Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Watu Hukunua Wewe Kabla Ya Bidhaa Yako; Jiuze Wewe Kwanza

Wateja wanapofika katika eneo lako, kitu cha kwanza kuwavutia ni mwonekano wako, maneno unavyoongea, tabasamu unaloonyesha mbele ya mteja. Ndivyo humfanya anunue.

Ukweli ni kuwa mauzo ni kitu muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu, hii ni kwa sababu kila mtu kuna kitu anauza. Iwe ni kwenye biashara, kazi au maisha ya kawaida, kuna kitu ambacho mtu unataka wengine wafanye, hayo ndiyo mauzo.

Sehemu kubwa ya maisha ni sisi wenyewe kuuza mwonekano wetu na hoja au sera zetu, hili ndiyo zoezi la kujiuza. Ili watu waweze kukubaliana na wewe kwenye kile unachouza, unahitaji kuwa na mbinu bora kabisa za mauzo.

Neno kuuza linavyotumika katika hapa sio kwamba wewe ni bidhaa kama zilivyo nyanya au vitunguu. Bali, yale maarifa na ujuzi ulionao katika kuwashawishi watu. Hayo ndiyo unayouza. Kwanini wauzaji wengi hatuuzi kwa viwango vya juu? Tupate simulizi kidogo kuna kitu cha kujifunza kuhusu mada ya leo;

“Ilikuwa siku ya Ijumaa asubuhi, katika kampuni moja ya uchimbaji wa madini. Wafanyakazi walikuwa ndio wanaingia kazini. Utaratibu wa pale ilikuwa kila ukiingia unaenda kusaini kwanza katika daftari la mahudhurio. Kisha, unaelekea eneo lako la kazi.

Wafanyakazi walipofika sehemu ya kusainia, kuna andiko waliona. Lile andiko lilikuwa linasema; “ANAYEKWAMISHA MAENDELEO YAKO AMEFARIKI JANA”. Tafadhali elekea Block C ndipo mwili ulipo na shughuli ya kumuaga inafanyikia”.

Kila aliyesoma tangazo lile, alifurahi sana. Kwamba anayekwamisha mafanikio yake amefariki. Matarajio makubwa ya kufanikiwa yakawa yanawajia. Lakini swali likabakia; atakuwa ni nani huyu, ni bosi, msimamizi wangu au rafiki yangu?

Kila mmoja aliwahi kufika eneo waliloelekezwa. Huku shauku kubwa ikiwa ni kumuona huyo anayezuia mafanikio yake. Wakakuta walinzi wako pale kwa ajili ya kutoa maelekezo. Kila mmoja akafika na kuketi, huku wakisubiria maelekezo. Ukimya ukiwa umetawala kila mmoja anamuangalia mwenzake kama yupo.

Baada ya muda mfupi wakaambiwa; atakuwa anapita mmoja mmoja, anaenda kumuaga mtu aliyekuwa anakwamisha mafanikio yake. Utaratibu ukawa unapomaliza kuaga, unapitia mlango mwingine. Hukutani na wenzako mliokuwa mmekaa wote.

Wakati wapo wote, kila mmoja alikuwa anamwagalia mwenzake kama yupo. Asije kuwa ndiye mhusika. Baadhi walionana, huku wengine hawakuonana. Swali likabaki atakuwa ni nani?

Muda ukafika. Mmoja mmoja akawa anaruhusiwa kwenda kutoa heshima za mwisho. Walipofika sehemu ya kuagia mwili. Hapakuwepo na mtu yeyote, bali kilikuwepo kioo chini.

Hivyo, ukipita kama unatoa heshima za mwisho ulikuwa unajiangalia. Halafu mbele kabla hujavuka kwenda nje, kuna kioo kingine kimeandikwa; “MTU PEKEE ANAYEKWAMISHA MAENDELEO YAKO NI WEWE.

Kila mfanyakazi aliyepita, alistaajabu na kushangaa sana. Walichokuwa wanategemea, sio walichokikuta. Walidhani atakuwepo mhusika, kumbe ni wao wenyewe.

Siku zilizofuata, kila mmoja aliweka nguvu kubwa kwenye kufanya kazi kwa umakini akiamini ni yeye pekee anayezuia mafanikio yake. Na Baada ya siku chache mafanikio yalikuwa makubwa kuanzia kwa mtu mmoja mmoja. Kwa sababu Kila mmoja alikuwa na ari, hamasa na kasi ya utendaji”.

Note; Wazo hilo lilibuniwa na meneja wa kampuni ile, baada ya kuona kazi haziendi wafanyakazi wake wanalalamika na kulaumiana.

Umejifunza nini kwenye simulizi hii? Hakuna wa kuyabadilisha mauzo, tofauti na wewe mwenyewe. Maisha ya rafiki yako, bosi wako au mzazi wako yakibadilika, sio yako, japo unaweza kuwa sehemu ya mabadiliko hayo. Inapokuja kuhusu wewe, maendeleo yako yanakutegemea wewe mwenyewe.

Maisha yako yatabadilika pale utakapobadilika. Sio kampuni yako ikikua, au watu wako wa karibu. Ukuaji wako unaanzia kwako. Uhusiano pekee unaopaswa kujenga ni ule wa kwako na nafasi yako. Ondoa imani haba kuhusu wanaozuia maendeleo yako. Usipofanya kazi, usitegemee ukuaji au mafanikio. Ni kupitia kazi unayofanya kwa unayofanya Kwa ubora na uaminifu mkubwa itakufanya ukue.

Ni kupitia mahusiano mazuri unayofanya na wateja wako, hukusaidia kuuza mauzo.

Tabasamu unaloonyesha mbele ya mteja humfanya anunue.

Uaminifu unaojenga mbele ya mteja, uwasilishaji wako, ujuzi wako au ufuatiliaji wako. Vyote hivyo humfanya anunue. Hadi hapo unaweza kuona watu wanakununua wewe kabla ya bidhaa. Hivyo, unapaswa kujiuza wewe kupitia huduma, uwasilishaji, tabasamu au uaminifu.

Je, anayekwamisha maendeleo yako ni nani? Bonga nasi 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz kwa maoni na ushauri.

Fanyia kazi yote uliyojifunza katika somo hili la leo katika biashara yako. Ili ukuze mauzo Yako.

Karibu tujifunze zaidi.

Leave a comment