Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Matumizi Bora Ya Hisia Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, huwa tunafanya maamuzi yetu mengi kwa hisia kwanza kisha kuyahalalisha kwa mantiki.Japo huwa tunapenda kujiona ni watu wa mantiki, lakini hilo ni gumu sana kwenye uhalisia.

Hivyo badala ya kupingana na hali yetu ya kuathiriwa na hisia, tunapaswa kujua jinsi ya kuitumia vizuri ili kuweza kupata kile tunachotaka.

Mafanikio kwenye mauzo, ambayo yanatokana na wewe kuwa muuzaji bora, yanategemea sana jinsi unavyoweza kutumia vizuri hisa.Na hili ni kwa pande zote, hisia zako binafsi na hisia za wengine.

Kwenye somo hili tunajifunza jinsi ya kutumia vizuri hisia ili kufanikiwa kwenye mauzo.Tutaangalia hilo kwa pande zote mbili, kwako binafsi na kwa wateja.

HISIA BINAFSI ZA KUFANIKIWA KWENYE MAUZO.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo unapaswa kuzitumia vizuri hisia binafsi ambazo zipo sita.

1. Upendo.Pendo ndiyo hisia binafsi yenye nguvu sana. Upendo wa kweli unapokuwepo, hakuna kinachoshindikana.Anza kwa kujipenda wewe mwenyewe, wapende wengine (pamoja na wateja wako) na penda kile unachofanya (unachouza).Ukiwa na upendo wa kweli kutoka moyoni kwako, utafanya makubwa.

2. Matamanio makubwa.Kuwa na matamanio makubwa ya kufanya makubwa kwenye maisha yako. Kuwa na ndoto kubwa unazopambania kuzifikia kwenye maisha.Matamanio yako makubwa yanapaswa kukukosesha usingizi na kukufanya ujutie pale unapohangaika na mambo yasiyokuwa na tija.Msukumo wa aina hiyo utakufanya utulie kwenye mauzo na ujisukume zaidi ya kawaida.

3. Kujikubali.Lazima ujikubali sana wewe mwenyewe kwamba unaweza kufanya makubwa unayotaka.Yeyote anayekubeza au kukukatisha tamaa unamcheka na kumbeza, kwa sababu unajua hakujui.Bila ya kujikubali kupitiliza, safari itakuwa ngumu kwa sababu vikwazo na wakatisha tamaa ni wengi.

4. Kuamini.Unapaswa kuwa na imani kali sana juu yako mwenyewe, juu ya wengine (pamoja na wateja wako) na amini kwenye kile unachofanya (unachouza).Amini wewe ni mtu sahihi kwenye hicho unachouza na utafanikiwa kadiri ya unavyotaka.Amini wateja wako wanataka unachouza na kina manufaa makubwa kwao.Na amini kile unachouza kina thamani kubwa na anayekipata anakwenda kunufaika nacho.Ni kiwango chako cha imani kwenye maeneo hayo matatu ndiyo kitawafanya wengine wakuamini na kukupa kile unachotaka.

5. Furaha.Wengi hudhani wakishafanikiwa ndiyo watafurahi. Lakini sahihi ni ukiwa na furaha ndiyo utafanikiwa. Yaani furaha inaanza kabla ya mafanikio unayotaka.Hivyo unapaswa kufurahia mchakato wako mzima wa mauzo. Furahia kila unachofanya. Furahia wale unaojihusisha nao.Unapokuwa na furaha unavuta fursa nyingi nzuri kuja kwako.Kuwa na furaha bila ya kujali nini unapitia, kwa sababu kama bado upo hai, una mengi ya kushukuru na kufurahia.

6. Utimilifu.Watu wengi huwa wanadhani wanapaswa KUFANYA ili KUPATA na hatimaye KUWA yule wanayemtaka.Hilo pia ni kinyume na mafanikio yanavyokuja.Unaanza kwa KUWA yule unayetaka kuwa, kisha UNAFANYA na KUPATA.Hivyo unapaswa kuanzia kwenye utimilifu, kwa kuwa na hisia ambazo utakuwa nazo pale unapokuwa umepata unachotaka.Kwa njia hiyo utakuwa na msukumo mkubwa wa kufanya na hapo utapata.

Jijengee hisia hizo sita kwako binafsi na zitumie kwenye mauzo ili uwe na msukumo mkubwa kwako kufanya makubwa.

HISIA ZA WATEJA ZA KUFANIKIWA KWENYE MAUZO.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo, unapaswa kugusa hisia za wateja ambazo zitawasukuma kuchukua hatua mara moja.Hisia za kugusa kwa wateja zipo sita.

1. Tamaa.Watu huwa wana tamaa yakupata zaidi. Waonyeshe kwa kununua kwako wanapata zaidi ya wakinunua kwa wengine.Pia waonyeshe wakinunua sasa watapata zaidi kuliko wakisubiri.

2. Hofu.Watu huwa wana hofu ya kupoteza kile walichonacho au walichotegemea kupata.Kwa kuwaonyesha watu nini wanakosa au kupoteza wasiponunua, wanasukumwa kufanya manunuzi ya kununua.

3. Wema.Watu huwa wanapenda kuonekana ni wema na kile wanachofanya kina manufaa kwa wengine.Waonyeshe wateja kwamba kwa kununua kwako wanakuwa wametenda wema kwa wengine wanaonufaika pia.Kwamba siyo wewe tu na mteja mnaonufaika, bali kuna wengine pia wananufaika.

4. Wivu.Dunia huwa inaendeshwa kwa wivu. Watu huwa wanasukumwa kufanya vitu kwa sababu hawataki kupitwa na watu wengine.Waonyeshe wateja jinsi ambavyo wengine wananufaika na unachouza huku wao wakiachwa nyuma.Hili litawasukuma kuchukua hatua ili wasiachwe.

5. Ufahari.Watu wanapenda ufahari na kuwa na hadhi ya juu kwa wengine.Waonyeshe wateja kwa kununua wanaongeza hadhi yao na watasukumwa kuchukua hatua.

6. Aibu.Watu huwa hawapendi kuonekana ni wajinga au washamba. Wanapenda kuonekana ni wajanja na wajuaji.Waonyeshe wateja kwa kununua unachouza wanakuwa sehemu ya wajanja wachache na hivyo kuepuka aibu ambayo wanaweza kukutana nayo kama hawatachukua hatua.

Tumia hisia hizi kwa wateja wako na utaweza kuongeza ushawishi wa kuwafanya wakubaliane na wewe na uweze kuuza zaidi.

Wewe kama kiumbe wa hisia, ukitumia vizuri hisia zako utaweza kuwa na msukumo wa kufanya makubwa. Na kwa kutumia vizuri hisia za wateja wako utaweza kuwa na ushawishi mkubwa.

Hayo yote yatakufanya wewe kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea kwa kukamilisha mauzo makubwa zaidi.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.Kocha Dr. Makirita Amani, Mkuu wa CHUO CHA MAUZOwww.mauzo.tz

Leave a comment