Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Sheria 20 Za Ukamilishaji Wa Mauzo-2

Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,

Leo ikiwa ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC:ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Leo tunakwenda kumalizia sehemu ya pili ya sheria 20 ambapo wiki iliyopita tuliangalia sheria namba moja mpaka kumi na leo tutaangalia sheria namba 11-20.

Eneo la ukamilishaji ndiyo eneo ambalo tunapaswa kuwa nalo makini, bila kukamilisha mauzo maisha yako hayawezi kwenda kwa sababu, mauzo ndiyo yanaleta fedha mfukoni.

 1. Mara zote jua mtafikia makubaliano.

Ipo kauli ya Kiswahili inayosema penye nia pana njia. Huo ndiyo mtazamo unaopaswa kwenda nao kwenye ukamilishaji, kuwa na nia ya kufikia makubaliano. Kwa nia hiyo, njia itajitokeza. Haijalishi mteja amejipanga kiasi gani kukupinga, kwa kuamini mtafikia makubaliano, utaona njia ya kuweza kufikia makubaliano. Linda sana fikra na mtazamo wako, usikubali kuingiza mawazo yoyote hasi au wasiwasi kwamba hutaweza kukamilisha mauzo. Uimara wa fikra ni muhimu sana kwenye ukamilishaji wa mauzo.

 1. Mara zote kuwa chanya bila kujali mteja amekujibu nini.

Mteja anaweza kukujibu vibaya, akakukatisha tamaa na kufanya vitu ambavyo vinaweza kukukasirisha. Wewe hakikisha unabaki chanya na imara mara zote. Uimara wako na kubaki chanya kutafanya hata wateja wakuheshimu, maana wengi hutegemea ukasirishwe na yale wanayokuwa wamefanya. Kwa kuendelea kuwa chanya na kumshawishi mteja akubali kile unachompendekezea, inakupa wewe nguvu kubwa ya kuaminika na kukubalika. Kuwa chanya, mara zote.

 1. Mara zote kuwa na tabasamu, bila kujali nini kimetokea.

Tabasamu huwa lina nguvu kubwa kwako mwenyewe na kwa wale unaokuwa unawashawishi. Hivyo mara zote kuwa na uso wa tabasamu, inakufanya weweujisikie vizuri na inawafanya wengine wavutiwe na kuwa tayari kufunguka kwako.

Hata kama hujisikii au huna tabasamu, igiza kuwa na tabasamu na utanufaika na hilo. Hakikisha uigizaji wako wa tabasamu ni halisi ili watu wasione unalazimisha. Kila siku na kila wakati fanya zoezi la kutabasamu ili iwe kitu cha kawaida kwako. Unapokuwa kwenye ukamilishaji wa mauzo, kiwe kitu cha kawaida kwako na siyo cha kulazimisha.

 1. Wachukulie wateja wanaweza.

Vile unavyowachukulia watu ndivyo wanavyokuwa au wanavyokujibu. Ukichukulia watu wanaweza, wataweza na ukiwachukulia hawawezi basi pia hawataweza. Kwa kila mteja unayeingia naye kwenye mchakato wa ukamilishaji, wachukulie wanao uwezo na wapo tayari kukamilisha manunuzi hapo hapo. Hilo litakupa nguvu ya kuendelea kung’ang’ana hata pale wanapokuwa na mapingamizi mbalimbali. Kuwa na uhakika kwamba wateja wako wanaweza kununua na simamia hilo, watanunua kweli.

 1. Watambue na kuwasifia wateja.

Kwa chochote ambacho wateja wanasema au kufanya, kitambue na kuwasifia au kuwashukuru. Hata kama ni kitu kidogo kuliko ulivyotegemea, anza kwa kutambua hicho walichofanya na kuwasifia au kuwashukuru. Hilo litawaweka wateja katika upande wa kujisikia vizuri na hivyo kuwa rahisi kushawishika zaidi na wewe. Kwa mfano pale mteja anapokupa bei yake, hata kama ni ndogo kuliko unayouzia, anza kwa kutambua na kumpongeza kwa kuwa tayari kulipia kiasi hicho, kisha endelea na kumwonyesha thamani zaidi ili awe tayari kulipa zaidi.

 1. Mara zote kubaliana na mteja, usipingane naye.

Mara zote kubaliana na chochote kile mteja anachosema au kufanya. Kitu unachopaswa kuepuka sana kwenye ukamilishaji na majadiliano na mteja ni kupingana na kubishana. Kwani mteja atasimamia upande wake na iwe uko sahihi au la, yeye ndiye atakayeshinda. Kwani hata kama utakuwa sahihi, yeye akiamua asinunue wewe ndiye unakuwa umeshindwa. Hivyo anza kwa kukubaliana naye kwa chochote anachosema au kufanya, kisha endelea na mchakato wa kumshawishi. Hakuna kitu kinaua ubishani haraka kama kukubali, kubali na mteja atakosa cha kubishana hivyo kuwa tayari kukusikiliza.

 1. Mara zote tafuta suluhisho. Dunia imejaa watu ambao wana mtazamo wa mambo ni magumu na hayawezekani. Watu ambao wanaangalia matatizo na kuona ni makubwa na
  yaliyoshindikana. Watu wa aina hiyo huwa hawafanikiwi kukamilisha mauzo. Wewe kuwa tofauti, kuwa na mtazamo wa inawezekana na kwa kila tatizo wewe tafuta suluhisho. Kwa kuwa upande wa kutafuta suluhisho, utaweza kuona njia za kutatua au kuvuka matatizo na vikwazo mbalimbali. Kwa kuwa mtu wa kutafuta suluhisho, utaweza kuvuka mapingamizi ambayo mteja anakupa na kumshirikisha katika kupata suluhisho na hatimaye kufikia hitimisho la kukamilisha.
 2. Jali sana kiasi cha kukataa kutokukamilisha.
  Unapaswa kukubali sana kile unachouza na kujali sana maslahi ya mteja kiasi kwamba unakataa kutokukamilisha mauzo. Hata mteja awe mbishi na kukataa kiasi gani, ona ni wajibu wako kuhakikisha anaelewa na kukubali, kwa sababu ni kitu sahihi na muhimu sana kwake. Kataa kabisa kutokukamilisha mauzo kwa sababu yoyote ile. Ona ni wajibu wako wa kimaadili kukamilisha mauzo, kwa sababu ulichonacho ndicho mteja anakihitaji zaidi. Unganisha kile unachouza na kusudi la maisha yako na hiyo itakupa msukumo mkubwa wa kuendelea licha ya magumu utakayokutana nayo. Huwezi kukubali chochote kikukwamishe katika kutimiza kusudi lako, na hivyo hutakubali kutokukamilisha mauzo. Wengi wanashindwa kuuza kwa sababu wanashindwa kuunganisha mauzo na kusudi la maisha yao, kwa sababu wengi hawajui hata kusudi la maisha yao. Jali zaidi na utakamilisha mauzo mengi zaidi.
 3. Tumia silaha zote za ukamilishaji. Haina maana kuwa na silaha nyingi kama huzitumii. Ondokana na mazoea ya kutumia silaha au zana ambazo umekuwa unatumia mara kwa mara. Fanyia kazi zana nyingi tofauti tofauti na zitumie wakati wa ukamilishaji wa mauzo. Kadiri unavyokwenda kuna zana chache utakazozipenda kwa sababu zina matokeo mazuri kwako, lakini hilo lisifanye uache kufanyia kazi zana nyingine. Kuna wakati utahitaji kuwa na zana nyingi zaidi, hivyo mara zote kuwa tayari kuzitumia.
 4. Mara zote jua hakuna kinachotokea kama mauzo hayatakamilishwa. Ukamilishaji wa mauzo ndiyo hatua muhimu sana kwenye mchakato wa mauzo. Kwani kama mauzo hayatakamilishwa, hakuna kitakachoweza kutokea. Masoko, uwasilishaji, kujenga imani, kufanya majaribio na mengine mengi yanayofanyika kwenye mchakato wa mauzo, hayatakuwa na maana kama mauzo hayatakamilishwa. Ni ukamilishaji wa mauzo ndiyo unaoleta fedha kwenye biashara, hivyo eneo hilo linapaswa kupewa uzito unaostahili. Kila muuzaji anapaswa kujua umuhimu wa hatua ya ukamilishaji na kuhakikisha anakuwa vizuri kwenye hatua hiyo ili kuweza kukamilisha mauzo kwa wingi zaidi. Zingatia sheria hizi 20 ulizojifunza hapa na utaweza kukamilisha mauzo mengi kitu kitakachokupa mafanikio unayoyataka kwenye maisha yako.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

Leave a comment