Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Majukumu Ya Msakaji Kwenye Kukuza Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya mauzo, eneo la usakaji.

Haya ni masomo yanayotuwezesha kutafuta wateja tafajiwa wapya kwa wingi zaidi kwenye biashara zetu ili tuweze kukuza mauzo.

Kauli mbiu yetu ni; USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Ni kupitia kusaka ndiyo biashara inatengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi.

Programu yetu ya CHUO CHA MAUZO inagawa mauzo kwenye sehemu tatu muhimu ambazo zote zinachangia kukuza mauzo.

Sehemu hizo ni USAKAJI ambao ni kufikia wateja kule walipo, UKAMILISHAJI ambao ni kuwashawishi wateja wakubali kununua na UHUDUMIAJI ambao ni kuhakikisha wateja wanapata yale waliyoahidiwa.

Usakaji ni kuwafikia wateja kule walipo, kuhakikisha wanaijua biashara na biashara inakuwa na taarifa zao kwa ajili ya kuwafuatilia.

Anayefanya kazi hiyo ya kuwafikia wateja kule walipo ndiyo anaitwa Msakaji.

Msakaji ni mtu muhimu sana kwenye biashara na ukuaji wa mauzo kwa sababu ndiye anayeiwezesha biashara kutengeneza wateja wapya.

Ni kupitia wateja wapya ndiyo biashara inapata nafasi ya kukua zaidi.

Majukumu makuu ya Msakaji.

Ili kutimiza lengo la biashara kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi, msakaji anakuwa na majukumu yafuatayo kwenye biashara.

1. Kuwafikia wateja kule walipo.

Wajibu mkubwa wa Msakaji ni kutoka na kuwafikia wateja kule walipo. Badala ya biashara kuwasubiri wateja waje, msakaji anawafuata wateja kule walipo.

Lengo ni kuhakikisha wateja wanaijua biashara na biashara pia inawajua wateja.

Kwa biashara kuwajua wateja inakuwa na ufuatiliaji endelevu ambao unawashawishi wateja kununua.

2. Kupokea wateja kutoka kwenye masoko.

Msakaji pia ana jukumu la kuwapokea wateja kutoka kwenye masoko yanayofanyika kwenye biashara.

Kwa mfano kama biashara inafanya matangazo yanayowataka wateja kuchukua hatua fulani, kama kutembelea biashara, kupiga simu au kutuma taarifa zao, msakaji ndiye anayewapokea kwa mara ya kwanza.

Tofauti ya usakaji na masoko ni kwenye masoko wateja wanaijua biashara, wakati kwenye usakaji biashara inawajua wateja.

3. Kuwachuja wateja kulingana na sifa.

Siyo wateja wote tarajiwa wanaifaa biashara, hivyo kuna sifa za kuwachuja wateja hao tarajiwa ili kubaki na wale walio sahihi na kuwafuatilia kwa uhakika.

Msakaji ndiye anayefanya kazi hiyo ya kuwachuja wateja na kubaki na wale ambao wakifuatiliwa wanaweza kuwa na manufaa kwenye biashara.

Ndiyo maana msakaji anakuwa wa kwanza kuwapokea wateja kutoka kwenye masoko, ili kuchuja wale wenye sifa ambao wataendelea kufuatiliwa zaidi.

4. Kuwazoesha wateja tarajiwa kwenye biashara.

Wateja tarajiwa wanaposikia kuhusu biashara kwa mara ya kwanza huwa wanapuuza, kwa sababu hawaijui biashara. Wanahitaji kusikia mara kwa mara mpaka waizoee biashara na kuwa tayari kununua.

Msakaji ndiye mwenye jukumu la kuwazoesha wateja tarajiwa kwenye biashara.

Anafanya hivyo kupitia ufuatiliaji endelevu ambao anaufanya kwa wateja tarajiwa wenye sifa.

Wateja tarajiwa wakishakuwa na sifa, wanapaswa kufuatiliwa kwa uendelevu bila kuachwa, haijalishi inachukua muda mrefu kiasi gani.

Ufuatiliaji endelevu una nguvu ya kuwafanya wateja waizoee biashara na kuwa tayari kununua.

5. Kuwapeleka wateja tarajiwa kwa wakamilishaji.

Msakaji atamchakata mteja tarajiwa mpaka anapokuwa tayari kununua kisha kumpeleka kwa mkamilishaji ili aweze kumkamilisha kwa kumuuzia.

Ni muhimu sana msakaji kumchakata mteja tarajiwa mpaka aizoee biashara kabla ya kumkabidhi mkamilishaji aendelee naye.

Hilo linawafanya wateja kuwa rahisi kukamilika, lakini pia inaokoa muda wa wakamilishaji, kuepuka kufuatilia wateja ambao wapo mbali na kununua.

Kwa ufuatiliaji endelevu wa wateja tarajiwa, msakaji anakuwa anajua wale ambao wameshafikia kununua na kuwasogeza kwa wakamilishaji.

Wasakaji wanafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na wakamilishaji ili kuhakikisha wateja tarajiwa wenye sifa wananunua kwenye biashara.

Sifa na ujuzi wa msakaji kuwa nao.

Ili kuweza kufanikiwa kwenye kutekeleza majukumu yake, Msakaji anapaswa kuwa na sifa na ujuzi ufuatao.

1. Kuwa na ujuzi wa kuwatembelea wateja na kuwafikia kule walipo. Hapa ushawishi wa kukutana na watu ana kwa ana unahitajika.

2. Ujuzi wa kuwasiliana na wateja kwa njia ya simu unahitajika, hasa kwa wateja ambao hawaijui biashara. Msakaji anapaswa kuwa mzuri kwenye simu ili kuweza kuwafikia wateja tarajiwa wengi zaidi.

3. Matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazorahisisha kuwafikia wateja ni ujuzi ambao msakaji anapaswa kuwa nao. Teknolojia hizo ni mitandao ya kijamii na njia zake mbalimbali za kuwafikia wateja.

4. Kujisimamia mwenyewe ni sifa muhimu ambayo msakaji anapaswa kuwa nayo ili kufanikiwa kwenye majukumu yake. Hiyo ni kwa sababu mara nyingi Msakaji anakuwa anafanya kazi nje ya biashara hivyo kukosa usimamizi wa moja kwa moja.

Kama msakaji hawezi kujisimamia mwenyewe kwenye kutekeleza majukumu yake, hataweza kuyakamilisha kwa usahihi.

5. Ung’ang’anizi ni muhimu. Usakaji ni zoezi lenye kukataliwa kwa hali ya juu sana. Hiyo ni kwa sababu wateja wanapofikiwa kwa mara ya kwanza wanakuwa hawaijui biashara, hivyo wanakataa. Msakaji lazima awe na ung’ang’anizi wa hali ya juu wa kuendelea kuwafuatilia wateja hata pale wanaposema hapana. Kwa sababu inachukua muda mpaka wateja kuizoea biashara na kukubali kununua kwa mara ya kwanza.

Wasakaji ni watu muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara kupitia kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi.

Wasakaji wakiwa na sifa sahihi na kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu, biashara inanufaika na ongezeko la wateja na hatimaye mauzo.

Usakaji ndiyo pumzi ya biashara, unapaswa kufanyika mara zote.

Kocha Dr. Makirita Amani,

Mkuu wa CHUO CHA MAUZO

www.mauzo.tz

Leave a comment