Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Ufuatiliaji Na Siri Ya Kuuza Zaidi Kwa Wateja Wako

Unapoamka asubuhi, kuna mipango mingi na mizuri unakuwa umepanga kuifanya. Lakini kadiri muda unavyozidi kusogea kuna mipango unaona kabisa ufanyikaji wake ni mgumu.

Hii ni kwa sababu siku yako inaingiliwa na vitu vingine vingi nje ya mipango yako. Ndiyo maana, unapanga hiki kinajitokeza kingine hadi unakuta umesahau baadhi ya mipango yako.

Hiyo ni hali ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Wala hupaswi kuwa na wasiwasi. Unavyoona mambo yako yanakuchanganya hata kwa mteja wako ipo hivyo.

Wateja ni watu kama wewe. Wana mambo mengi, wanavurugwa na kelele na usumbufu unaoendelea kwenye maisha yao.

Kutokana na kelele hizo, wanakosa nafasi ya kuendelea kukufikiria kama hutakuwa na sababu ya kuwafanya wakukumbuke.

Kuwasiliana na wateja mara kwa mara ni moja ya njia za kuhakikisha wanaendelea kukukumbuka. Sio kila unapowasiliana na mteja unamtaka anunue, wakati mwingine taka tu kujua wanaendeleaje, mpe salamu za pongezi kwa mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye maisha yake.

Moja ya huduma nzuri anayohitaji mtu wako wa karibu ni kufuatiliwa. Kupitia ufuatiliaji wa mara kwa mara ndipo yeye hujisikia vizuri, na kuendelea kuwa karibu yako. Kama hufanyi hivyo, hapo katikati akaji tokeza mtu anayeonekana kumfuatilia ni rahisi kumchukua.

Wauzaji wa madaraja ya juu huweka utaratibu mzuri wa kufuatilia wateja wao. Wanahakikisha angalau kwa wiki wanamgusa mteja kwa kitu kimoja.

Inaweza kuwa ujumbe wa kufuatilia, maudhui elimishi, ujumbe binafsi, kuwasilisha mapendekezo au ujumbe wa salamu.

Kwanini wanawafuatilia wateja hao? Hapa chini nimekuwekea sababu;

Moja; Kuwa karibu yake.
Hii ipo wazi, mara zote akili yetu huwa inampa nafasi ya pekee mtu anayekuwa karibu yake. Unachopaswa kujua ni kwamba wateja wanapitia changamoto mbalimbali. Wanaweza wasikwambie moja kwa moja lakini zipo changamoto zinawasumbua.

Sisi wauzaji tupo kwa ajili ya kuzitatua, ndiyo maana tupo kwa ajili yao. Kupitia ufuatiliaji unamfanya mteja ahisi upo karibu naye. Anapopata changamoto ni rahisi kukushirikisha kuona namna gani unaweza kumpatia suluhu. Maana kupitia ufuatiliaji unamfanya kuwa karibu nawe.

Mbili; Kufanya atukumbuke sisi na biashara au huduma yetu.
Kwenye maisha kuna mambo mengi yanatokea, iwe tunapenda au hatupendi. Mambo ya kuumwa, kufiwa, kupata ajali na mambo mengine. Mambo haya yanapotokea ni dhahiri kuna huduma inabidi itolewe kukidhi mahitaji. Unapokuwa unawafuatilia wateja wako, linapojitokeza jambo lolote katika ya hayo na ukawa unatoa huduma hiyo ni rahisi mtu kukumbuka.

Unakumbuka kuna siku ulipigiwa simu na rafiki yako akakueleza kuwa amefungua huduma ya chakula. Anashughulika na kuhudumia sherehe, siku za kuzaliwa na vitu kama hivyo, ulipokua kwenye kikao cha harusi yako wakahitaji mhudumiaji upande wa chakula ulimtafuta nani? Kwa haraka ulimtafuta rafiki yako.

Pengine namba yake hukuwa nayo, ukaingia sehemu ya waliokupigia siku za karibuni ukawasiliana naye. Kilichofanya uwasiliane naye ilikuwa ni kumbukumbu na kutaka akupe huduma nzuri.

Tatu; Kuonyesha tunamjali.
Moja kati ya falsafa ya biashara ni hii, “wajali wateja wako nao watajali kuhusu biashara yako”. Namna bora ya kuwajali ni pamoja na kuwafuatilia ili kujua maendeleo yao. Uzuri sisi binadamu tuna tabia ya kuwa karibu au kupenda kuwashirikisha fursa watu wanaoonekana kuwa karibu yetu na kutujali. Hili lipo wazi.

Unapokuwa unawajali wateja ni sawa na umewapa deni kubwa. Namna pekee ya wao kulilipa ni kununua kwenye biashara yako au kukuletea wateja wengine. Hakuna mtu asiyependa kuona wengine wanamjali.

Lengo kuu la ufuatiliaji tunataka kuondoa dhana ya kumtafuta mtu wakati wa shida. Ndiyo maana nasema ufuatiliaji mzuri sio wa kumfuatilia mteja ukimuomba anunue. Mfuatilie kwa nia njema, akihitaji huduma yako atakwambia wewe maana upo karibu naye.

Wauzaji bora wenye mafanikio makubwa wanafanya ufuatiliaji kwa muda mrefu bila kuacha na kwa msimamo na hiyo ndiyo siri kuu ya ushindi wao katika kuuza zaidi.

Unachopaswa kujua ni kwamba;
Kwenye mauzo na maisha kiujumla mambo hayatakuwa mepesi. Yaani kwenda vile unavyotaka. Ndiyo maana tunasema. Ili uwe mfuatiliaji mzuri huhitaji kuruhusu sababu. Maana ni mengi utayaona. Iwe ni matatizo yetu au wapinzani wetu lakini hali ya ukinzani utakutana nayo. Kutakuwa na milima tunayotakiwa kupanda kuelekea kileleni.

Swali la kujiuliza, unapokutana nao au hali za namna hivyo unafanyaje? Bila kujali uwezo, uelewa, malighafi, elimu, pesa, historia yako. Endelea kujiuliza namna gani unaweza kufanya kitu ilimradi usirudi nyuma.
Unafanyaje unapokutana na Goliath, hasira, chuki, uongo, woga vikwazo, umechoka na mapingamizi? Yote kwa yote tunapaswa kupambana zaidi.

Je, unawafuatilia wateja wako? Bonga nasi kwa chochote hapa hapa.

Kwa mafundisho zaidi pata kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA Ndani yake kimeelezea mengi kuhusu ufuatiliaji wenye tija kwa wateja, kuomba rufaa na kuwabakiza Katika biashara yako milele.

Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi
Karibuni.

4 Comments

  • Charles
    Posted November 10, 2023 at 9:46 am

    Yamoto sana hii, imeshiba vya kutosha. Madini ya gharama kubwa sana.

    • Post Author
      Lackius Robert
      Posted November 13, 2023 at 6:10 am

      Wao! Amazing message. Asante sana, Karibu tujifunze zaidi

  • Miraji abdallah
    Posted November 10, 2023 at 2:54 pm

    Wateja wanavurugwa na Mambo mengi hivyo ni vigumu kuendelea kukumbuka.
    Baada ya mteja kuwa umeshamuuzia endelea kuwasiliana nae mala kwa mala na hiyo itasaidia akukumbuke pale apatapo changamoto .
    Asante Sana kocha.

    • Post Author
      Lackius Robert
      Posted November 13, 2023 at 6:09 am

      Karibu sana Miraji Abdallah. Tufanyie kazi masomo haya.

Leave a comment