Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Sheria 20 Za Ukamilishaji Wa Mauzo-1

Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea,

Leo ikiwa ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu;
ABC -ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA

Tunakwenda kupata sheria 10 za ukamilishaji wa mauzo.

Mauzo ni mchezo na kila mchezo huwa una sheria zake. Ili uweze kupata ushindi kwenye mchezo wowote ule, unapaswa kuzijua sheria zake na kuzizingatia. Kwa mfano, kwenye CHUO CHA MAUZO tuna mambo ya kuzingatia kama vile sheria 13 za mauzo, maneno 24 ya ushawishi, mambo 16 ya kuzingatia wakati wa mazungumzo na mambo 10 ya kuzingatia wakati wa ukamilishaji wa mauzo.
Haya yote ukiyafanyia kazi yatakupa matokeo mazuri kwenye mchakato mzima wa mauzo.

Kuna sheria 20 za msingi kabisa kwenye hatua ya ukamilishaji mauzo, ambazo unapaswa kuzijua na kuzizingatia ili uweze kukamilisha mauzo kwa uhakika. Hapa tunakwenda kujifunza sheria hizo na jinsi ya kuzifanyia kazi. Na leo tutapata sheria 10 tu na wiki ijayo tutapata sheria 10 nyingine.

1. Kamilisha na jadiliana ukiwa umekaa. Kamwe usifanye ukamilishaji au majadiliano ya ukamilishaji ukiwa umesimama. Kufanya hivyo kunapeleka watu wasikupe uzito unaostahili na hivyo kutokushawishika. Fanya uwasilishaji wako ukiwa umesimama, lakini inapofika kwenye ukamilishaji au majadiliano, hakikisha wewe na mteja wote mmekaa.
Hii inatoka na aina ya biashara unayofanya, kama biashara yako inahitaji mtu akae fanya hivyo hata mteja anapokuja na mko kwenye makubaliano ya bei mpe kiti akae au kaeni mezani mtakamilisha dili nzuri.

2. Wasilisha mapendekezo yako kwa maandishi.

Watu huwa hawaamini kile wanachosikia, bali wanachoona. Hivyo baada ya uwasilishaji na majadiliano, weka mapendekezo yako kwa maandishi. Watu wanaposoma kitu wanakipa uzito mkubwa kuliko wanaposikia pekee. Kuwa pia na utaratibu wa kuchukua notisi pale mtu anapokuwa anaongea, anaona unaweka umakini mkubwa. Na muhimu zaidi, chochote unachomwelewesha mteja, fanya hivyo kwa maandishi, kinaeleweka zaidi.
Kwa mfano, kama unafanya biashara inayohusu mambo ya mikataba, hakikisha unatumia hii sheria.

3. Kuwa na uwasilishaji unaoeleweka.

Fanya mazoezi ya kutosha kwenye uwasilishaji wako kabla ya kuwasilisha kwa mteja, ili unapofika kwa mteja uweze kuwasilisha kwa usahihi na kwa kueleweka. Kuwa na wasiwasi au kutokujiamini wakati wa uwasilishaji unapunguza ushawishi wako kwa watu. Kuwa na uwasilishaji bora kwa kufanya mazoezi na kuboresha kila hatua.

4. Waangalie machoni.

Pale unapokuwa unaongea na mtu, hakikisha unamwangalia machoni. Hilo linawafanya waone una umakini na kujiamini kwenye kile unachoongea, kitu ambacho kitawafanya washawishike zaidi. Kama unaangalia chini au pembeni wakati unaongea na wengine, wataona hujiamini hivyo kutokushawishika.

5. Mara zote kuwa na kalamu. Unapokwenda kwenye mazungumzo ya ukamilishaji wa mauzo, hakikisha umebeba mkataba wa manunuzi na kalamu ya mteja kuweka sahihi kwenye mkataba huo. Nenda ukiwa na maandalizi ya kutosha kukupa ushindi. Hakuna kitu kinakwamisha kama umekazana kumshawishi mteja na akakubali, lakini huna kalamu. Kwa mfano, unafanya biashara ambayo mtu anapaswa kuweka sahihi yake, hakikisha unafanya hivyo, kuwa na kalamu kabisa hata mbili ili moja ikigoma unayo nyingine itakayokusaidia kumsainisha.

6.Tumia vichekesho kupunguza shinikizo.
Wafanye wateja wacheke na itakuwa rahisi kuwashawishi kununua. Hatua ya kukamilisha mauzo ina shinikizo na msongo mkubwa. Hilo huwafanya wateja kuwa upande wa kujihami na kujiandaa kupinga chochote unachowaambia. Ili kuvunja huo ukuta, unapaswa kuwachekesha. Wape hadithi na mifano inayochekesha, wakicheka wanaondoa msongo na kuvunja ukuta wa kujihami, kitu kinachowafanya wawe wazi kushawishika.

Epuka kutumia vichekesho vyenye ubaguzi au vinavyoweza kutafsiriwa kama matusi au udhalilishaji kwa wengine. Angalia kwenye jamii, watu huwa tayari kulipa gharama kubwa kwenye burudani kuliko kwenye elimu. Hiyo ni kwa sababu burudani zinawafanya watu wajisikie vizuri na watu wanapenda sana kujisikia vizuri.

Fanya mchakato wako mzima wa ukamilishaji kuwa mchezo ambao unawapa watu burudani, wanacheka na kufurahi na watakuwa tayari kukubaliana na wewe.

7. Mara zote uliza zaidi. Ukamilishaji siyo rahisi, ndiyo maana wengi wanashindwa kukamilisha. Lazima uwe king’ang’anizi na usiyekata tamaa. Hiyo ni kwa sababu utakataliwa mara nyingi. Pale mteja anapokuambia hapana au sitaki, haimaanishi ndiyo mwisho wa mchakato. Unatakiwa kujiuliza hujamwambia nini, kisha kumuuliza tena. Endelea kuuliza bila kuchoka mpaka pale unapopata jibu la ndiyo. Kama kile unachouza kina manufaa kwa mtu na unaamini hilo bila shaka, usikatishwe tamaa na majibu yake ya hapana, endelea kuuliza mpaka akubali.

8. Kuwa na silaha nyingi za ukamilishaji ili usirudie zile zile. Ukiwa na silaha chache na kuzitumia hizo kila wakati huwa zinakosa nguvu kwa watu kuzizoea. Unapaswa kuwa na silaha nyingi ili kila wakati uwe na silaha mpya unazotumia ambazo wateja hawajawa na kinga nazo. Hapa unahitaji kuweka juhudi sahihi kwenye kujifunza na kufanya mazoezi ili uwe na uwanja mpana wa kuwashawishi wateja.

9. Tumia muda mwingi na mteja. Wakati wa mchakato wa ukamilishaji, tumia muda mwingi kuwa na mteja. Ukimwacha mteja peke yake kwa muda mrefu, unamfanya ajipe wasiwasi juu ya manunuzi unayomshawishi. Hupaswi kumwacha mteja na fikra zake kwa muda mrefu, unapaswa kuwa naye karibu, kuhakikisha unamfanya awe na fikra sahihi za kuhitaji kile unachomuuzia. Usimpe mteja upendo wa kuwa na wasiwasi juu ya kile unachomshawishi kununua.

10. Mchukulie kila mteja kama mnunuaji. Usiende kwenye mchakato wa ukamilishaji wa mauzo ukiwa unajiambia mteja siyo mnunuaji. Ukiwa na mtazamo huo ni bora hata usiingie kwenye mchakato huo, kwa sababu hayo ndiyo matokeo utakayoyapata.

Ingia kwenye mchakato wa ukamilishaji ukiwa na uhakika, bila ya shaka yoyote kwamba mteja ni mnunuaji na unakwenda kukamilisha mauzo. Mtazamo na imani hiyo vitakupa nguvu ya kuendelea kuwa na msisitizo kwa mteja kumshawishi akubali kununua. Haijalishi mteja anakupa sababu gani, wewe jiambie huyu anakwenda kununua na kweli atanunua.

ABC:ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

1 Comment

  • Faraji
    Posted November 30, 2023 at 5:38 am

    Mchukulie kila mteja kama mnunuaji

Leave a comment