Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Uwasilishaji Unaoenda Kukupa Ushindi Mbele Ya Mteja Na Kuongeza Ushawishi

Ndugu, Ni imani yangu kuwa umewahi kwenda sehemu kwa ajili ya mazungumzo na mtu. Iwe unajua unachoenda kuzungumza au hukuwa unajua. Ila kuna vitu uliona katika mazungumzo hayo. Kuna namna uliona ugumu fulani kuzungumza kitu chako lengwa.

Hiyo ndiyo changamoto wanayokutana nayo wengi wetu hasa pale wanapoenda kukutana na watu baada ya kuwaomba miadi. Maswali mengi yamekuwa ninaweza kuanzia wapi kuzungumza, vipi kuhusu kumshawishi? Makala ya leo inayo jawabu, ifuatilie;

Miadi ni ahadi iliyotolewa na kukubaliwa ya kukutana na mtu kwa wakati, mahali fulani na mada maalumu. Ahadi inahusisha ukutanishaji wa pambe mbili. Kwenye mauzo miadi ina maana muuzaji anakutana na mteja. Mnakutana mahali fulani na mnakuwa na mada ya mazungumzo ndani ya muda husika.

Unachopaswa cha kwanza kuhusiana na miadi ni hiki; miadi sio mauzo au kuuza. Ila ni sehemu tu unayoweza kutumia kuuza. Usije kusema kwa kuwa mteja fulani amenipa miadi ninaenda kumuuzia. Sio kweli, mnaweza kufanya miadi hata mara nne bila kumuuzia. Hili lazima ulijue ili ujiandae kisaikolojia kwa matokeo yoyote yatakayojitokeza.

Miadi inakupa nafasi ya kuelezea kwa kina kuhusu bidhaa au huduma yako kwa mteja. Inapotokea ukakutana na mtu asiye na uhitaji wa bidhaa yako usimuache au kusema ndio basi tena huwezi kuuza. Unacho kitu kimoja cha kumuomba. Muombe akusaidie mtu au watu wanaoweza kunufaika na biashara yako.

Mteja anapokupa watu, ongea nao. Waambie jinsi ulivyoongea na mhusika, akawa hana utayari kwa muda huo labda kulingana na sababu nje ya uwezo wake, ndipo akaona ni bora akupatie mtu kama yeye mwenye uwezo wa kunufaika na bidhaa yako. Mazungumzo yakiwa mazuri weka miadi ya huyo mteja muongee zaidi. Ukimpata na yeye muombe rufaa. Hili zoezi ni endelevu halina ukomo.

Unapoenda kukutana na mteja ni vizuri kuwa na kitu cha kuzungumza naye. Bila hivyo utaanza kubabaika na kupoteza muda. Ndiyo maana tunasema unahitaji kuwa ya mada ya mazungumzo, utakayoiwasilisha mbele ya mteja. Usije kufanana na bwana mmoja aliyekutana na Bill Gate, akaanza kumshangaa na kukosa kitu cha kuzungumza naye.

Kwenye kuwasilisha mada yako tambua kuwa uwasilishaji sio mauzo bali ni sehemu ya mauzo. Isije kuwa unaenda kuwasilisha kitu chochote kwa mteja ukajua umeuza tayari sio kweli. Unaweza kuwasilisha na usiuze. Kwa sababu kadhaa labda uwasilishaji wako haukuwa mzuri au hujaweza kuwashawishi watu kuungana wewe kwenye biashara yako.
Mambo ya kuzingatia kwenye uwasilishaji;

Moja; Mada ya mazungumzo. Hapa unaelezea kile unachoenda kuwasilisha mtu anajua na anajiandaa kwa hilo.

Mbili; Wahusika. Ni mteja unayekutana naye, hivyo lazima ujiulize ninaenda kuzungumza na nani? Hii inakusaidia katika kuwasilisha kwako kitu, ikiwa ni mtu wa kawaida kuna mahali unapaswa kuishia. Kama unayeongea naye ni mfanya maamuzi kwa maana ya meneja au bosi mwenyewe kuna namna ya kuongea naye.

Tatu; Muda. Lazima ujue muda unaoenda kutumia. Hii itakuepusha kuongea bila kuwa na mpangilio.

Muda; Tatizo. Uwasilishaji wako unaenda kugusia wapi. Na hapa ndipo kuna kiini cha uwasilishaji.

Uwasilishaji wa kwanza sio wa kuuza kamwe. Ondoa wazo hilo, itakusaidia kuweka mkazo ili baadaye upate nafasi ya kuwauzia baadaye katika uwasilishaji mwingine na hii inafanya kazi iwe ana kwa ana au kwa njia ya simu.

Ikitokea mteja akashawishika kununua sawa. Ila usiuchukulie kama wa kuuza moja kwa moja. Hivyo, jitahidi ufanye maandalizi mazuri kabla hujaanza uwasilishaji.

Je, uwasilishaji wako unayazingatia hayo?

Habari Njema Ni Kwamba Kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo tayari Hardcopy. Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu ushawishi unahitaji kuwa nao na namna nzuri ya kutoa huduma bora. Tuwasiliane 0767702659, utafikishiwa popote Tanzania karibu tujifunze zaidi.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.

Hakika; Mauzo ni huduma na huduma ni mauzo.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi

Leave a comment