Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Jinsi Ya Kutumia Silaha Ya Ushawishi Ya Dhamira na Msimamo Kwenye Mauzo

Karibu sana kwenye jumamosi ya ushawishi huku tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema; HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Sisi binadamu huwa tunapenda kuonekana ni watu wenye msimamo.
Hivyo basi, kama mtu akianza kufanya kitu mara moja atataka kukiendelea ili kulinda ile dhamira na msimamo wake aliouonesha.
Hakuna mtu asiyependa kuonekana haaminiki na kukosa msimamo kwenye maisha yake.

Kwa kawaida, huwa tunapenda kuonekana tuna msimamo ili watu wengine waweze kutuamini na kututegemea.

Pale tunapokuwa tunaahidi kitu, huwa tunasukumwa kukitekeleza na tunapoanza kitu kimoja, inakuwa rahisi kwetu kuendelea na kitu kingine.

Kwa mfano kwenye jamii, silaha ya dhamira na msimamo, ina nguvu kubwa kwenye ushawishi kwa sababu ni kitu ambacho kinathaminiwa sana kwenye jamii.
Watu huwa wanahukumiwa kulingana na msimamo walionao.
Kama mtu hana msimamo, yaani matendo yake hayaendani na vile anavyoonekana kuwa huwa haaminiwi kwenye jamii.

Na jamii huwa inawathamini sana wale ambao wana msimamo. Amhao imani, maneno na matendo yao vinaendana.

Na kinachochea msimamo ni dhamira. Pale mtu anapokuwa anadhamiria kufanya kitu, hapo ulipo msimamo unapoanzia, atahakikisha anakifanya kama alivyodhamiria kufanya na ataendelea kufanya.

Dhamira huwa ina nguvu zaidi pale inaposemwa hadharani au mtu kuandika na kuweka sahihi kile alichodhamiria.
Na mara nyingi watu wakifanya hivyo wanataka kuonesha msimamo wao.

Sasa tunatumiaje hii silaha ya ushawishi ya dhamira na msimamo kwenye mauzo?

Tunatumia hii pale tunapomshawishi mteja kununua kitu kimoja ni rahisi mteja kununua kitu kingine yaani kufanya mauzo ya ziada.
Kwa sababu, mtu akishanunua mara moja anataka kuendelea kuonesha msimamo wake wa kununua.

Anza kumshawishi mteja anunue kitu kimoja ili aendelee tena kufanya yale unayokuwa unamshawishi afanye. Kwa mfano mteja akinunua kitu kimoja, mpendekezee tena kitu kingine cha mauzo ya ziada.
Kumbuka, mauzo ya ziada yanapaswa kuwa madogo kuliko mauzo ya awali.

Mtu akishafanya mauzo yoyote yale ni rahisi kumuomba mteja yafuatayo;

Mteja wa rufaa. Kama mtu amenunua hawezi kuona shida kukupatia mtu mwingine ambaye atakuja kununua kwenye kile unachouza.
Na wateja wa rufaa ndiyo wateja rahisi kufanya nao biashara kwa sababu watu wapoambiana wanakuwa wanaaminiana sana. Kwani neno la mdomo lina nguvu sana.

Simu, mtu akikubali kununua ni rahisi kukupa namba ya simu kwani kama ameweza kununua ya nini akunyime na namba ya simu?

Tunatumia silaha hii ya ushawishi, kumshawishi mteja akubaliane na sisi kwenye kitu fulani. Mteja akisema ndiyo mara moja, ni rahisi kusema ndiyo nyingine zaidi. Na wengi wanapenda kuendeleza kile walichoanzisha ili waonekane kwamba ni watu wa msimamo.

Hatua ya kuchukua leo; mshawishi mteja akubaliane na wewe kwenye kitu kimoja ili uendelee kumshawishi kwenye vitu vingine.
Mfanye mteja aseme ndiyo moja ili aendelee kusema ndiyo nyingine kwenye vile utakavyomtaka afanye.

Kumbuka, ni rahisi mteja kukubaliana na wewe kwenye mauzo ya ziada kama tu ulifanikiwa kumshawishi kwenye mauzo ya awali.
Watu wanapenda kuonekana wana msimamo na kuendeleza dhamira yao ya ndani. Itumie hii silaha ya ushawishi kuongeza mauzo zaidi kwenye kile unachouza.

Kauli mbiu yetu ni HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Mwl.Deogratius Kessy
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz

Leave a comment