Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Matumizi Bora Ya Muda Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora.

Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Ubora na mafanikio ya mtu yanategemea sana matumizi ya muda alionao.

Habari njema ni kwamba binadamu wote tuna muda uliolingana.

Na habari mbaya ni kwamba wengi wamekuwa wanashindwa kutumia muda wao vizuri ili kufanikiwa.

Hilo linaenda kuwa mwiko kwako leo, kwani unakwenda kujifunza matumizi bora ya muda wako ili kufanikiwa kwenye mauzo.

Kwa kuwa muda ni rasilimali adimu na yenye ukomo, ni wale tu wanaoweza kuutumia ndiyo wanaoweza kufanya makubwa.

Hatua Sita Za Matumizi Bora Ya Muda.

Kuna hatua sita kubwa za kuwa na matumizi bora ya muda kwako binafsi na kwa biashara yako.

Hizi ni hatua ambazo ukizijua na kuzifanyia kazi, utaweza kupata matokeo makubwa mno kwenye maisha yako na mauzo pia.

Karibu ujifunze hatua hizo sita na uende ukazifanyie kazi.

Hatua Ya Kwanza; Gusa Mara Moja.

Unapogusa kitu chochote, kifanyie kazi na kumalizana nacho mara moja. Muda mwingi wa watu huwa unaishia kwenye kugusa kitu, kukipangia muda mwingine kisha kuja kukifanya tena.

Mfano mtu anafungua barua pepe, anasoma na kugundua kuna hatua fulani anapaswa kuchukua, anapanga kuja kukamilisha hilo baadaye na hivyo kufunga barua pepe hiyo kama haijasoma. Hapo ni kupoteza muda kwa sababu jukumu bado linaendelea kuwa kwenye fikra zake.

Zoezi la kufanya; kila unapogusa kitu cha kufanya, malizana nacho kabisa, usikiache kwa ajili ya baadaye.

Hatua Ya Pili; Tengeneza Orodha.

Usiianze siku yako ya kazi bila kuwa na orodha ya majukumu unayokwenda kuyakamilisha kwenye siku hiyo (TO DO LIST).

Majukumu hayo yanapaswa kupangwa kulingana na vipaumbele vyake na hayapaswi kuwa mengi sana. Idadi ya majukumu sita muhimu ya kukamilisha kwa siku ni nzuri ambayo ukiifanyia kazi utakuwa na matokeo mazuri.

Sababu kubwa ya watu wengi kupoteza muda ni kufanya mambo kwa mihemko, kukabiliana na kila jambo linalokuja mbele yao. Wanakuwa hawana kipaumbele chochote kwenye siku yao, hivyo chochote kinachokuja mbele yao kinakuwa ndiyo kipaumbele kwao.

Nyongeza; pia unapaswa kuwa na orodha ya majukumu ambayo hutayafanya kwenye siku yako (NOT TO DO LIST). Haya ni yale majukumu unayopenda kuyafanya ila hayana mchango kwako kuwa bora na kukuza mauzo. Ukishaandaa orodha hiyo ya pili, hakikisha hayo huyafanyi kwenye muda wako muhimu.

Zoezi la kufanya; kila siku orodhesha majukumu yasiyozidi sita ambayo utayakamilisha kwenye siku hiyo. Usiianze siku yako bila orodha ya majukumu ya kukamilisha uliyoiandaa.

Hatua Ya Tatu; Panga Muda Utakaotumia Kwenye Kila Jukumu.

Kwenye majukumu sita uliyopanga kufanya kwenye siku yako, panga muda utakaotumia kufanya kila jukumu. Usikimbilie kupanga utafanya wakati gani, kwanza jua ni muda kiasi gani itakuchukua kufanya kila jukumu.

Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha majukumu uliyopanga yanaweza kufanyika ndani ya siku kama ulivyopanga. Na kama kuna jukumu ambalo haliwezi kuisha ndani ya siku moja, panga ni muda kiasi gani wa siku utaweka kwenye jukumu hilo.

Zoezi la kufanya; mbele ya kila jukumu uliloweka kwenye orodha yako, weka muda utakaohitaji ili kulikamilisha. Kwa majukumu yote yaliyo kwenye orodha yako, hakikisha jumla ya muda wa kukamilisha yote hauzidi muda wako wa kazi kwenye siku.

Hatua Ya Nne; Pangilia Siku Yako.

Baada ya kupanga muda ambao kila jukumu litachukua, sasa unakwenda kuipangilia siku yako, kwa kujua ni jukumu gani unafanya kwenye muda gani.

Pangilia masaa yote ya kazi kwenye siku yako kwa kuyaweka majukumu kwenye muda wa siku kulingana na muda wa jukumu.

Hapa unapaswa kuepuka kuyabananisha majukumu makuu pamoja na pia unapaswa kuacha muda iwapo kutatokea dharura yoyote inayohitaji muda wako. Ndiyo maana ni muhimu majukumu yako makuu yasichukue siku yako nzima. Badala yake uwe na muda kwa ajili ya mambo mengine yanayopaswa kufanyika lakini siyo muhimu kabisa.

Zoezi la kufanya; pangilia siku yako nzima ya kazi, saa kwa saa. Kila saa andika nini utafanya kulingana na orodha yako. Huo unakuwa ndiyo mwongozo wa siku yako nzima ambao unaufuata bila kuuvunja.

Hatua Ya Tano; Weka Vipaumbele.

Kwa majukumu uliyopanga kufanya kwenye siku yako, hayalingani. Kuna ambayo ni muhimu zaidi kuliko mengine. Na kwa yale muhimu zaidi, huwa ndiyo magumu kufanya, hivyo wengi huwa wanakwepa kuyafanya na kukimbilia yale rahisi.

Bila ya kuweka vipaumbele, utajikuta kila siku inaisha ukiwa umechoka, lakini hakuna makubwa ambayo unakamilisha. Hivyo anza kwa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kabla ya yale ambayo siyo muhimu.

Tunaijua kanuni ya Pareto inayosema asilimia 80 ya matokeo inatokana na asilimia 20 ya juhudi. Maana yake kuna majukumu machache ambayo ukiyakamilisha matokeo unayoyapata yanakuwa makubwa.

Anza na majukumu hayo machache muhimu zaidi na usiruhusu usumbufu wa mambo mengine nje ya ulivyopanga.

Kwenye mauzo, kipaumbele cha kwanza ni kuwafikia wateja kwa njia mbalimbali ambazo tumeshashirikiana. Hivyo asilimia 80 ya muda wako wa kazi kwenye mauzo unapaswa kutumika kwenye kuwagusa wateja. Yaani kama unafanya kazi masaa 10 kwa siku, masaa 8 unapaswa kuyaweka kwa wateja moja kwa moja na masaa 2 ndiyo unafanya mambo mengine ya kwenye biashara.

Bila ya kuwa na vipaumbele sahihi kila siku itaanza na kuisha bila ya kukamilisha yaliyo muhimu na hatimaye kukwama bila kupiga hatua.

Zoezi la kufanya; kwenye kutekeleza majukumu ya siku, anza na yale makubwa na muhimu, ambayo pia huwa ndiyo magumu zaidi. Ukiyaanza hayo mapema wakati bado una nguvu, utaweza kuyafanya vizuri. Lakini ukiyasogeza mbele kwenye siku yako, inakuwa rahisi kuyaahirisha.

Hatua Ya Sita; Jiulize, “Je Itadhuru Nikitupilia Mbali?”

Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 80 ya vitu ambavyo watu wanahifadhi kwa ajili ya baadaye huwa hawavitumii au kuvifanyia kazi tena. Lakini bado watu huwa wanajidanganya kwa kuhifadhi vitu kwa ajili ya baadaye.

Tukirudi kwenye hatua ya kwanza, unapaswa kugusa kitu mara moja tu. Na kama kitu unaona utakihitaji tena baadaye, jiulize kama itadhuru ukikifuta kabisa. Mara nyingi huwa haina madhara, hivyo ni bora kufuta kuliko kukiacha tu kikisubiria.

Zoezi la kufanya; achana na vitu vingi ambavyo umevishikilia na vinachukua muda wako mwingi. Futa, ondoa na achana na vilivyo vingi, kama utakuja kuvihitaji baadaye, utavipata tu.

Neno muhimu kutumia kwenye muda.

Kwa umuhimu ambao muda unao, watu wengi wamekuwa wanauwinda sana. Wanaoutaka muda wako ni wengi kuliko unavyoweza kuwapa.

Na pia mambo ya kufanya ni mengi kuliko muda ulionao. Hayo yote yanafanya muda kuwa na uhaba mkubwa na wengi kushindwa kuutumia kwa tija.

Lipo neno moja unalopaswa kulifanya kuwa rafiki kwako na kulitumia kila mara ili kulinda muda wako na kuutumia vizuri. Neno hilo ni HAPANA. Hapana siyo tu neno, bali ni sentensi iliyokamilika, ikiwa na maana ukishasema hapana hulazimiki kujieleza zaidi.

Sema hapana kwa jambo lolote unalishawishiwa au kushawishika kufanya nje ya orodha yako na mpangilio wako wa siku.

Kama ni jambo muhimu limejitokeza, liweke kwenye orodha na kulifanya kama muda utabaki.

Hapana ni neno ambalo unalitumia hata kama hutaki. Kwa sababu hata kama utawaambia wengine NDIYO ili kuwaridhisha, utakuwa umejiambia wewe HAPANA.

Unaposema ndiyo kwa chochote nje ya mipango yako, maana yake umesema hapana kwenye mipango uliyonayo. Kitu ambacho siyo sahihi kwako wala mipango yako.

Jiheshimu wewe mwenyewe na muda wako kwa kutumia sana neno HAPANA.

Tumia muda wako vizuri ili uweze kuwa bora wewe mwenyewe na kisha kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea.

Wajibu wako mkubwa ni kusimamia hatua hizi sita muhimu;

• Gusa kitu mara moja.

• Tengeneza orodha ya majukumu sita muhimu ya kukamilisha kwenye kila siku yako.

• Panga ni muda kiasi gani kila jukumu litachukua.

• Pangilia muda ambao utakamilisha kila jukumu kwenye siku yako.

• Weka vipaumbele kwa kuanza na majukumu magumu na muhimu.

• Jiulize, “Je Itadhuru Nikitupilia Mbali?”

Huhitaji kufanya mambo mengi ili kutumia vizuri muda wako, unachohitaji ni kubobea kwenye mambo haya sita pekee. Yafanye wewe kila siku na hakikisha kila mtu aliyepo kwenye biashara yako anayajua na kuyafanya.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.

Kocha Dr. Makirita Amani,

Mkuu wa CHUO CHA MAUZO

www.mauzo.tz

Leave a comment