Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye sehemu nyingine ya masomo ya Usakaji.
USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.
Hiyo ndiyo kauli mbiu yetu ya usakaji ambayo tunaiishi na kuifanyia kazi.
Kwenye somo hili tunajifunza kikwazo kikuu cha ukuaji wa mauzo na jinsi ya kukivuka ili tuweze kufanya mauzo makubwa zaidi.
Kwenye falsafa kumekuwa na swali moja ambalo limekuwa linaibua mijadala mbalimbali.
Swali hilo linasema; Kama mti umedondoka msituni na hakuna mtu ambaye alikuwepo wakati mti huo unadondoka, je mti huo unakuwa umetoa sauti?
Kwa maneno mengine swali linauliza kama kitu kimetoa sauti, lakini hakukuwepo na mtu wa kusikia hiyo sauti, je hiyo sauti imetoka?
Hili ni swali ambalo tunaweza kujiuliza kwenye mauzo na kama tutajijibu vizuri basi tutaweza kufanya mauzo makubwa.
Watu wote huwa tunaingia kwenye biashara kwa kudhani.
Tunakuwa na dhana mbalimbali juu ya kile tunachouza na hitaji la soko.
Kwa mfano unakuwa na bidhaa au huduma ambayo unadhani watu wanaihitaji.
Lakini soko linavyokwenda ndiyo litatupa mrejesho kama dhana zetu ni sahihi au la.
Hivyo basi swali linakuwa, kama una bidhaa au huduma ambayo unadhani watu wanaihitaji, umeingia kwenye biashara lakini watu hawainunui, je wanaihitaji?
Swali jingine ambalo ndiyo tutajadili leo ni kama umeingia kwenye biashara ukiwa na bidhaa au huduma ambayo ina uhitaji, maana yake umeshapata watu ambao wananunua, lakini hufanyi mauzo makubwa, je unajulikana kama upo?
Rafiki yangu muuzaji, kikwazo kikuu cha ukuaji wa mauzo ni KUTOKUJULIKANA.
Watu wengi waliopo kwenye biashara huwa wana bidhaa na huduma ambazo watu wanazihitaji.
Lakini wanaojua kuhusu uwepo wao wanakuwa ni wachache sana, kitu kinachofanya mauzo kuwa madogo pia.
Kutokujulikana ni kikwazo kikubwa kwenye ukuaji wa mauzo.
Kwenye zama tunazoishi sasa, biashara zinazouza zaidi siyo zile zenye bidhaa bora kuliko nyingine, bali zile zinazojulikana zaidi ya nyingine.
Zama za kuwa na bidhaa au huduma bora pekee na watu kukutafuta popote ulipo zimeshapitwa na wakati.
Kwenye zama hizi za kelele na usumbufu, watu wamevurugwa na hawana utulivu.
Itawachukua muda mrefu sana kwa wao kujua kuhusu uwepo wako kama hutachukua hatua za makusudi ili kujulikana.
Jinsi ya kuondokana na kikwazo cha kutokujulikana.
Njia pekee na ya uhakika ya kuondokana na kikwazo cha kutokujulikana ni kufanya USAKAJI kwa ukubwa na msimamo bila kuacha.
Na kwa sababu zama tunazoishi sasa ni zama za kelele, basi na wewe unapaswa kupiga kelele nyingi na kubwa sana.
Wajibu wako namba moja kama mfanyabiashara na muuzaji ni kuhakikisha kila anayeweza kunufaika na kile unachouza anajua kuhusu uwepo wako na jinsi anavyoweza kunufaika.
Hii ni kazi kubwa, inayohitaji mtu kuamini na kuifanya kwa imani na ukubwa.
Kwa sababu watu ambao hawajui kuhusu biashara yako ni wengi sana kuliko wale wanaoijua.
Na hii ndiyo maana kauli mbiu ya usakaji kwenye CHUO CHA MAUZO ni kitu cha kufanya mara zote bila kuacha.
Kinachowakwamisha wengi kupiga kelele.
Inaeleweka wazi kwamba watu hawawezi kununua kwako kama hawajui uwepo wako na manufaa wanayoweza kupata.
Na pia ushahidi unatuzunguka kila mahali, kwa kuanza na kampuni ya simu unayotumia, kila mara wanakuletea jumbe mbalimbali, ambazo hata huzihitaji.
Lakini bado wafanyabiashara na wauzaji wengi wamekuwa hawapigi kelele zinazowawezesha kuwafikia wengi zaidi.
Hiyo ni kwa sababu wanajiona wao ni wastaarabu na hawataki kuwasumbua watu.
Hivyo wakishawaambia watu mara moja kuhusu kile wanachouza, hawawaambii tena kwa kuona tayari wanajua.
Wanadhani wakiwaambia watu kitu mara moja basi watakumbuka milele.
Kinachowashangaza ni pale wanapokutana na mtu ambaye walishamwambia wanachouza akiwa amenunua kwa mtu mwingine.
Wanapowauliza kwa nini wamenunua pengine ambacho wewe unauza, majibu ndiyo yanawashangaza.
Watu hao wanawajibu kwamba hawakujua kama wanauza kitu hicho.
Na hapa ndipo tunaporudi kwenye swali la kifalsafa tuliloanza nalo; kama umewaambia watu kile unachouza ila wakaenda kununua kitu hicho hicho kwa mtu mwingine, je wamekusikia?
Jibu ni hawajakusikia.
Na hatua ya kuchukua ni kupiga kelele zaidi.
Tumekuwa tunaambiana hili mara kwa mara na tutalirudia tena hapa, ustaarabu pekee kwenye biashara ni kuuza.
Kama huuzi, huna ustaarabu, hata kama unajifariji kiasi gani.
Hivyo unapaswa kufanya kila kilicho sahihi kuhakikisha unauza.
Na kwa zama hizi za usumbufu wa kila aina, lazima upige kelele nyingi sana ndiyo uweze kusikika na kuuza kwa wingi.
Hizo kelele tunazozungumzia ni zipi hasa?
Unaposikia kuhusu kupiga kelele kwenye mauzo ni kufanya usakaji mkubwa na kwa msimamo bila kuacha.
Ni kutumia kila njia inayoweza kutumika kuhakikisha unawafikia wale wanaoweza kunufaika na kile unachouza.
Inaweza kuwa kwa kuomba rufaa, kuwatembelea, kuwapigia siku, kuwatumia jumbe, kuwapa maudhui, kuungana nao kwenye mitabda na nje ya mitandao.
Na njia kubwa zaidi ya kupiga kelele ni kufanya matangazo ya kulipia ambayo yanawafikia wengi zaidi kwa haraka.
Ili ufanye mauzo makubwa, lazima upige sana kelele.
Lazima kila siku watu wapya wajue kuhusu uwepo wako na kile unachouza.
Lazima wale ambao wameshasikia lakini bado hawajawa na imani ya kununua waendelee kukusikia ili kujenga imani zaidi.
Lazima wale ambao wameshanunua warudi tena kununua na kukuletea wengine nao wanunue.
Na lazima wale ambao walikuwa wananunua huko nyuma ila wakaacha kwa sababu zozote zile warudi tena kununua kwa kukusikia upya.
Hatua za kuchukua.
Ondoka kwenye somo hili ukiwa umedhamiria kupiga kelele kubwa sana kwenye kile ambacho unauza.
Dhamiria kuhakikisha kila anayeweza kunufaika na unachouza anajua kuhusu uwepo wako na kushawishika kununua.
Kataa kujifariji na ustaarabu usio sahihi, ustaarabu pekee kwako ni kuuza na kupiga kelele ni sehemu ya ustaarabu huo.
Kubaki kwamba kama hawajajujua, basi hawajasikia, hivyo kelele hazijatosha, unapaswa kuziongeza zaidi.
Kubali kwamba kwa maisha yako yote utakuwa mpiga kelele. Utawapigia watu kelele kabla hawajajua hata kama upo, utaendelea kuwapigia kelele mpaka wanunue.
Na hata baada ya kununua, utaendelea kuwapigia kelele kwa maisha yao yote.
Kila unapotaka kujidanganya kwamba hupaswi kupiga sana kelele, angalia makampuni makubwa na yenye wateja wengi.
Kila siku utakutana na matangazo mengi ya makampuni hayo.
Huwa hayaachi kupiga kelele kwa sababu yanajua hicho ndiyo kimewafikisha pale walipo sasa.
Piga sana kelele, kama watu hawanunui kwako, hawajui kuhusu uwepo wako. Na njia pekee ya kuhakikisha wanajua na kununua ni kwa kupiga kelele kwa wingi na ukubwa, kwa msimamo bila kuacha.
Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz