Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Fanya Yaliyo Muhimu, Utapata Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako

Alikuwepo bwana mmoja Mr. Ton huyu alikuwa fundi mzuri katika kushona nguo. Ton alikuwa analalamika sana kuhusu kazi kuwa kubwa na haoni matokeo.

Anasema; wakati anashona nguo moja, ikitokea anakuja mteja hiyo anaiacha na anaikimbilia mpya. Mwisho wa siku anajikuta amechoka sana kwa kufanya kazi nyingi. Ila akijaribu kupima uzito wake anaona nguvu aliyotumia ni kubwa kuliko matokeo aliyopata.

Mr. Ton aliona ni vema kumtafuta mtaalamu wa masuala na maendeleo binafsi (Personal Develepment Issues) ili aone kama anaweza kupata msaada.

Siku ilifika, mtaalamu akaonana nae. Ton akajielezea namna anavyotaka asaidiwe. Mtaalamu alimsikia vizuri, akamwambia sentensi moja; “Naomba ukimaliza kazi zako leo, niandikie vitu vitano na vikiwa sita sio mbaya unavyoenda kufanya kesho”.

Ton akamuangalia mtaalam na kumuuliza; “Ina maana kukuita kwangu kote hapa na malipo ninayokupa, hiki ndo umeona kinaweza kunisaidia?” Mtaalamu akamwambia, naomba usinipe pesa yako. Ila hivi vitu vitano nilivyokwambia wewe nitumie. Kisha, endelea kufanya hivyo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi mitatu. Ukimaliza utaniambia nafaa kulipwa au kukulipa.

Ton alilalamika sana kwa kutosikia neno la hamasa na pole kutoka kwa mtaalamu. Kwa mbinde sana, Ton akakubali kufanya kama alivyoambiwa. Akilini mwake alifanya kama kumkomoa mtaalamu. Kweli, vitu vitano au sita tu ndo nifanya kila siku? Mh! Hapa nimekula kamongo. Haya! Ngoja nifanye, nione.

Kesho yake akamtumia orodha ya vitu hivyo. Siku hiyo ya kwanza akafanikisha kufanya vitu vinne pekee. Siku iliyofuata alifanikisha vitu vitatu. Baada ya wiki moja, Ton akaangalia kwenye orodha yake. Akagundua bado hata hivyo sita hajavifanya katika kiwango kizuri na kila akipanga havimalizi. Akaamua kuweka nguvu kwenye kuzingatia orodha yake.

Siku inapoisha, anapitia kuona kama alivyokamilisha ni kweli au la. Baada ya mwezi mmoja kuisha, aligundua vitu vingi sana. Na ilipofika miezi mitatu alikuwa na maendeleo mazuri. Kwanza, alianza kuiona kazi yake kama inampa matumaini kifedha na mambo ya muhimu angalau yalikuwa yanafanyika. Hii ni kwa sababu alikuwa anaenda na namba zake za siku.

Baada ya hapo aliomba kuonana na mtaalamu kwa ajili ya kupata mrejesho na ushauri mwingine. Mtaalamu alikubali ombi lake na akaja tena ofisini kwake Ton. Mazungumzo yalianza huku Ton akianza kuomba samahani kwa maneno makali aliyotamka siku ile. Akasema, mwanzoni nilichukulia kama kitu cha hovyo kisicho na maana lakini nilivyoanza kufanya, niliona ugumu na umuhimu wake.

Siku zilivyoenda, nikawa ninapata unafuu. Najikuta hata muda wa kupumzika ninaupata. Kitu ambacho hapo awali hakikuwepo. Nilikuwa “bize” asubuhi hadi jioni. Nashona nguo hii, haijaisha nashona hii. Hali iliyofanya nisimalize nguo kwa wakati. Wateja walinilaumu sana na baadhi ya pesa nilizikosa.

Huwezi amini, mke wangu Mama Queen anashangaa ninaenda mapema nyumbani huku nikiwa sina kazi nyingi za kufanya tofauti na hapo awali. Kwa kweli, ninakushukuru sana.

Naomba tu nikupe hiki kiasi cha pesa kama shukurani. Umenisaidia pakubwa. Naomba uwe unafuatilia maendeleo yangu, nitakulipa kiasi utakachoniambia. Mtaalamu akampongeza Ton na kazi ikaendelea.

Huenda na wewe unapitia hali kama aliyokuwa anaipitia Ton. Japo wewe sio Ton kuna duka unauza, kuna huduma unaitoa. Ukiwa eneo lako la kazi siku yako inakuwa na vitu vingi ambavyo mwisho wake ukiangalia namba zako hazikai sawa. Ni maeneo machache yamefanyika. Inafika mahali unakosa hata muda wa kukaa na ndugu, jamaa au familia yako. Muda wote umechoka. Wakati ndio huu.

Fanya mambo yaliyo muhimu kwanza. Simaanishi mengine sio muhimu, hapana. Kama upo dukani mambo muhimu ni kuongea na mteja ana kwa ana au kuwasiliana na wateja. Vitu zaidi ya hapo sio muhimu sana katika kuongeza mauzo.

Kuweka orodha ya mambo unayoenda kuyafanya kwa siku ni kitu muhimu zaidi. Maana kinakusaidia kuitawala siku yako. Wengi wetu tumezoea kusema vitu vyangu navijua kichwani. Sikia, “wino uliokauka ni bora kuliko akili” kwa sababu akili inaweza kusahau lakini wino ulioandikwa tayari hauwezi kuondolewa.

Kuweka orodha ya mambo unayoenda kufanya kwa siku sio zoezi jepesi, maana wengi wetu hatuna mazoea. Ni zoezi linalohitaji msukumo na ufuatiliaji wa mara kwa mara. Ukifanikisha hili, utakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mambo yako yasonge mbele.

Siku ya leo unapomaliza kusoma au kusikiliza somo hili, anza kuweka orodha ya mambo unayoenda kufanya kwa siku yako, inayofuata ili yakusaidie zaidi.

Kwenye orodha yako zingatia;

Mbili; Weka vipaumbele
Kipi kianze kufanyika na kipi kifuate baada ya hicho. Weka akilini kuwa, vipaumbele sio suala utakalokuwa wa kwanza kulifanya. Halijaanza leo wala jana, lilianza muda mrefu tangu enzi za uumbaji na Mungu.
Wakati wa uumbaji, Mungu hakuumba kila kitu kwa siku moja.

Alitafuta kitu kikubwa ambacho kitaweza kutegemewa na kila kitu atakachoumba. Kuna wakati nawaza kama angeanza na wanyama au binadamu ingekuwaje, sio kwa giza hilo. Na hapakuwepo na maji wala kitu chochote. Hata wewe vipo vipaumbele muhimu kuvifanyia kazi.

Mbili; Usihifadhi kitu au kuacha hewani
Kuwa na vipaumbele bado hakukusaidii kutawala siku yako ikiwa wewe ni mtu wa kuachia vitu hewani.Hupaswi kuacha kitu hewani au kukihifadhi kwa ajili ya baadaye. Tafiti zinaonyesha kwamba; asilimia 80 ya vitu ambavyo watu wanahifadhi kwa ajili ya baadaye huwa hawavitumii au kuvifanyia kazi tena. Lakini bado watu huwa wanajidanganya kwa kuhifadhi vitu kwa ajili ya baadaye.

Tatu; Muda.
Kila mmoja anazo saa 24, ndani za saa hizo kuna mambo mengi muhimu yanapaswa kufanyika. Vipaumbele unavyoweka lazima viende sambamba na muda.

Nne; Mahitaji.
Kitu kinaweza kuwa kinahitajika sasa je, kipo ndani ya kipaumbele au hitaji letu muda huo? Lazima ulijue hili vema.

Je, ni mambo yapi muhimu unayafanyia kazi ili kuitawala siku yako?

Fanyia kazi uliyojifunza katika somo hili.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi.
Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.
Karibu tujifunze zaidi.

Leave a comment