Kuomba rufaa ni kitendo cha kumuomba mteja uliyempatia huduma au uliyekutana naye, akupe mtu mwingine, anayeweza kunufaika na bidhaa au huduma yako. Kwa lugha rahisi, mteja wa rufaa ni zao la mteja uliyehudumia au kukutana naye(Rafiki wa mteja wako).
Katika wateja wote unaokutana nao au kuwasiliana nao. Hakuna mteja rahisi kama mteja wa rufaa. Maana unapewa na mtu wake wa karibu Ili uongee naye kisha umshawishi kumuuzia.
Faida za kupata mteja wa rufaa;
Moja; Bei inakuwa sio tatizo kwao. Kwa kuwa anatoka kwa mtu anayeaminiana naye kwako anataka uaminifu basi.
Mbili; Rahisi kuwauzia.
Hii ipo tofauti na mteja unayemtafuta wewe upya, ambaye anahitaji kukujua na kukuamini. Ila mteja wa rufaa tayari kuna mtu wake wa karibu wanaaminiana anapoona amechukua bidhaa kwako inakuwa rahisi pia kuchukua.
Tatu; Unakuwa na pa kuanzia. Unapoanza kuongea na mteja wa rufaa huanzi upya mwanzo kuelezea kuhusu biashara yako. Unaanza kuelezea namna mtu wake wa karibu aliyenufaika na bidhaa yako. Hilo linamfanya awe mwepesi kukusikia na kuchukua hatua.
Nne; Hawachukui muda mrefu kufanya maamuzi. Mteja mpya tarajiwa unayemtafuta wewe anahitaji muda; kwanza kuijua biashara yako na kukuamini pia, anakuwa na hofu kuhusu ubora wa biashara yako na mahitaji yake. Lakini mteja wa rufaa hiyo yote haimpi shida. Anaamini mtu wake wa karibu hajafanya makosa kukuchagua wewe.
Tano; Mteja wa rufaa hahitaji gharama kubwa kumpata. Maana ni zao la mteja uliyempatia huduma nzuri.
Pamoja na uwepo wa faida nyingi zinazotokana na kuomba wateja wa rufaa cha kushangaza baadhi yetu hatuombi rufaa. Unataka kujua kwa nini? Hizi hapa sababu za wauzaji kutoomba rufaa;
Moja; Wanasahau.
Zipo sababu nyingi zinazofanya wauzaji wasahau kuomba rufaa. Wengi wetu huwa hawana utamaduni wa kuomba. Hivyo, hushtuka baada ya mteja kuwa ameondoka.
Mbili; Kutojiamini.
Wauzaji wengi wanaogopa kusikia “hapana” kutoka kwa mteja. Wengine wanahofia wateja kutorudi tena kununua. Au watabadili mtazamo wa kununua. Wengine wanadhania mteja huyo hastahili kuombwa rufaa. Kwa hiyo, hayo yote yanawafanya kushindwa kuomba rufaa.
Tatu; Ubora wa bidhaa zao.
Wauzaji wengine huhofia ubora wa bidhaa zao, ikiwa hazitamsaidia mteja kupata anachotaka. Ndiyo maana huogopa kuomba rufaa. Huku, wengine wakishindwa kuielezea biashara yao.
Nne; Kutoijua biashara.
Kushindwa kuijua biashara kwa kina ni moja ya sababu inayowafanya wauzaji kushindwa kuomba rufaa. Maana ushawishi unakuwa mdogo.
Tano: Hawajui namna ya kuomba rufaa.
Hii ni sababu ya mwisho, inayowafanya wauzaji kushindwa kuomba rufaa. Hawakuwahi kufundishwa shuleni au mahali popote ndiyo maana hawaombi. Wanashindwa mahali pa kuanzia.
Je, wanaofanikiwa kuomba rufaa huomba kwa muda upi au mazingira yapi? Hapa chini kuna nyakati nzuri za kuomba rufaa kutoka kwa mteja;
Moja; Baada ya manunuzi kufanyika.
Kwa kuwa tayari mteja katoa pesa. Hivyo, anatamani hata rafiki yake au mtu wa karibu naye atoe pesa kulipia bidhaa.
Mbili; Mteja anaposhukuru.
Kushukuru ni zao la kufurahia huduma. Mteja hawezi kushukuru kama hujamhudumia vema. Hivyo, baada ya mteja kushukuru ni wakati mzuri kuomba maana mteja anatamani pia mwenzake afurahie.
Tatu; Mteja anapokaa kwenye biashara yako muda mrefu.
Huyu ni mteja mzuri kukupa rufaa maana hakai bure kwako kuna kitu kizuri anapata kutoka kwako na anatamani mtu mwingine apate.
Hivyo, ni wajibu wako kama mtu wa mauzo kuweka juhudi na kutoa thamani kubwa kwa mteja unayemuhudumia kwenye biashara yako. Maana kupitia huyo kuna watu wengi unakuja kuwapata.
Wakati wa uwasilishaji wako au mazungumzo yako, jitahidi kujibu mapingamizi unayokutana nayo ili uweze kuongeza namba ya watu unaowauzia kwenye biashara yako. Kwa kila mtu unayezungumza naye au kumuuzia usiache kuomba rufaa. Ni wajibu wako mtu wa mauzo kuomba rufaa.
Fanyia kazi yote uliyojifunza katika makala ya leo. Tuwasiliane 0767702659 au
mkufunzi@mauzo.tz kupata vitabu vyetu vya Mauzo Ni Raha, Mauzo Ni Huduma, Mauzo Ni Mahusiano na Mauzo Ni Mchezo Wa Namba.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi.
Tufuatilie pia www.mauzo.tz