Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Kusaka wateja kwa njia ya utembeleaji na kukutana ana kwa ana.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, eneo la usakaji. Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tafajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

Kauli mbiu yetu ni; USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Ni kupitia kusaka ndiyo biashara inatengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi. Na biashara yenye wateja tarajiwa wengi, haiwezi kushindwa kufanya mauzo makubwa kama watafuatiliwa vizuri.

Njia ya kutembelea wateja na kukutana nao ana kwa ana ni moja ya njia zenye ushawishi mkubwa.Hiyo ni kwa sababu pale watu wanapokutana, kunakuwa na fursa kubwa ya kutumia mbinu nyingi za ushawishi kama tabasamu, shauku na kunasa umakini wa mtu kwa mambo mbalimbali.

Njia za mawasiliano zinarahisisha kuwafikia wateja wengi ndani ya muda mfupi. Lakini njia hizo huwa haziwezi kuwa na ufanisi mkubwa kwa wateja kama njia ya ana kwa ana.Ndiyo maana licha ya uchache wake kwenye watu wanaoweza kufikiwa, bado matokeo yake ni mazuri.

Njia ya kutembelea na kukutana na wateja ana kwa ana imegawanyika kwenye sehemu mbili.

Moja ni kutembelea wateja bila ya kuwa na miadi. Hapa unakwenda kwa wateja bila ya miadi ya kukutana.Japo inakuwa haina uhakika wa kuwakuta, ina matokeo mazuri ya kuwafikia wengi zaidi.Kwa sababu kupata miadi inaweza kuwa vigumu, lakini kwenda bila miadi inaweza kutengeneza nafasi ya kuwafikia wateja wanaolengwa.

Mbili ni kutembelea wateja kwa miadi. Hapa kunakuwa na miadi inayokuwa imewekwa na mkutano unategemewa na pande zote mbili.Hii ni njia nzuri kwenye mikutano ya mauzo inayofuata. Lakini kwa mkutano wa kwanza, njia hii haina matokeo mazuri.Ni vigumu mtu asiyekujua kabisa kukupa miadi. Hivyo kwa mara ya kwanza mtu anapaswa kwenda bila miadi na hapo kutengeneza miadi ya baadaye.

Ili usakaji kwa njia ya kutembelea na kukutana na wateja ana kwa ana uwe na tija, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.

1. Utembeleaji unapaswa kupangiliwa vizuri ili maeneo yote lengwa yaweze kufikiwa na muda mwingi usipotee kwenye kuzunguka, bali utumike kukutana na wateja.

2. Fanya utafiti wa wale unaowatembelea kabla ya kukutana nao. Nenda kwao ukiwa na taarifa fulani kuwahusu, watakuona ni makini na kukupa nafasi.

3. Andaa vizuri uwasilishaji unaokwenda kufanya kwa wateja unaokutana nao, ukiwa na mifano na shuhuda mbalimbali.

4. Kuwa na mwonekano nadhifu unapoenda kukutana na wateja, watu wanakuhukumu kwa mwonekano wako wa nje kabla hata hawajakusikiliza.

5. Heshimu kila unayekutana naye kwenye eneo unalotembelea hata kama siyo mhusika unayemlenga, huwezi kujua umuhimu wake. Maeneo mengi unayotembelea kunaweza kuwa na watu wa kati ambao wanaonekana kikwazo kwako kuwafikia unaowalenga. Jenga nao mahusiano mazuri na watakupa fursa ya kuwafikia unaowalenga.

6. Nenda ukiwa umejiandaa kuuza kabisa na pale fursa inapojitokeza itumie kukamilisha mauzo.

7. Maliza kila mkutano wa kukutana na mteja mkiwa mmekubaliana hatua ya kuchukua. Kama ni miadi ya uwasilishaji zaidi, au yeye kufanya maamuzi, au wewe kumtumia taarifa zaidi.

8. Kuwa na ufuatiliaji kila baada ya kutembelea na kukutana na wateja. Usiwe mtu wa kugusa wateja mara moja na kuwaacha. Baadhi ya wateja wanataka mkutane mara nyingi mpaka wajenge imani na kununua kwako.

9. Tumia fursa za kukutana na wateja wengi kwa mara moja ili kutumia nguvu ya ana kwa ana kwa ufanisi zaidi. Mfano kushiriki matukio mbalimbali ya kibiashara, kimichezo na kijamii ambapo wateja unaowalenga wanakuwepo kwa wingi.

10. Kuwa na ung’ang’anizi kwenye zoezi la utembeleaji na kukutana na wateja ili uweze kupata matokeo mazuri. Unaweza kukataliwa mwanzoni, lakini hupaswi kukata tamaa. Endelea kurudi kwa wateja na kila mara wape thamani kubwa hata kabla ya kununua kwako. Hilo litakupa nafasi ya kupata kile unachotaka.

Kila biashara inapaswa kufanya usakaji wa kutembelea wateja kule walipo kwa ajili ya kuwafanya waijue biashara, na pia waweze kununua.Wateja wengi kwa sasa hawatembelei sana maeneo ya biashara, hivyo biashara inayosubiri wateja waende itakuwa na wakati mgumu kwenye mauzo.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.

Kocha Dr. Makirita Amani, Mkuu wa CHUO CHA MAUZOwww.mauzo.tz

Leave a comment