Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Jinsi Ya Kujua Maumivu Ya Mteja Na Kumshawishi Kununua

Maumivu ni kile kinachomfanya mteja kufika katika eneo lako au ni kitu kinachomuumiza zaidi. Hakuna mtu anaweza kuacha maduka au sehemu zingine zote na kuja kwako bila kuwa na uhitaji wa kitu.

Labda wewe ushindwe tu kuongea naye na kujua kinachomsibu. Mfano mzuri tuchukulie mtu anayeumwa labda malaria au kichwa. Ili apate suluhisho anapaswa kwenda hospitali au duka la dawa.

Ili uweze kumshawishi mtu huyo kununua, unapaswa kujua maumivu aliyonayo na kuyagusa hayo wakati unazungumza naye.

Maumivu huwa yanajificha nyuma ya hisia anazokuwa nazo mtu. Kwa kuzijua hisia hizo kwa mteja na kuzitumia, unakuwa umegusa maumivu yake na kuweza kuwashawishi kununua.

Kwa mtu anayeumwa kichwa au malaria lazima atakuwa anaongea kwa unyonge sana, kazi kwako muuzaji kumsikiliza na kumuuliza maswali. Bila kujua hasa nini kinamuumiza akili hutoweza kumshawishi kununua.

Sisi binadamu huwa ni viumbe wa kihisia zaidi, tunapenda kujiona kwamba tunafanya maamuzi yetu kwa kufikiri kwa kina. Lakini huo sio kweli, huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia na kuyahalalisha baadaye.

Kama mtu unakipenda kitu, utakikubali kwanza, halafu ndiyo utaanza kuangalia sababu za kukikubali. Kama hutaki kitu, utakikataa kisha kutafuta sababu za kukikataa.

Kama muuzaji unayetaka kumjua mteja, hili ni jambo muhimu sana unalopaswa kulijua sio tu kwenye mauzo, bali kwenye maeneo yote ya maisha yako. Pale unapotaka kuwashawishi mtu, anza kwa kugusa hisia zake.

Ndiyo maana mtu anapotaka kukuibia huwa anaanza kuteka hisia zako. Anakwambia ukilipa hii utapata hiki ndani ya muda mfupi utakuwa umepata pesa nyingi zaidi. Kwa kuwa pesa ni eneo linaloleta msisimko mkubwa mtu unapolisikia unajaa.

Unapojaa unakuwa na uwezo mkubwa kukushawishi na kukuibia pesa zako. Ukweli ni kwamba hisia zikiwa juu kiwango cha maamuzi sahihi kinakuwa kipo chini.

Chukua mfano huu, mtu anataka kukupa Elfu kumi ya ziada, anakupa shilingi uirushe hewani. Utachagua upande utajitokeza juu, iwe ni kichwa au mkia.

Ukirusha shilingi hiyo na upande uliochagua ukijitokeza juu, anakupa sh. Elfu kumi. Lakini kama utarusha shilingi hiyo na upande utakaojitokeza juu ukawa tofauti na ule uliochagua basi wewe utapaswa kutoa sh.elfu kumi. Je utakubali kucheza mchezo huo? Jibu lipo wazi ni hapana.

Unataka kujua kwa nini? Kwa sababu maumivu ya kupoteza elfu kumi uliyonayo ni makubwa kuliko raha ya kupata elfu kumi nyingine.

Ndiyo maana Dale Carnegie aliwahi kusema: “Kuna njia moja pekee ya kumshawishi mtu afanye kitu chochote. Njia hiyo ni kumfanya atake kufanya kitu hicho. Kumbuka hakuna njia nyingine.” Njia hiyo ni kumpa kitu anachotaka.

Huo ndiyo msingi mkuu wa kuwashawishi watu wafanye chochote kile, kwa kuwafanya wao wenyewe watake kufanya kitu hicho. Na njia ya kuwafanya watu watake kufanya kitu chochote kile ni kugusa hisia zao.

Kwa kuwa watu hufanya maamuzi kwa hisia, unapogusa hisia sahihi kwa watu, unawafanya wao wenyewe watake kufanya kitu, ili wapate wanachotaka au wasipoteze walichonacho.

Take away point za jinsi ya kujua maumivu ya mteja na kumshawishi;

Moja: Uliza Maswali.
Uzuri wa maswali yanamfanya mtu aongee. Mtu akiongea ukiwa mdadisi ni haraka kujua maumivu yake.

Mbili; Msikilizaji Mzuri.
Mtu akiwa anaongea na wewe ukawa umasikiliza ni rahisi kujua kinachomuumiza. Kwenye maumivu ndipo unapoweka nguvu. Mwishowe anashawishika kununua.

Tatu; Jali Maslahi ya mteja.
Kila mtu kuna kitu anataka, kazi yako ni kumsaidia kupata kitu hicho. Anapoona unaelekea kumsaidia lazima akuonyeshe jinsi gani anataka kitu hicho.

Nne; Msaidie Kufanya Maamuzi.
Kwenye mauzo kamwe usimlazimishe mteja kuchukua bidhaa yako bali msaidie. Mweleze namna anavyoenda kupata matokeo kupitia huduma au bidhaa yako.

Ukizingatia mambo hayo utajiweka kwenye nafasi kubwa ya kumshawishi mteja na kumuuzia.

Àsante sana, karibu tujifunze zaidi.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mkufunzi, Mjasiriamali na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 kwa masomo na ushauri na kupata vitabu vyetu. Kama;
MAUZO NI HUDUMA
MAUZO NI RAHA
MAUZO NI MAHUSIANO
MAUZO NI MCHEZO WA NAMBA.
CHUO CHA MAUZO.

Pia, karibu Chuo Cha Mauzo Tanzania. Huku tunafundisha mafunzo ya mauzo kwa vitendo. Lengo kuu ni kukuza mauzo angalau mara mbili kwa mwaka.

1 Comment

 • Miraji abdallah
  Posted November 23, 2023 at 5:14 pm

  _unapotaka kumshawishi mtu Anza kwa kugusa hisia zake
  _ili uweze kujua tatizo au maumivu ya mtu muulize maswali pia msikilize kwa umakini mkubwa , utajua na utaweza kumshawishi kununua
  _Hisia zikiwa juu kiwango Cha kutoa maamuzi sahihi kinakuwa chini
  _Msaidie mteja. mweleze namna anavyokwenda kupata matokeo kupitia huduma au bidhaa yako
  ASANTE . MKUFUNZI LACKUS ROBERT.

Leave a comment