Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Matumizi Bora Ya Mwili Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Mwili wako ni rasilimali muhimu sana kwa mafanikio makubwa unayotaka kupata kwenye maisha yako. Mwili ndiyo nyumba yako ya milele, ambayo kama unataka kufanikiwa ni lazima uitumie vizuri. Na ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye mauzo, mwili imara unahitajika.

Warren Buffet amewahi kusema; fikiria umepewa gari moja tu ambalo ndiyo utaliendesha kwa maisha yako yote, hutaruhusiwa kuwa na gari nyingine yoyote. Je utaitunzaje hiyo gari ili iweze kuwa na manufaa kwako?

Anamalizia kwa kusema gari hiyo ni mwili wako. Umepewa mwili mmoja pekee ambao ndiyo utaishi nao kwa maisha yako yote. Cha kushangaza, watu wengi huwa wanatunza vizuri zaidi magari na mali zao nyingine vizuri kuliko wanavyotunza miili yao.

Hilo ni jambo la kushangaza, kwa sababu rasilimali nyingi ambazo watu wanaziheshimu na kuzitunza wanaweza kuzipata tena. Lakini rasilimali mwili ambayo watu wanaipuuza, wanayo moja tu na wakishaipoteza hawawezi kuipata tena. Hivyo basi, kama una kiu ya kupata mafanikio makubwa, kama upo tayari kuyafanya makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kutunza vizuri sana raasilimali yako ya mwili.

Mambo matatu muhimu ya kuzingatia kwenye matumizi ya mwili kwenye mauzo.

Ili kutumia vizuri rasilimali mwili na kufanikiwa kwenye mauzo, kuna mambo muhimu matatu ambayo unapaswa kuyafanyia kazi kwa uhakika.

Jambo la kwanza ni kutunza afya yako.

Afya ndiyo mtaji namba moja kwenye mafanikio yoyote unayotaka kuyapata. Bila ya afya bora, mipango mingine yote inashindwa. Watu huwa hawaoni umuhimu wa afya mpaka pale wanapoipoteza kwa kupata magonjwa sugu na ya kudumu. Hapo ndipo wanaona jinsi ambavyo kudorora kwa afya kunakuwa kikwazo kwao kuweza kuweka juhudi kubwa zinazohitajika ili kufanikiwa.

Mwili wenye afya bora ndiyo rasilimali muhimu kwenye kujenga kila aina ya mafanikio kwenye maisha.

Ili kutunza vizuri afya yako, kuna vitu vinne vya kufanya. 1. Unapaswa kuwa na ulaji mzuri na wa afya. Changamoto nyingi za kiafya, hasa za kuwa na uzito uliopitiliza zinaanzia kwenye ulaji. Ulaji wa vyakula vya wanga kwa wingi vimekuwa chanzo cha uzito uliopitiliza na kukaribisha magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la juu la damu (presha).

2. Unapaswa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya yako. Majukumu ya wengi siyo ya kuhusisha sana mwili bali akili. Hivyo chakula unachokula kinaweza kisiwe na matumizi makubwa sana. Kufanya mazoezi kunatumia chakula cha ziada ambacho kingehifadhiwa. Lakini pia kufanya mazoezi kunaimarisha kinga ya mwili na kumfanya mtu ajisikie vizuri.

3. Unapaswa kutenga muda wa kupumzika. Mwili wako unahitaji mapumziko ili kujifanyia maboresho mbalimbali. Hivyo unapaswa kutenga muda wa kulala ambao utakuwa tulivu ili upumzike vizuri.

4. Unatakiwa kujikinga na magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kukingwa. Hapa ni kuanzia magonjwa yanayoambukizwa, yasiyoambukizwa na hata ajali. Inapokuja kwenye afya, kinga ni bora na nafuu kuliko kinga. Usiwe mzembe na kujipeleka mwenyewe kwenye changamoto za kiafya ambazo zitakusumbua kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua; Tunza vizuri afya yako, huo ndiyo mtaji wa kwanza kwako. Kula kwa afya, fanya mazoezi, pumzika na jikinge na magonjwa.

Jambo la pili ni kulinda nguvu zako.

Unachotumia kwenye mwili wako ili kuweza kufanya makubwa ni nguvu unazokuwa nazo. Bila ya nguvu, mwili unakuwa hauwezi kufanya chochote kikubwa. Nguvu ya mwili wako ni kama chaji ya simu. Kama umeiweka simu kwenye chaji mpaka ikajaa, kila unapoitumia, chaji hiyo inapungua. Chaji inaenda ikipungua mpaka kufika sifuri na simu kuzima kabisa.

Kadhalika kwenye mwili, unapolala usiku na kuamka asubuhi, ni kuuchaji mwili wako. Unaamka ukiwa na nguvu kwenye mwili wako. Lakini sasa, kila unachofikiria na kufanya, kinatumia na kupunguza nguvu hizo. Mpaka unapofika tena kwenye mwisho wa siku, nguvu zako zinakuwa zimeisha na umechoka sana.

Kwenye kulinda na kutumia vizuri nguvu za mwili wako unapaswa kuweka vipaumbele kwenye mambo unayofanya. Yale mambo ambayo ni muhimu zaidi na magumu kufanya, unapaswa kuyafanya muda wa mapema wakati mwili bado una nguvu ya kutosha. Usikubali kuianza siku yako na mambo yasiyo muhimu, ambayo yanatumia nguvu zako na kukuchosha. Unapoanza na yale muhimu, unajiweka kwenye nafasi ya kupata mafanikio unayoyataka.

Ukianza na mambo yasiyo muhimu na kuchoka mapema, unajikuta ukiahirisha yale ambayo ni muhimu. Na hii siyo tu kwenye mambo unayofanya, bali pia kwenye fikra unazokuwa nazo na maamuzi unayoyafanya. Kadiri unavyofikiria mambo mengi na kufanya maamuzi mengi, ndivyo unavyochosha akili yako na kushindwa kufanya mengine muhimu. Hivyo unapaswa kupunguza mambo unayofikiria na maamuzi unayofanya ili uwe na nguvu za kuhangaika na yale muhimu.

Hatua ya kuchukua; weka vipaumbele sahihi kwenye mambo unayofikiri, kupanga na kufanya. Yale yaliyo muhimu zaidi yaweke kwenye mwanzo wa siku ambapo unakuwa na nguvu zaidi. Yasiyo muhimu yapeleke mwisho wa siku ambapo unakuwa huna nguvu.

Jambo la tatu ni kuwa na mwonekano mzuri.

Huwa kuna kauli inasema hatupaswi kuhukumu kitabu kwa mwonekano wa nje. Lakini kwa bahati mbaya sana, hiyo ndiyo tabia yetu binadamu. Huwa tunahukumu kitu kwa mwonekano wa nje. Na mbaya zaidi mwonekano wa mara ya kwanza ndiyo ambao watu huenda nao.

Kwenye mauzo hili lina nguvu kubwa ya kukufanya ufanikiwe au ushindwe. Kama muuzaji, wateja wanakununua wewe kwanza kabla hawajanunua kile unachouza. Wanakukubali wewe kwanza kabla hawajakubali kile unachowashawishi. Na vile wateja wanavyokuona kwa mara ya kwanza, ndivyo watakavyokuchukulia kwa maisha yao yote.

Hakikisha wewe nwenyewe unauzika na kukubalika na wateja kabla hujawauzia ulichonacho. Kuna matarajio ambayo wateja wanayo kwa muuzaji wa kila aina, hakikisha wewe unakuwa juu ya matarajio hayo.

Ili kuwa na mwonekano mzuri utakaokupa mafanikio kwenye mauzo na maisha kwa ujumla, zingatia haya matatu;

1. Vaa mavazi nadhifu muda wote. Mavazi nadhifu ni yale ambayo ni ya heshima na masafi. Epuka mavazi yanayowafanya watu wakuhukumu vibaya. Ni muhimu uwe na sare maalumu ya kazi ambayo unaivaa muda wote wa majukumu yako. Hilo linakusaidia usisumbuke sana ni nini uvae ili uwe na mwonekano mzuri.

2. Kuwa msafi muda wote. Zingatia sana usafi wa mwili wako kwa kuhakikisha nywele zako ziko vizuri, kucha zako na hata harufu ya kinywa na mwili. Hivyo ni vitu vidogo vidogo unavyoweza kupuuza, lakini vikakukwamisha sana pale wateja wanapokuwa hawajisikii vizuri kuwa karibu na wewe.

3. Mara zote vaa uso wa tabasamu bila ya kujali nini kinaendelea kwenye maisha yako. Tabasamu linawavutia watu kwako na kuwakaribisha. Watu wanajisikia vizuri zaidi pale wanapokuwa na mtu anayetabasamu kuliko wakiwa na ambaye hatabasamu. Pia tabasamu linaficha mambo mengi ambayo yangeweza kukukwamisha. Usijiruhusu mteja akuone ukiwa huna uso wa tabasamu kwa wakati wowote ule. Kwa sababu kile mteja anachoona mara moja, ndivyo anavyokuchukulia muda wote.

Hatua ya kuchukua; kuwa nadhifu kwa kuvaa sare za biashara ambazo ni safi, kuwa msafi wa mwili na mara zote tabasamu na utaweza kuutumia mwili wako kuuza zaidi.

Kwenye somo hili tumejifunza na kuona jinsi ambavyo mwili ni rasilimali muhimu sana kwa mafanikio yako kwenye mauzo na maisha kwa ujumla. Mwili tayari unao, haijalishi uliutumiaje huko nyuma, kwa kuwa bado upo hai, unaweza kufanya mabadiliko makubwa. Anza sasa kuyaweka kwenye matendo haya uliyojifunza hapa ili uweze kuutumia mwili wako kwa manufaa makubwa.

Kwa kuutumia vizuri mwili wako utaweza kuwa mtu bora na kisha muuzaji bora kuwahi kutokea. Huhitaji kuingia gharama zozote kubwa ili kutumia mwili wako kwa manufaa, anza sasa kwa yale ambayo ni ya msingi kabisa na utaweza kuutumia mwili wako kufanya makubwa sana.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora. Kocha Dr. Makirita Amani, Mkuu wa CHUO CHA MAUZO www.mauzo.tz

1 Comment

  • Faraji
    Posted December 18, 2023 at 6:00 am

    Inashangaza waajiliwa wanakuwa nadhifu kuliko wenye biashara

Leave a comment