Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Matumizi Bora Ya Roho/Imani Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Watu wanapokuangalia kwa nje, wanakuona kama mwili wako.

Hivyo wanakuchukulia wewe kama mwili.

Lakini wewe unavyojiona ndani yako siyo kama mwili.

Wewe mwenyewe unajiona zaidi ya mwili.

Na ndiyo maana viungo vya mwili huviiti wewe, bali unaviita vyako.

Utasema kichwa changu kinauma.

Au mikono yangu ni michafu.

Swali ni je huyo mwenye kichwa na mikono ni nani hasa?

Hapo ndipo penye jibu lenye nguvu ya kukupa mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.

Huyo mwenye mwili wako wewe ambaye ni roho inayokaa kwenye huo mwili.

Pamoja na watu wengine kukuona wewe kama mwili, ukweli ni wewe ni roho iliyo kwenye mwili.

Ndiyo maana roho hiyo inapotoka, mwili hubadilika na kuitwa maiti ya fulani.

Kujua kwamba wewe ni roho iliyo ndani ya mwili ulionao ni hatua muhimu sana kwako kuweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha.

Hatua ya kwanza na muhimu kabisa ni kutambua kwamba wewe kama roho haupo hapa duniani kwa bahati mbaya.

Bali upo hapa duniani kwa kusudi maalumu. Ili kuyaishi maisha yako kikamilifu, ni lazima ukamilishe kusudi hilo.

Lakini pia unapaswa kujua hakuna mtu wa nje anayeweza kujua kusudi lako ni nini. Hata wazazi waliokuzaa, hawawezi kujua hilo.

Kwa bahati nzuri sana, ndani yako ipo sauti inayokuambia nini unapaswa kufanya na maisha yako.

Wajibu wako ni kuisikiliza sauti hiyo na kuifuata, kwa sababu kamwe haiwezi kukupoteza.

Mauzo ni moja ya njia ya kukuwezesha wewe kuishi kusudi la maisha yako.

Kwani mara nyingi sana, kusudi la maisha huwa linahusisha kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Kupitia mauzo unayo fursa kubwa ya kuyafanya maisha ya watu wengine kuwa bora.

Unatekeleza hilo kwa kuwauzia watu vitu vyenye thamani na vinavyotatua matatizo na changamoto walizonazo.

Jambo la msingi zaidi kuhusu mauzo na roho/imani ni kujua una wajibu wa kimaadili wa kuhakikisha wateja wananunua kile unachouza.

Kama kweli kile unachouza kina thamani kwa wateja unaowalenga, basi ni wajibu wako wa kimaadili kuhakikisha wanakipata.

Hata kama watu hao watakuwa wabishi na wasiotaka kukusikiliza, tambua umepewa wajibu wa kuhakikisha wanapata kitu hicho ili maisha yao yawe bora.

Ona unakuwa umefanya dhambi kubwa sana pale unaposhindwa kuwashawishi watu wanunue kile unachouza.

Imani kwenye kile unachouza ni hitaji muhimu sana kwako ili uweze kufanya mauzo makubwa zaidi.

Huwa kuna usemi kwamba mauzo ni mabadilishano ya imani.

Yaani mteja ananunua pale anapopata imani kupitia muuzaji.

Kitu muhimu kujua hapa ni kwamba mteja huwa hataki sana kuamini kile unachomuuzia ndiyo akubali kukinunua.

Bali mteja anataka kuamini kwamba wewe unakiamini kweli kile unachomuuzia.

Ni imani yako kwenye kile unachouza ndiyo itamshawishi mteja anunue.

Hivyo wajibu wako mkubwa kama muuzaji ni kuamini sana kwenye kile unachouza.

Kiamini kweli na kuwa na ushahidi wa hiyo imani yako.

Na pale unapokuwa unazungumza na mteja kumshawishi kununua, hakikisha unaionyesha hiyo imani yako.

Kuna wateja watakaojaribu kutikisa imani yako kwenye hicho unachouza, usikubali kutetereka.

Usionyeshe wasiwasi wa aina yoyote ile juu ya kile unachouza.

Hakuna kitu ambacho watu wanakinasa haraka kama wasiwasi na kukosa imani.

Amini kile unachouza bila ya chembe yoyote ya shaka na utaweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

Mambo mawili muhimu sana ya kuondoka nayo hapa ni haya;

Moja; Wewe kama roho, tumia mauzo kutimiza kusudi la wewe kuwa hapa duniani. Yafanye maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia kile unachouza.

Mbili; Amini sana kwenye kile unachouza. Kuwa na imani isiyotetereshwa juu ya kile unachouza na utawafanya wateja wakuamini na kuwa tayari kununua. Imani hii isiwe ya kuigiza, bali iwe halisi na yenye ushahidi.

Zingatia hayo mawili na utaweza kutumia roho/imani kufanikiwa kwenye mauzo na maisha kwa ujumla.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.

Kocha Dr. Makirita Amani,

Mkuu wa CHUO CHA MAUZO

www.mauzo.tz

Leave a comment