Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Hii Ndiyo Njia Iliyothibitishwa Kukupatia Wateja Wengi Zaidi Katika Biashara Yako

Ndugu, Wateja ulionao katika biashara yako, ni watu muhimu kuikuza biashara kwa sababu wanaiamini sana kuliko watu wengine.

Wateja hao ni mgodi unaoweza kukusaidia wewe kukuza mauzo yako. Hivyo, unaweza kuwatumia kupata wateja wengine zaidi na kuikuza biashara yako. Hii ni kwa sababu watu wanapoambiwa na watu wao wa karibu wanaowaamini ni rahisi wao kukubali. Maana kunakuwa na uaminifu mkubwa ndani yao. Njia ya kuwatumia wateja ulionao kupata wateja zaidi inaitwa rufaa.

Kuomba rufaa ni kitendo cha kumuomba mteja uliyempatia huduma au uliyekutana naye, akupe mtu mwingine, anayeweza kunufaika na bidhaa au huduma yako. Kwa lugha rahisi, mteja wa rufaa ni zao la mteja uliyehudumia au kukutana naye. Anakupa mawasiliano yake au kumwelekeza kuja katika biashara yako. Anapokupa mawasiliano unapata urahisi wa kumfikia kwa njia ya mawasiliano. Ila kama unaweza kumfikia ana kwa ana ni nzuri pia. Mfikie.

Katika wateja wote unaokutana nao au kuwasiliana nao. Hakuna mteja rahisi kama mteja wa rufaa. Maana unapewa na mtu wake wa karibu. Mtu ambaye wanaaminiana. Hutumii nguvu kubwa kumpatia huduma. Ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikishauri wauzaji wengi kuomba rufaa. Maana ni njia rahisi kuwageuza wateja kuwa kamili. Faida saba za mteja wa rufaa;

Moja; Mteja wa rufaa ni rahisi kupata miadi. Hii ni kwa sababu anatoka kwa mtu anayekujua, kukwamini na kukupenda.

Mbili; Bei inakuwa sio tatizo kwao. Kwa kuwa anatoka kwa mtu anayeaminiana naye kwako anataka uaminifu basi.

Tatu; Wateja wa rufaa ni rahisi kufunga nao biashara au kuwauzia. Tofauti na mteja unayemtafuta wewe upya, ambaye anahitaji kukujua na kukuamini. Ila mteja wa rufaa tayari kuna mtu wake wa karibu wanaaminiana anapoona amechukua bidhaa kwako inakuwa rahisi pia kuchukua.

Nne; Wanakuwa tayari wameshaambiwa kuhusu wewe. Unapoanza kuongea nao huanzi upya mwanzo kuelezea kuhusu biashara yako. Unaanza kuelezea namna mtu wake wa karibu aliyenufaika na bidhaa yako. Hilo linamfanya awe mwepesi kukusikia na kuchukua hatua.

Tano; Hawachukui muda mrefu kufanya maamuzi. Mteja mpya tarajiwa unayemtafuta wewe anahitaji muda; kwanza kuijua biashara yako na kukuamini pia, anakuwa na hofu kuhusu ubora wa biashara yako na mahitaji yake. Lakini mteja wa rufaa hiyo yote haimpi shida. Anaamini mtu wake wa karibu hajafanya makosa kukuchagua wewe. Ndiyo maana hachukui muda mrefu kufanya maamuzi.

Sita; Mteja wa rufaa hujenga uaminifu mkubwa kutoka kwa mtu wake wa karibu.

Saba; Mteja wa rufaa hahitaji gharama kubwa kumpata. Maana ni zao la mteja uliyempatia huduma nzuri.

Wajibu wako kama mtu wa mauzo kuweka juhudi na kutoa thamani kubwa kwa mteja unayemuhudumia kwenye biashara yako. Maana kupitia huyo kuna watu wengi unakuja kuwapata.

Wateja wa rufaa unapowapata unaweza kuwaweka kwenye makundi tofauti labda kundi A, B na C kulingana na mwitikio wao.

Wakati wa uwasilishaji wako au mazungumzo yako, jitahidi kujibu mapingamizi unayokutana nayo ili uweze kuongeza namba ya watu unaowauzia kwenye biashara yako.

Kwa kila mtu unayezungumza naye au kumuuzia usiache kuomba rufaa. Wengi wetu tunaogopa sana suala la rufaa linapokuja. Ni wajibu wako mtu wa mauzo kuomba rufaa.
Sababu za wauzaji kutoomba rufaa kwa watu wanaozungumza nao au kuwauzia;

Moja; Wanasahau.
Zipo sababu nyingi zinazofanya wauzaji wasahau kuomba rufaa. Wengi wetu huwa hawana utamaduni wa kuomba. Hivyo, hushtuka baada ya mteja kuwa ameondoka.

Mbili; Kutojiamini.
Sababu nyingine inayowafanya wauzaji kushindwa kuomba rufaa ni woga, wanaogopa wateja watawaonaje. Wanaogopa kusikia hapana. Wengine wanahofia wateja kutorudi tena kununua. Au watabadili mtazamo wa kununua. Wengine wanadhania mteja huyo hastahili kuombwa rufaa. Kwa hiyo, hayo yote yanawafanya kushindwa kuomba rufaa. Kama wewe ni mtu wa namna hiyo jua hutoweza kuomba rufaa.

Tatu; Ubora wa bidhaa zao.
Wauzaji wengine huhofia ubora wa bidhaa zao, ikiwa hazitamsaidia mteja kupata anachotaka. Ndiyo maana huogopa kuomba rufaa. Huku, wengine wakishindwa kuielezea biashara yao.

Nne; Kutoijua biashara. Kushindwa kuijua biashara kwa kina ni moja ya sababu inayowafanya wauzaji kushindwa kuomba rufaa. Maana ushawishi unakuwa mdogo.

Tano: Hawajui namna ya kuomba rufaa.

Hii ni sababu ya mwisho, inayowafanya wauzaji kushindwa kuomba rufaa. Hawakuwahi kufundishwa shuleni au mahali popote ndiyo maana hawaombi. Wanashindwa mahali pa kuanzia.
Hizi sababu unapaswa kuzifanyia kazi kama ni meneja au unao wafanyakazi wako. Ili uone namna gani unaweza kuwasaidia waweze kuomba rufaa na kuikuza biashara yako. Unahitaji kuwa na mfumo tunaouita endeless referral yaani rufaa isiyo na ukomo. Ikiwa na maana ya kulala usingizi mwororo, huku ukijua kuna wateja wanaisubiri biashara yako siku inayofuata.

Habari Njema Ni Kwamba Kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo tayari Hardcopy. Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu namna ya kushughulika na wateja wa rufaa, kuwafuatilia na kuwabakiza Katika biashara. Tuwasiliane 0767702659, utafikishiwa popote Tanzania karibu tujifunze zaidi.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi.

Leave a comment