Ndugu, Mafanikio katika biashara hayapatikani tu kwa kuwa na bidhaa nzuri, bali pia kwa kutoa huduma inayoendana na viwango vya wateja wako. Unaweza kuwa na bidhaa nzuri sana lakini usipate mafanikio kwa sababu unatoa huduma mbovu kwa wateja wako.
Hivyo, ni jambo muhimu sana kwa mjasiriamali au mtoa huduma kwa mteja kutoa huduma bora kwa wateja wake.
Huduma ambayo mtu anapata kwako tu, tofauti na sehemu zingine. Huduma inayofanya kila wakati aiwazie biashara yako. Hiyo ndiyo inaenda kuikuza biashara yako na kuendelea kupata wateja wengi zaidi.
Hapa chini nimeweka mambo ya kuzingatia wakati wa kutoa huduma kwa wateja, ili uwabakize katika biashara yako milele;
Jambo la kwanza; jua bidhaa zako.
Katika mchakato mzima wa kutoa huduma hakikisha angalau unajua bidhaa au huduma mnazotoa.
Lengo ni kupata urahisi pale mteja anapokuuliza kitu. Hali ya kukosa cha kufanya ikijitokeza, inamkatisha tamaa mteja anaona kama kitu alichotarajia kukipata sio sawa. Kuzijua bidhaa ulizonazo inakusaidia kujiamini na kupunguza hofu wakati wa kuongea na mteja. Pia, hukuongezea kasi ya utoaji wa huduma.
Jambo la pili; Tabasamu na uchangamfu wako.
Mteja anapokuja kwako anakuwa na mawazo yake (stress), kitendo cha wewe kuonyesha tabasamu na uchangamfu kinamfanya anasahau mawazo yake na kujiona mpya.
Ndiyo maana tunashauri mara nyingi kwamba unapokuwa katika uhudumiaji unapaswa kuacha habari za nyumbani huko na kuendana na mazingira ya kazini.
Jukumu lako mtoa huduma ni kumhudumia mteja zaidi ya matarajio yake. Hiyo hali inamfanya ajisikie vizuri. Hapo ndipo unasikia mteja anasema nimepata huduma nzuri katika ofisi au kampuni ya fulani. Inapotokea anahitaji bidhaa au huduma kama yako lazima aiwazie biashara yako.
Jambo la tatu; Lugha unayotumia.
Asilimia kubwa ya utoaji wa huduma zetu tunakuwa tunaongea na wateja iwe ana kwa ana au njia nyingine za mawasiliano. Ni mara chache kutumia lugha za ishara au mwili. Pengine tunavitumia vyote kwa pamoja.
Hivyo, lugha unayotoa kwa mteja lazima iwe nzuri na yenye kuvutia huku ikimshawishi kuchukua bidhaa au huduma yako. Lugha inayozingatia heshima na maadili ya jamii husika. Mfano benki wale “Teller” asilimia kubwa kazi yao ni kuwasikiliza wateja na kuwahudumia asilimia kubwa wanatoa lugha nzuri.
Jambo la nne; Muda unaotumia kuhudumia.
Hii inategemea na huduma unayotoa. Hapa kwenye muda ndipo kuna kasheshe, baadhi ya wahudumiaji wamekuwa wanajisahau. Unakuta mteja badala ya kuhudumiwa ndani ya dakika kumi anahudumia ndani ya saa moja au nusu saa. Hii kiujumla inaboa na kukatisha tamaa. Mfano unatoa huduma ya chakula, mteja anayekuja kwako anakuwa na njaa.
Anapokwambia chakula anachotaka maana yake ni kwamba anaangalia muda unaotumia kuleta chakula hicho. Hapo Kuna kuwahi na kuchelewa. Unapochelewa anaona hilo ni doa kesho anaenda sehemu nyingine. Ukiwahi inamtia moyo kesho anarudi katika biashara yako.
Muhimu; Mteja Anachokumbuka kwako ni huduma nzuri aliyopata. Anaweza asikariri sura yako lakini akumbuka namna biashara yako ilivyomhudumia vema. Kama ni hivyo, kwanini usitoe huduma nzuri?
Fanyia kazi yote ukiyojifunza katika makala hii. Habari Njema Ni Kwamba Kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo tayari Hardcopy. Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu namna ya kuwahudumia, kuomba rufaa, kuwafuatilia na kuwabakiza Katika biashara yako milele. Ni wewe tu kuchukua kitabu hicho kwa ajili ya kupata maarifa zaidi.
Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.
Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi
Hide comments