Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Mtazamo Sahihi Wa Kujijengea Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Kitu kimoja cha kushangaza sana kuhusu sisi binadamu ni kwamba huwa hatuoni vitu kwa jinsi vilivyo, bali tunaona vitu jinsi tulivyo sisi.

Ndiyo maana linaweza kutokea tukio mahali na mashuhuda wawili waliokaa karibu, kila mtu akaeleza kivyake na wakawa tofauti kabisa.

Hiyo ina maana kwamba, hakuna kitu kimoja kinachoweza kuonekana sawa kwa watu wote.
Mwonekano wa kitu chochote unaanzia kwenye mtazamo wa mtu.

Tunaweza kusema mtazamo ni sawa na miwani ambayo mtu amevaa.
Mtu akivaa miwani nyeusi, hata kama ni mchana wa jua kali, ataona ni usiku.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo, unapaswa kujijengea mtazamo sahihi.
Mtazamo ambao utakuwezesha kuweka juhudi kubwa na kuvuka kila aina ya changamoto unazokutana nazo kwenye safari ya mauzo.

Mauzo ni kazi nzuri na inayoweza kukupa chochote unachotaka. Ni kazi ambayo unaweza kuingiza kipato kisichokuwa na ukomo.
Lakini pia ni kazi yenye changamoto nyingi, ikiwepo kukataliwa na wateja.

Wauzaji wengi huwa wanakata tamaa mapema, ambapo kama wangeendelea kung’ang’ana kidogo tu, wangepata ushindi mkubwa.
Ili wewe usiwe mmoja wa wanaokata tamaa mapema, huu hapa ni mtazamo sahihi wa kujijengea kwa mauzo.

Mtazamo huo ni; MIMI NI MUUZAJI BORA KUWAHI KUTOKEA.

Huu ni mtazamo ambao umebeba vitu vingi ndani yake.

Moja ni UCHANYA.
Unapojiambia ni muuzaji bora kuwahi kutokea, unakuwa chanya juu yako mwenyewe na mauzo kwa ujumla.

Mbili ni UWEZEKANO.
Unapojiambia wewe ni bora, maana yake tayari unajichukulia kuwa bora, hivyo unakuwa kwenye hali ya uwezekano.

Tatu ni KUJIAMINI.
Unapojiambia ni bora, unakuwa unajiamini, kitu ambacho kitakuvusha kwenye mambo mengi.

Jinsi ya kujijengea mtazamo huo.

Mtazamo wowote kwenye maisha huwa unajengwa na vitu vitatu;
1. Taarifa.
2. Ushahidi.
3. Marudio.

Mtu anapata taarifa fulani, inayoambatana na ushahidi kisha kujirudia rudia kwa muda mrefu.

Ili kujijengea mtazamo wa MIMI NI MUUZAJI BORA KUWAHI KUTOKEA, fanya haya matatu;

Moja; ipe akili yako taarifa kwamba wewe ni muuzaji bora.
Kila siku andika, tamka na sikiliza sauti yako uliyorekodi ukisema; MIMI …. NI MUUZAJI BORA KUWAHI KUTOKEA.
Fanya hivyo mara nyingi kadiri uwezavyo kwenye siku yako, isishuke chini ya mara tatu, yaani asubuhi, mchana na jioni.

Mbili; tumia kila ushahidi kuweka uzito kwenye kauli yako ya MUUZAJI BORA.
Kwa kila hatua unayochukua kwenye mauzo, ihesabu kama ushindi kwako.
Umepiga simu kwa mteja, huo ni ushindi.
Umekamilisha mauzo, huo ni ushindi.
Umepata rufaa, huo ni ushindi.
Umemfuatilia mteja muda mrefu bila kukata tamaa, huo ni ushindi.
Muhimu; hesabu ushindi kwenye hatua ulizochukua na siyo matokeo uliyopata.
Hapo utakuwa na ushahidi mwingi sana kwamba wewe ni bora na utapata  msukumo wa kuendelea.

Tatu; rudia rudia kama kanda mbovu.
Rudia hatua hizo mbili kila siku na kila saa ya maisha yako.
Haijalishi unapitia nini, jiambie na jipe ushahidi.
Hata kama mambo ni magumu kiasi gani na huoni mbele, wewe jiambie ni bora na chukua hatua sahihi.
Ushindi huwa upo kwa wale wanaong’ang’ana hasa.
Kuwa mmoja wa hao, kwa sababu unaweza, na kwa sababu tayari wewe ni bora.

Tayari una uwezo mkubwa ndani yako wa kuwa vile unavyotaka, umechagua mauzo, hivyo tumia uwezo huo kuwa MUUZAJI BORA KABISA KUWAHI KUTOKEA.
Jijengee mtazamo huu uliojifunza hapa na utaweza kupata mafanikio makubwa kwenye mauzo.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

Leave a comment