Kwenye misingi ya kukubaliana na watu, somo lililopita, tulijifunza kanuni ya pili ya misingi ya kukabiliana na watu ambapo kwenye kanuni ya pili tulijifunza; toa sifa na shukrani za kweli na dhati.
Na habari njema ni kwamba leo katika misingi ya kukubaliana na watu, tunakwenda kujifunza kanuni ya tatu ambayo ni; tambua hitaji la msingi la mtu.
Rafiki yangu nikupendaye muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Unapoenda kuvua samaki kwenye ndoano yako, unaweka chambo. Wakati mwingine wewe mwenyewe hupendi hata wadudu unaowatumia kama chambo.
Lakini huwezi kupata samaki unaowataka bila ya kutumia wadudu hao.
Sina uhakika kama itakufaa lakini, ili kuvua samaki, lazima kwanza uwape kile ambacho wanakitaka, hitaji lao la msingi.
Hata kwenye mahusiano yetu na wengine, ndivyo hali ilivyo. Kama unataka watu wakubaliane na wewe au wafanye unachotaka basi anza kwa kutambua hitaji lao la msingi kabisa, kisha wape hitaji hilo.
Ibua ndani yao tamaa ya kupata hitaji hilo na waoneshe njia ya kukipata kupitia wewe.
Kwenye mauzo ili uweze kuuza, unapaswa ujali kwanza maslahi ya mteja wako.
Sisi binadamu kwa asili ni wabinafsi hilo wala halina ubishi. Huwa tunaangalia tunapata nini kwanza ndiyo tunawajibika bila hivyo, watu hawajigusi.
Kwa kuwa wewe ni muuzaji na unashughulika na watu unapaswa kwanza kujali maslahi ya mteja wako.
Angalia mteja wako anapata kwanza matokeo anayotaka kisha na wewe utapata.
Mteja anakuwa na swali kichwani kwake, kama nikinunua spea za pikipiki kwako ninapata nini? Kama nikinunua maziwa yako ninapata nini? Kama nikinunua vifaa vya ujenzi kwako nini cha ziada nitapata kwako?
Kama nikinunua simu kwako ni zaidi nitapata?
Kama nikifanya biashara ya skepa na wewe nitapata nini cha ziada ukilinganisha na kule kwa awali?
Mteja anataka kuona anapata matokeo gani akinunua bidhaa au huduma unayotoa?
Kwa kulijua hilo uwe mtu wa kujua hitaji la ndani kabisa la mtu linalomsukuma kuchukua hatua ya kununua.
Waambie wateja kuwa ukinunua bidhaa yetu unapata matokeo haya moja, mbili, tatu na mteja atashawishika kununua na siyo kumpa mteja sifa za biashara yako.
Kumbuka, sifa haziwezi kumsaidia mteja kutatua changamoto zinazomkabili, bali mteja anataka matokeo au suluhisho juu ya kile kinachomsumbua.
Usiangalie kwanza hitaji lako, bali angalia mteja atawezaje kunufaika na kile unachouza au huduma anayotoa. Ukiweza kujua hitaji la msingi lililo ndani ya mtu, na kisha kulichochea, mtu huyo atakuwa tayari kufanya unachotaka afanye.
Kabla hujaangalia utanufaikaje kwanza wewe, fikiria kwanza mteja wako atanufaikaje. Kuwa na msukumo wa kutaka kutimiza hitaji la msingi la mteja.
Na wala usiwe na wasiwasi, kwamba vipi kama nikijali sana maslahi ya mteja mimi nitanufaikaje? Utanufaika, mteja wako akishiba na wewe utashiba. Wewe unataka samaki halafu hutaki kuweka chambo. Wape samaki hitaji lao la msingi ambalo ni chambo na wewe utapata samaki.
Hata kwenye kuuza kitu chochote, utaweza kuuza zaidi kama utajua hitaji la msingi ambalo mtu analo, labda changamoto au maumivu anayoyapata, kisha ukamwonesha jinsi kile unachomuuzia kitamsaidia kuondokana na maumivu hayo, atakua tayari kununua.
Kumbuka, ukimweleza mtu kuhusu sifa za kile unachouza, haitamsukuma lakini, ukimwonesha jinsi kinamnufaisha, hasa kwenye hitaji lake kuu, atasukumwa kununua.
Kitu kimoja zaidi, unapaswa kufanya hili kwa uaminifu mkubwa. Usiwadanganye watu kwamba watapata hitaji lao la msingi na baadaye wasilipate.
Mara zote kuwa mwaminifu na ahidi kile unachoweza kutekeleza na kuwa na nia ya kweli ya kumsaidia mtu kile anachotaka kweli.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz