Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Kufuatilia Rufaa Ili Kutengeneza Wateja Wengi Tarajiwa.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, eneo la usakaji. Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tafajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

Kauli mbiu yetu ni; USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Ni kupitia kusaka ndiyo biashara inatengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi. Na biashara yenye wateja tarajiwa wengi, haiwezi kushindwa kufanya mauzo makubwa kama watafuatiliwa vizuri.

Tumeona kwenye njia nyingi za kusaka wateja wapya tarajiwa, rufaa ndiyo njia yenye nguvu zaidi.

Wateja wanaopatikana kwa rufaa huwa ni wa uhakika na rahisi kuwakamilisha kuliko wanaopatikana kwa njia nyingine.

Pamoja na ubora na urahisi wa njia ya Rufaa, bado haimaanishi kwamba kazi haihitajiki kufanyika.

Bado kazi kubwa sana inapaswa kufanyika kwenye zoezi la rufaa ili kuweza kupata wateja wapya tarajiwa kwa uhakika.

Unapoomba rufaa, kuna matokeo ya aina tatu yanayoweza kupatikana;

1. Kukosa rufaa, kwa mteja kukuambia hana. Hili huwa ni kwa wingi zaidi.

2. Kupata rufaa lakini zisiwe na sifa ya kuwa wateja. Hili huwa ni kwa kiasi.

3. Kupata rufaa na zikawa na sifa ya kuwa wateja. Hili huwa ni kwa uchache sana.

Kwa matokeo yote matatu, kuna kitu kimoja chenye nguvu ya kuleta matokeo mazuri kwenye zoezi la rufaa.

Kitu hicho ni kufanya ufuatiliaji wa uhakika kwenye zoezi zima la rufaa.

Na hapa unakwenda kujifunza jinsi ya kufanya ufuatiliaji wa uhakika kwenye matokeo yote matatu ili uweze kupata wateja wengi kupitia rufaa.

Ufuatiliaji unapokosa rufaa.

Unapomwomba mteja akupe rufaa na akakuambia hana mtu anayeweza kukupa, hilo halimaanishi ndiyo mwisho wa kumwomba.

Moja anaweza kuwa anakudanganya, anaweza kuwa na watu wengi tu, ila anakuwa hajakuamini vya kutosha.

Mbili anaweza kuwa ni mkweli, kwamba hana aliyenaye kwa wakati huo unaomwomba.

Kwa vyovyote vile, ufuatiliaji wa karibu unahitajika sana. Pale unapomwomba mteja rufaa na akakukatalia, mchezo ndiyo unakuwa umeanza.

Utaendelea kumwomba rufaa kwa mwendelezo, angalau mara moja kila wiki mpaka atakapokupa.

Hata kama atakukumbusha kwamba alishakujibu hana, mwambie unamkumbusha ili akikutana na mwenye uhitaji asikusahau.

Unapofanya ufuatiliaji wa aina hiyo unajua nini kitatokea? Mteja atakuamini na kukuheshimu kwa ung’ang’anizi wako na atakupa rufaa.

Na hata kama hatakupa, utaendelea kuomba, kwa msimamo bila kuacha.

Ufuatiliaji unapopata rufaa zisizo na sifa.

Kupewa rufaa lakini zisiwe na sifa haimaanishi zoezi zima la rufaa halina maana. Bali ni fursa ya kuendelea na ufuatiliaji mpaka upate wale wenye sifa na ambao utawauzia.

Ufuatiliaji kwa rufaa zilizokosa sifa fanya yafuatayo;

Moja; rudi kwa aliyekupa rufaa, mshukuru kwa kukupa rufaa na mweleze aliyekupa hajawa na sifa. Hivyo mwombe akupe mwingine mwenye sifa, huku ukiainisha sifa za wanaokufaa zaidi.

Mbili; endelea kufuatilia rufaa uliyopata bila kikomo. Kukosa sifa sasa haimaanishi atakosa sifa milele. Miezi kadhaa ijayo anaweza kuwa na sifa ya kuwa mteja. Kwa kumweka kwenye ufuatiliaji endelevu itakupa fursa ya kuwa wa kwanza kwake pale anapopata uhitaji.

Tatu; omba rufaa kwa rufaa hiyo. Pamoja na wao kukosa sifa, wanaweza kuwa wanawajua wengine wenye sifa. Hivyo omba kila rufaa unayopata ikupe rufaa nyingine zaidi. Hili linaweza lisikupe matokeo mazuri kwa sababu rufaa inakuw bado haina imani na wewe, lakini je unapoteza nini kwa kuomba? Wewe omba na omba bila kukoma.

Ufuatiliaji unapopata rufaa zenye sifa.

Kupata rufaa yenye sifa huwa ni ushindi mkubwa sana. Kwani huwa ni mteja rahisi kumkamilisha, anafanya manunuzi makubwa na hasumbui. Ukipata rufaa moja ya uhakika, unatamani wateja wako wote wangekuwa kama rufaa hiyo.

Wengi kwa kufurahia ushindi wa kupata rufaa, huwa wanajisahau na kutokufanya ufuatiliaji wa uhakika kwa rufaa hizo, kitu kinachowazuia wasinufaike nazo vya kutosha.

Ufuatiliaji kwa rufaa zenye sifa fanya yafuatayo;

Moja; toa huduma bora sana kwa rufaa uliyopata ili kumfanya aliyekupa rufaa ajivunie kufanya hivyo. Kuwahudumia vizuri wateja wa rufaa ni kufungua milango ya kupata wengine wengi

Mbili; washukuru waliokupa wateja hao wa rufaa na waombe wakupe wateja wengine kama hao. Kushukuru ni kuomba tena, hivyo pale unapomshukuru aliyekupa rufaa, anasukumwa kukupa rufaa zaidi.

Tatu; endelea kuomba rufaa kwa wote, kwa waliokupa na kwa unaowapata. Kitendo cha kupata rufaa nzuri, kiwe msukumo kwako kuendelea kuomba rufaa bila kukoma. Hata pale unapokosa rufaa, jikumbushe rufaa nzuri ambazo umewahi kupata na hivyo endelea kuomba bila kukoma.

Ufuatiliaji una nguvu kubwa sana kwenye kila eneo la mchakato wa mauzo.

Na kwenye rufaa, bila kufanya ufuatiliaji wa uhakika, zoezi zima litakosa tija.

Fanyia kazi njia hizi za kufuatilia rufaa ili uweze kupata wateja wapya tarajiwa wengi zaidi kwa njia ya rufaa. Kwa kuwa njia ya rufaa ndiyo njia bora na yenye ushawishi, ni wajibu wa kila muuzaji kuitumia kupata wateja wapya tarajiwa.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.

Kocha Dr. Makirita Amani,

Mkuu wa CHUO CHA MAUZO

www.mauzo.tz

Leave a comment