutoka ndani ya moyo bila kumuumiza.

Ukiwajali wateja wako, kutoka ndani ya moyo wako, nao watakua tayari kujali biashara yako na kukupa zawadi ambayo ni kufanya manunuzi kwenye kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Mfano mwingine, kwa sasa tunaendesha program ya NGUVU YA BUKU, ni program ya bure na tunawapigia simu washiriki na kuwafuatilia wawekeze na kuwapa elimu elimishi juu ya fedha na uwekezaji kwa ujumla.
Kadiri ya uzoefu, wengine wanakufuata kikashani yaani inbox au kukupigia, kwa kweli mnatupenda na kutujali kutoka ndani ya mioyo yenu.
Yaani fedha ni zetu, manufaa ni yetu lakini mnatufuatilia, ni upendo wa hali ya juu ilihali hampati maslahi.

Kwa kutumia mifano hii tuliyojifunza leo, tunaona kwamba kama tukiwajali wengine kutoka moyoni kabisa wanajua na hii inatufanya kujenga ushawishi na kuwafanya watu wakukubali.

Kabla hujawataka wengine wakujali na kukubali, anza wewe kuwajali na kuwakubali. Hapa unakuwa unatumia silaha ya kwanza ya ushawishi ambayo ni kulipa fadhila, unaanza kutengeneza madeni kwao, kwa kuanza wewe kuwapa kile wanachotaka kisha na watakuwa tayari kukupa na wewe kile unachotaka. Kama unauza bidhaa au huduma atanunua tu kwa njia ya kulipa fadhila.

Muuzaji bora kuwahi kutokea, tukirudi kwenye asili ya binadamu ambayo ni ubinafsi, tunajifunza kwamba kila mtu huwa anajijali yeye mwenyewe kwanza.
Muda mwingi wa mtu huwa anautumia kufikiria mambo yake.
Hivyo basi, kama wewe utaonekana kumjali, basi atakukubali sana.

Hii iko wazi kabisa, kila mtu bila kujali kazi au nafasi yake, huwa anawakubali wale wanaomkubali na kumheshimu.
Kama unataka kutengeneza marafiki au wateja wengi basi unapaswa kuwajali, kwa kufanya vitu ambavyo vina manufaa kwao. Kwa mfano, maslahi yao, kuwapa elimu elimishi, kuwasaidia, kuwapigia simu, kufuatilia wateja na kuwa na nao vizuri kujua wanaendeleaje. Kifupi, MAUZO NI MAHUSIANO. Jenga ushawishi, imarisha mahusiano na wafanye wateja kuwa wako daima.

Hatua ya kuchukua leo; je unataka watu wakukubali?
Unataka kujenga ushawishi kwa wateja wako na wale wote ambao unahusiana nao?
Unataka kutengeneza marafiki wa kweli, kama unataka kuwasaidia wengine huku ukijisaidia wewe mwenyewe pia, basi shikilia msingi huu, wajali wengine kutoka ndani ya moyo wako.

Kitu kimoja zaidi,
Kuna vitu vidogo vidogo ambavyo ukivifanya vitawafanya watu wajue kweli unawajali na watakukubali.
Wasalimie watu kwa hamasa kubwa, wapokee wateja wako kwa shauku, tabasamu, onesha kufurahi kukutana nao.
Kadiri unavyowakubali watu kweli, ndivyo na wao wanavyokukubali.
Kumbuka kujifunza kutoka kwa mbwa na mfugaji wake na mara zote na wewe fanya hivyo kwa wateja wako na utauza mpaka watu watasema unatumia kizizi, nenda kayafanyie kazi haya maarifa na utakuja kutushukuru baadaye.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

Leave a comment