Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Jinsi ya kupangilia usakaji kwa utembeleaji ili kupata matokeo mazuri.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, eneo la usakaji. Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tarajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

Kauli mbiu yetu ni; USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Ni kupitia kusaka ndiyo biashara inatengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi. Na biashara yenye wateja tarajiwa wengi, haiwezi kushindwa kufanya mauzo makubwa kama watafuatiliwa vizuri.

Njia ya kutembelea wateja na kukutana nao ana kwa ana ni moja ya njia zenye ushawishi mkubwa.

Ili usakaji wa wateja kwa njia ya kuwatembelea na kukutana nao ana kwa ana uwe na tija, lazima upangiliwe vizuri.

Kama usakaji hautapangiliwa vizuri, hautakuwa usakaji bali uzururaji. Mtu atazunguka sana, lakini hatapata matokeo mazuri.

Kitu kimoja muhimu sana cha kujua kuhusu usakaji kwa kutembelea, ambacho pia ndivyo kilivyo kwa mambo mengine ya mauzo, hutamtembelea mteja mara moja na ukapata unachotaka.
Ni lazima urudie rudie kumtembelea mteja mara nyingi mpaka upate kile unachotaka, iwe ni kupata taarifa zake kama mteja tarajiwa au kukamilisha mauzo.

Hivyo kwa mpango wako wa kutembelea wateja, unapaswa kuhakikisha unarudi kwa wateja mara nyingi mpaka upate unachotaka.

Hilo la kurudi kwa wateja ambao umeshawatembelea, linafanya kazi ya usakaji kwa kutembelea kuwa na majukumu mawili.
Moja kufikia wateja wapya ambao bado hawajafikiwa.
Mbili kuwarudia wateja ambao tayari walishafikiwa.

Bila ya kuwa na mpango mzuri, kuna wateja ambao watarudiwa mara nyingi, wakati wengine hawatafikiwa kabisa.
Ndiyo maana ili utembeleaji uwe na tija, lazima upangiliwe vizuri.

Kupangilia usakaji kwa utembeleaji kunahusisha vitu vitatu.

Moja ni kupanga siku na muda wa kutembelea.

Hiki ndiyo kitu cha kwanza cha kupangilia ili utembeleaji uwe na tija.
Kwa siku zako za kazi kwenye wiki, panga jinsi utakavyozitumia kwenye utembeleaji, ukizingatia jografia ya eneo husika.

Kulingana na wateja unaowalenga, shughuli zao na kule unakoenda kuwatembelea, utembeleaji hauwezi kuwa sawa kwa wote.
Unapaswa kutembelea kwenye siku na muda ambao utawakuta wateja wengi unaowalenga.

Kadiri unavyofanya utembeleaji na kupata taarifa, utaendelea kuboresha siku na muda wako wa utembeleaji.

Mbili ni kupanga maeneo ya kutembelea.

Ili usichanganye au kuwasahau wateja, unapaswa kupangilia maeneo yako ya kutembelea.
Kwa wateja unaowalenga na eneo unalotembelea, gawa kwa kanda na kila siku ya kutembelea ipe ukanda wake.

Unaweza kugawa kwa kanda za kaskazini, kusini, mashariki na magharibi. Au unaweza kugawa kwa kufuata ramani iliyopo, mfano barabara, mitaa, kata, tarafa n.k.

Lengo ni kwenye siku moja ya kutembelea unakuwa kwenye eneo moja tu na kulitembelea kwa uhakika.
Hiyo inaepusha kupoteza muda kutoka eneo moja kwenda eneo jingine la mbali kwenye siku moja ya utembeleaji.

Unapaswa kugawa eneo lako la utembeleaji kiasi kwamba kila wiki unapita sehemu mara moja.
Ukishapita kurudi tena ni mpaka wiki inayofuata.
Unawafanya watu wajue kabisa kwamba siku fulani ya wiki ndiyo unatembelea eneo lao, hivyo baada ya muda wanakuwa wanategemea kabisa utaenda.

Tatu ni kupanga unachokwenda kufanya wakati wa utembeleaji.

Usiamke tu na kwenda kutembelea wateja kama unafanya utalii.
Badala yake weka mpango wa nini unaenda kufanya, siku moja kabla hujaenda kutembelea.

Panga wateja ambao ulishawafikia na ambao utawarudia tena, ukijua kabisa nini unaenda kuwaeleza au kuwashawishi wanunue.
Pia panga wateja wapya utakaowafikia ambao bado hujawafikia na kujua nini unaenda kuwaambia.

Unapoenda kutembelea, kulingana na ratiba ya siku, hakikisha unatoka na sababu za kurudi tena eneo hilo siku kama hiyo wiki inayofuata.
Kwa kufanya hivyo kila wakati utakuwa na mpango mzuri wa nini cha kufanya kwenye utembeleaji.

Kwa kuweka mipango hii mitatu vizuri, utaweza kufanya utembeleaji wenye tija na kupata matokeo mazuri.

Mambo muhimu ya kuendelea kuzingatia kwenye utembeleaji.

1. Kuwa na ufuatiliaji endelevu kulingana na ahadi za wateja, usichoke wala kuacha.

2. Kila unapoenda kuwatembelea wateja, wape thamani hata kama hawajanunua. Wafanye wajifunze na kuwa bora zaidi kupitia wewe.

3. Kuwa na utembeleaji wenye msimamo kwa kila siku ya wiki kuwa eneo ulilopanga kiasi cha watu kuzoea na kutegemea uwepo wako.

4. Jenga mahusiano na watu maarufu wa kila eneo unalotembelea, hao wanaweza kukuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi unaowalenga, kwa rufaa au mapendekezo.

5. Unapoenda kutembelea mahali na ukakataliwa au kuambiwa usiende tena hapo, kajipange na urudi kwa namna tofauti ambapo utaongeza thamani zaidi kwao. Usikate tamaa kwa sababu umekataliwa, kama umeshaona kuna mteja tarajiwa, endelea na ufuatiliaji mpaka utakapompata.

Pangilia vizuri usakaji wako kwa njia ya utembeleaji ili uweze kuufanya kwa tija na kupata matokeo mazuri.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.

Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

Leave a comment