Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Jinsi Ya Kutumia Silaha Ya Ushawishi Ya Kupenda Kufanya Mauzo Zaidi

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye kwenye jumamosi ya ushawishi tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Kwa kulijua hilo, kwamba hatupati tunachostahili bali tunapata kile tunachoshawishi.
Na hii ndiyo sababu ya sisi kujifunza ushawishi ili tuweze kuwashawishi watu wengine waweze kukubaliana na sisi kupitia kile tunachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kwenye somo letu la leo, tutajifunza silaha ya nne ya ushawishi ambayo ni kupenda.

Iko hivi rafiki yangu, kisaikolojia huwa tunakubaliana zaidi na wale tunaowapenda kuliko ambao hawatupendi.
Na hilo limewafanya wale wanaotaka kutushawishi kujua njia ya rahisi ya sisi kukubaliana nao.

Njia hiyo ni wao wao kujiweka kwenye mazingira ambayo yanatufanya tuwapende.
Kwa mfano, wanavaa mavazi mazuri na kujiweka kwenye hali za kupendeza, wanatabasamu na kufanya mengine, yote haya ni kwa lengo la kutufanya tuwapende na hapo tukubaliane na kile wanachotaka.

Kabla hatujaendelea na kwanza tupate mifano mifupi ya jinsi silaha hii ya ushawishi ya kupenda inavyofanya kazi na ilivyo na nguvu kwenye jamii yetu.

Kwa mfano, biashara za mtandao yaani network /multilevel marketing.
Mfumo huu wa biashara unamtaka mtu ajiunge na kuwa mteja, kisha awashawishi marafiki na watu wake wa karibu nao kujiunga kuwa mteja.
Kama ulishawahi kualikwa uhudhurie mikutano ya biashara hizi, utagundua kwamba ulialikwa na mtu wako wa karibu.

Na alipokualika hata kama ulikuwa hutaki kwenda, hukuwa tayari kukataa, badala yake ulikubali kuhudhuria na huenda hata kujiunga.

Kwa nini unafikiri silaha hii ina nguvu kubwa? Kwa sababu silaha ya kupenda ina nguvu ya kubwa kwa sababu ni vigumu sana kumkatalia mtu ujayemjua na kumpenda.

Kwa mfano, kwenye rufaa, ni vigumu sana mtu kukukatalia pale anapokuja kukuambia kwamba rafiki yako fulani alinufaika na kitu fulani, hivyo amekupendekeza na wewe uweze kunufaika na bidhaa au huduma fulani.
Kwa mazingira kama hayo, mtu anaona akikataa, anakuwa hajakataa bidhaa au huduma bali amemkataa aliyempendekeza, hivyo mtu anaona ni bora akubali kwa sababu mahusiano yana nguvu ndiyo maana tunasema mauzo ni mahusiano, wale tunahusiana nao wana nguvu ya kubwa ya kutushawishi au kuwashawishi wakubaliane na sisi kwenye jambo fulani.

Mteja akisikia tu jina la rafiki yake, linatosha kukamilisha mauzo kwa sababu anaona ni heshima kubwa kumpendekeza yeye miongoni mwa wengi.

Mfano mwingine ni muuzaji aliyevunja rekodi ya dunia kwa kutumia silaha ya kupenda.
Mtu huyo siyo mwingine bali ni Joe Girard. Girard alikuwa ni muuzaji bora kuwahi kutokea, alikuwa ni muuzaji namba moja wa magari duniani na aliyevunja rekodi ya kuuza magari mengi mpaka kuingia kwenye kitabu cha maajabu ya dunia.

Na alipoulizwa kuhusu siri ya mafanikio yake makubwa kwenye mauzo ya magari alisema ni vitu viwili, ambavyo ni urafiki na bei nzuri.
Anasema kwamba, pale mteja anapokutana na muuzaji anayempenda na muuzaji akampa bei nzuri, lazima atanunua.

Na pale watu walipoanza kufuatilia ili kujua kwa nini wateja wanampenda sana Joe Girard kuliko wauzaji wengine, ndipo walipogundua siri yake ambayo ni alijenga mahusiano ya urafiki na ukaribu na kila mteja wake.

Na cha kushangaza Joe Girard alikuwa na orodha ya wateja wake wote ambao wamewahi kununua kwake na wale ambao analenga kuwauzia.
Kisha, kila mwezi alituma kadi moja kwa kila mteja wake. Alikuwa na malaki ya wateja lakini wote aliwakumbuka.
Je, wewe huwa unawakumbuka wateja wako kama Joe Girard?

Somo kubwa la kuondoka nalo hapo kwa Joe Girard ni kwamba usiwasahau wateja wako, jenga falsafa ya mauzo ni mahusiano na pale wateja wanapokuwa wanahitaji kitu, wanaenda kwa mtu wao wa karibu na kununua hakikisha unalifanya hilo kwenye biashara yako.
Usiwakumbuke wateja tu kwa kutaka wakupe oda kwa sababu kuna biashara nyingine wao wanawakumbuka wateja kwa kuwapigia kwa lengo la kuomba oda na siyo kujenga mahusiano.

Ili silaha hii ya ushawishi ya kupenda ifanye kazi vizuri huwa ina vigezo vyake vinavyotumika.
Vigezo hivi vikiwepo kwa mtu anapendwa zaidi ya wengine.

Vifuatavyo ni vigezo vyenye nguvu kwenye kupenda.

Moja ni mwonekano mzuri.
Wale ambao wana mwonekano mzuri, warembo, au watanashati huwa wanapendwa zaidi kuliko wasio na mwonekano mzuri.
Na hii huwa inatokea bila hata ya anayevutiwa kujua kwamba mwonekano ndiyo umemfanya avutiwe.

Hatua ya kuchukua hapa, kuwa na mwonekano mzuri kwa sababu watu wenye mwonekano mzuri wanaonekana wana tabia na sifa nzuri hata kama siyo kweli.
Huonekana ni wema zaidi, waaminifu na wenye akili.

Mtu mwenye mwonekano mzuri basi ni mtu mzuri.
Tafiti zinaonesha kwamba watu wenye mwonekano mzuri wamekuwa wanapata fursa nzuri kwenye jamii kuliko wasiokuwa na mwonekano mzuri na kwenye biashara kukubalika zaidi.

Mbili, kufanana.
Watu wanapenda watu wanaofana nao kuliko wasiofanana nao.
Na haijalishi ufanano huo uko  kwenye kitu gani, inapokuwa tu kuna kitu ambacho wanakubaliana pamoja basi ushawishi unakuwa mkubwa zaidi.
Kwa mfano, mfanano kwenye kushangilia timu za mpira au chama, shule au chuo kimoja huwa wanapendana zaidi kuliko kuliko kutokuwepo kwenye ufanano huo.

Tumia ufanano wewe kama muuzaji kuweza kuwashawishi wateja wako kwa kuwa upande wao kwenye vile wanavyopenda kushabikia.
Ufanano una nguvu kubwa hata kwenye vitu vidogo kama vile mavazi, umri, jinsia, dini, siasa, starehe na kadhalika.

Tatu ni pongezi.
Pale mtu anapotusifia tu huwa tunakubaliana naye kwa urahisi zaidi.
Pongezi imekuwa ni njia inayotumika kuibua kupenda na kushawishika zaidi.
Haijalishi kama pongezi ni ya kweli au la , ambacho mtu anaangalia ni  kama kweli inatoka ndani ya mtu.

Kwa mfano, kwa kila kadi ambayo Joe Girard aliyokuwa anawatumia wateja wake alimalizia kwa kusema nakupenda.

Tafuta chochote cha kupongeza kwa mteja wako kwa sababu pongezi huwa ina nguvu kubwa na inakuwa rahisi kwetu kuwashawishi wateja mara baada ya kuwapongeza.

Nne, ukaribu na ushirikiano.
Hapa tengeneza mazingira ya  kuleta ushirikiano na ukaribu kwa mteja wako.
Ukaribu na ushirikiano umekuwa unampelekea watu kupendana. Kwa mfano, hata watu wakiwa hawajuani au wanatofautiana wakikaa karibu kwa muda na kushirikiana katika jambo hujikuta wanapendana na kukubaliana.

Tano ni hali na uhusianisho

Huwa tuna tabia ya kuhusishanisha watu na hali wanazokuwa nazo.
Ukitaka kuwashawishi watu hakikisha unajihusisha na vitu vizuri ili tu watu wakupende na kukubaliana na wewe.

Kwa mfano, wasanii na watu maarufu wanapochaguliwa balozi wa kitu fulani au taasisi fulani, biashara fulani au wanatumika kwenye matangazo.
Mfano, kampuni ya Pepsi, balozi wake ni ni msanii diamond anapokuwa anaonekana kwenye tangazo akinywa Pepsi na watu wengine nao wanajiona nao ni sehemu ya watu maarufu kwa sababu hata watu maarufu wanatumia kitu fulani.

Tumia silaha hii ya ushawishi ya kupenda kuweza kuwashawishi wateja na kisha kununua kwako.
Mara zote tengeneza mazingira ya watu kukupenda na kufanana nao ili uweze kuwashawishi.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

Leave a comment