Kila wakati unapaswa kujifunza na kuwa na msukumo mkubwa wa kutaka kuboresha mahusiano yako na ushawishi wako kwa wengine.
Kwa sababu, kwenye maisha kama kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, kila mara jiambie, umaarufu wangu, furaha yangu na utajiri wangu vinategemea uwezo wangu wa kuendana na watu. Kwa kulitambua hilo, leo ikiwa ni jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza misingi ya kukabiliana na watu na leo tunaangalia kanuni ya kwanza ya kukabiliana na watu.
Kwenye maisha kuna wakati unajikuta unakabiliana na watu ambao wanaamini tofauti na uvyoamini wewe.
Watu wa aina hii, ukiwaonesha kwamba wanakosea watazidi kushikilia wanachoamini.
Hivyo basi, hapa tunakwenda kujifunza kanuni ya kwanza ya kukabiliana na watu ambayo ni ;
USIKOSOE, KUHUKUMU AU KULAUMU.
Katika maisha yetu huwa tunakutana na watu ambao wanafanya vitu tofauti na tunavyowategemea wafanye.
Ni rahisi kuona kwamba watu hao wanakosea, lakini usichojua ni kwamba, kwa upande wao wanaona wako sahihi kwa kile wanachofanya.
Unaweza kuona ni sahihi kuwarekebisha kwa kile wanachokosea kwa kuwakosoa, kuwahukumu au kuwalalamikia, lakini hilo limekuwa halisaidii.
Kwani unapomkosoa, kumhukumu au kumlalamikia mtu, anazidi kusimamia kile ambacho hutaki afanye. Kwa mfano, unamwambia msaidizi wako, mtu wako wa karibu au mtoto kwamba wewe ni mjinga na huna unachojua.
Kama ni mtoto kila wakati atakua anakosea kwa sababu ulishamwambia ni mjinga, na yeye anataka kudhihirisha kile ambacho anacho ambacho ni ujinga.
Mwandishi Dale, anatuambia kwamba, kama unataka kupata asali, usipige mzinga. Kukosoa huwa hakuzai matunda, kwa sababu yule unayemkosoa hutafuta njia ya kujitetea. Lakini pia, kukosoa ni hatari kwa sababu kunaumiza sifa ya mtu na hivyo atapambana kuilinda.
Hata ukikutana na wateja wako, usiwakosoe, bali wasifie kwani ukiwakosoa, utakosa asali yaani mauzo na ni sawa na kupiga mzinga huku ukitegemea utapata asali.
Kadiri ya tafiti za mwanasaikolojia Skinner zinaonesha kwamba watu huwa wanajifunza kwa haraka zaidi wanaposifiwa kuliko wanapokosolewa.
Kama unataka kuboresha mahusiano yako na kuwa na ushawishi na wateja au wengine,basi acha mara moja tabia kukosoa, kuhukumu au kulaumu wengine kwa kile wanachofanya.
Badala yake, jiweke kwenye nafasi yao, kisha wasaidie kuona kile wanachopaswa kuona na kitakachowasukuma kufanya maamuzi ya kubadilika wao wenyewe.
Njia bora ya kuwabadili wengine, ni kwa kuanza kubadilika wewe mwenyewe kwanza. Ni rahisi kubadilika wewe mwenyewe, na wengine wanapoona umebadilika wanashawishika kubadilika pia. Kwa mfano, badala ya kuwaambia wasaidizi wako wawahi kazini, wewe anza kuwahi na wao watawahi.
Unapokabiliana na watu,tambua kwamba hukabiliani na viumbe wa kifikra, bali viumbe vya hisia.
Sisi binadamu huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia na siyo kwa fikra kama tunavyodhani.
Kukosoa, kuhukumu, kunakwenda kugusa hisia za watu hapo watajibu kwa njia ya kujilinda.
Kitu kimoja zaidi, mpumbavu yeyote anaweza kukosoa, kuhukumu na kulaumu na wapumbavu wengi hufanya hivyo.
Wewe usiwe mpumbavu, jijengee tabia ya kujidhibiti , kuelewa na kusamehe na hilo litakusaidia kuendana na watu wengine.
Ishi na watu vizuri kwa sababu kile unachotaka utakipata kwa watu, kama unataka asali, usipige mzinga.
Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz