Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Misingi Ya Kukubaliana Na Watu Kanuni Ya Pili

Kwenye misingi ya kukubaliana na watu sehemu ya kwanza tulijifunza USIKOSOE KUHUKUMU au KULAUMU.
Kwa njia ya kukosoa, kulaumu au kuhukumu hakuna tunachopata zaidi kupoteza.
Kama unataka kupata asali basi usipige mzinga.

Habari njema ni kwamba leo kwenye kanuni ya pili ya misingi ya kukabiliana na watu tunakwenda kujifunza kanuni ya pili ambayo ni, toa sifa na shukrani za kweli na za dhati.

Njia ya kuhakika ya kuweza kuwashawishi watu wafanye unachotaka au wakupe unachotaka ni kuwafanya wawe tayari kufanya hivyo.

Kama unataka kitu kutoka kwa watu, usitumie nguvu na mabavu kuwalazimisha watu wafanye au wakupe wanachotaka  lakini njia hizo zitakuja na madhara baadaye.

Njia pekee ya kuwafanya watu wawe tayari kukupa wewe kile unachotaka ni kwa wewe kuanza kuwapa kile wanachotaka.

Unaweza kujiuliza je, watu wanataka nini?
Na majibu Yako wazi, majibu yamekuwa yanashirikishwa na wengi;

Mwanasaikolojia Sigmund Freud amewahi kusema kile ambacho mtu anafanya kinasukumwa na tamaa mbili, ngono na ukuu.
Watu wanasukumwa kwa kupata ukuu , hivyo basi wewe kama muuzaji wape watu ukuu kwa kuwasifia ili upate kile unachotaka.

Mwanafalsa John Dewey aliwahi kunukuliwa akisema, hitaji la kuu la kila mtu ni kutaka kuonekana wa muhimu.

Abraham Lincoln amewahi kusema kila mtu anapenda kusifiwa. Huku William James akisema kanuni kuu ya asili ya binadamu ni kutaka kuthaminiwa.

Watu wengi wanapenda kuthaminiwa, kusifiwa na kuonekana ni wa thamani.
Hili ndiyo hitaji ambalo limekuwa linatusukuma kufanya yale tunayofanya kwenye maisha yetu ya kila siku.

Kwahiyo, wewe kama muuzaji unapaswa kujua kwamba,  kila mmoja anataka kukubalika na kusifiwa na wengine.
Kama tukiweza kuwapa watu kitu hicho, basi watakuwa tayari kwa hiari yao, kufanya au kutupa kile tunachotaka.

Tunaishi na watu, na waswahili wanasema, ongea na watu ili uvae viatu.

Kitu kimoja zaidi, njia rahisi ya kuwakubali na kuwafanya watu wajione ni wa muhimu ni kushukuru.
Watu wamekuwa wanafanya vitu kwa ajili yetu lakini tunasahau kuwashukuru.
Kitendo cha kuwasifia na kuwashukuru inawafanya wajisikie ni wa muhimu na wanakubalika.

Hatua ya kuchukua leo; wasifie wateja wako, wafanye wajione ni wa muhimu na watakuwa tayari kukupa kile unachotaka kutoka kwako.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

Leave a comment