Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Kuuza Ni Rahisi, Mpe Hiki Mteja Wako

Ndugu, Hivi unajua kuwa kuuza ni rahisi? Ndiyo! Kuuza ni rahisi. Kinachonichanganya ni kuona wauzaji wengi wanaleta ugumu katika hili. Wananichanganya sana.

Kuuza wanaona kama ni kitu chenye ugumu sana. Ngoja nikwambie kitu, watu pamoja na makampuni mbalimbali wanahitaji kununua. Wanazo changamoto wanataka zitatuliwe. Ni wajibu wetu sisi wauzaji kuwahudumia. Namna pekee kuwahudumiwa ni kuwajua wako wapi na wanahitaji nini unachoweza kuwahudumia.

Unachopaswa kujua ni kwamba, kuuza hakujaanza leo, yaani karne ya 21, kumeanza miaka mingi iliyopita. Unachopaswa kujua ni kwamba, ikiwa utafanya vema kwenye kuuza hasa kwa wateja wako basi jua mafanikio yanakuhusu. Unaenda kuuza ziadi na kuikuza biashara yako.

Vitu vinavyotukwamisha na kufanya tushindwe kukuza biashara mpya ni hofu. Hofu inafanya tushindwe kutoa mahitaji lengwa kwa wateja wetu. Wengine tunaogopa kuwafikia. Ndiyo maana biashara mpya tunazoanzisha hazikui badala yake zinakufa. Hatuweki nguvu kujua mahitaji yao, tunaangalia sana juu ya mahitaji yetu.

Sheria ya mahitaji inasema, “kadiri unavyohitaji kitu ndivyo ufinyu wa kukipata unakuwa mkubwa”. Ukiwa huna wateja wa kuhudumia uhitaji wao unakuwa mkubwa sana kwako. Hali inayokunyima utulivu na kuanza kugusa kitu juu juu. Na ni rahisi watu wengine kujua hali uliyonayo maana sauti, toni, mazungumzo, lugha ya ishara, ujumbe unaotuma unaonyesha mazingira yenye huhitaji wa haraka sana. Uzingativu na utulivu unakosekana maana matokeo ndiyo unahitaji haraka. Unaweza kukutana na mteja wa kwanza asipoeleweka muda huo unamuacha unaenda kwa mwingine. Kwa sababu unahitaji kuuza haraka sana.

Hali hiyo ipo pia kwa wateja wako. Mteja akiwa na uhitaji wa kitu sio rahisi kuanza kupoteza muda. Anaenda moja wa moja kwenye kupata kitu hicho.

Chukulia mfano unapoenda hospitalini ukiwa unaumwa na unahitaji matibabu. Unapofika kwa daktari huna muda wa kupoteza, unakuwa mpole huku ukielezea shida yako ili akusaidie upone. Chochote anachokwambia fanya unatii haraka sana. Hata kwa wateja wako ipo hivyo ni wewe kujua mahitaji yao na kuyafanyia kazi. Katika uhitaji huo utulivu kwao unakuwa chini maana wanataka matokeo ya haraka. Wakati mwingine hupelekea usumbufu mkubwa.

Ukiwa katika hali ya uhitaji unakuwa na maamuzi yasiyo sahihi na kihisia unakuwa huna utulivu kabisa. Kukosa utulivu kihisia na maamuzi mabaya vinakuingiza kwenye msongo wa mawazo. Hali inayokufanya ushindwe kuuza kwa wateja wako. Hata kwa mteja inakuwa hivyo akiwa na uhitaji wa kitu ni rahisi wewe kumshawishi haraka akachukua. Ila unapaswa kujua kwamba kuwa na maumivu ni suala moja na kuwa na mahitaji ni suala jingine.

Unapoongea na mteja lazima uwe na umakini wa hali ya juu. Gusa hadi hisia zake. Sheria ya tabia inasema “Watu hufanya kitu kwa hisia na kuhalalisha kwa mantiki”. Ndiyo maana mara nyingi nasema, sisi binadamu ni watu wa hisia. Ukiweza kuteka hisia za mteja utakuwa na uwezo mkubwa kumuuzia.

Umewahi kuona mtu ambaye anaumwa kabisa, lakini kila mkimwambia aende hospitali kupata matibabu anakataa. Anaanza kusema; Oh! nitakuwa sawa ngoja nisikilizie kesho nitakavyoamka.

Lakini majira ya saa nane usiku hali inavyozidi kwa maana ya kukohoa au kuharisha damu anavyokuwa mpole na kuomba awahishwe hospitalini kupata matibabu! Au mtu mwingine anayo njaa kweli kweli na pesa anayo lakini akakaa na njaa yake hadi jioni, au mwingine anahitaji kuwahi mahali fulani pesa anayo lakini anaamua kutembea na kusema bora lawama kuliko kutumia pesa yangu. Njaa inapozidi kunakuwa hakuna jinsi anaitumia haraka na kupata hitaji lake.

Ipo hivyo kwenye mauzo. Mteja anaweza kuwa na uhitaji wa kitu kabisa lakini asifanye maamuzi ya kukichukua. Ni mgonjwa anaumwa lakini hataki kununua dawa. Hili ni suala unalopaswa kulijua ili unapokutana na mteja uongeze nguvu ya kumshawishi ili afanye maamuzi ya kuchukua hitaji hilo.
Alikuwepo bwana mmoja tumuite Tonny. Alikuwa anawakatia watu bima.

Siku moja alienda kumtembelea rafiki yake Jerry, alipofika alikaribishwa vizuri. Wakafanya mazungumzo vizuri, kisha akamshirikisha mpango wake kuwa anahitaji gari yake ikatiwe bima lakini sio kwa wakati huo.

Anahitaji hilo suala lifanyike baada ya miezi sita atakapokuwa amepata pesa ya kulipia gharama. Mkata bima akamweleza kuwa yeye atamkatia bima, kwa gharama za awali kisha ikipita miezi sita atamalizia malipo lakini rafiki yake alikataa.

Tonny alimweleza Jerry madhara yanayoweza kumkumba asipokatia bima gari yake pamoja na kumuonyesha ushuhuda wa watu waliokata bima na kunufaika nayo. Ilimchukua masaa kadhaa kumshawishi hatimaye akawa amekubali kukatiwa bima. Kilichomshangaza Tonny ni malipo aliyofanya Jerry.

Maana mwanzoni alisema hana pesa ya kulipia hadi hapo baadaye. Lakini alipompata ushuhuda na kumwelezea manufaa alishawishika ana akalipia gharama zote. Haikupita wiki moja gari la Jerry ikapata ajari, kwa kuwa alikuwa ameikatia bima akapata fidia. Hapo hapo akamtafuta Tonny na kumshukuru kwa namna alivyomsaidia kumkatia bima ya gari yake.

Unaweza kuona kuwa pamoja na kuwa na maumivu ya kitu lakini suala la kufanya maamuzi na kupata mahitaji muhimu kutatua maumivu hayo linatupa shida. Kazi uliyonayo mtu wa mauzo ni kumsaidia mteja wako kufanya maamuzi.

Tonny angemuacha Jerry bila kumwelezea madhara ingekuwa hasara kwake. Huenda angehusika kuchangia gharama za urekebishaji maana walikuwa marafiki.

Hali hiyo ipo kwa wateja wako, ili uweze kuwauzia vizuri hakupaswi kuishia tu kwenye matokeo nenda mbele mpe ushuhuda. Huu unaongeza nguvu na kumfanya mteja aone kwamba hayuko peke yake.

Muhimu; Mteja wako mpe matokeo. Mwambie anaenda kupata moja mbili tatu. Hapo utakuwa na nafasi ya kumsogeza karibu na mauzo.

Fanyia kazi yote ukiyojifunza katika makala hii. Habari Njema Ni Kwamba Kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo tayari Hardcopy. Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu namna ya kuwahudumia, kuomba rufaa, kuwafuatilia na kuwabakiza Katika biashara yako milele. Ni wewe tu kuchukua kitabu hicho kwa ajili ya kupata maarifa zaidi.

Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi

Leave a comment