Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Siri Ya Kuwafikia Wateja Wengi Yafichuka, Ujumbe Mfupi Wahusika.

Kitu cha kushangaza katika mchakato wa kuwafikia wateja 100 kwa siku ni kwamba, baadhi ya wauzaji wamekuwa wanasema siwezi kuwafikia. Kila nikiwatembelea siwakuti au sipati nafasi ya kuonana nao au nikipiga simu hawapokei.

Lakini nikwambie kitu, ipo njia nyingine ya kumfikia mteja. Njia hiyo ni ya kutumia ujumbe mfupi. Kwa Kiingereza inaitwa “Short Message Sending” (SMS).

Faida za kutuma ujumbe Mfupi;

Moja; SMS ni haraka na rahisi kutuma.
Ili utume SMS huhitaji kuwa elimu kubwa au simu kubwa. Simu ya aina yoyote inaweza kumfikia mhusika ndani ya muda mchache.

Tafiti zinaonyesha asilimia 77% ya wateja hutumia muda kujibu SMS. Hii ni kwa sababu kila mmoja anamiliki simu.

Mbili; SMS zinaimarisha mahusiano mazuri na wateja.
Mtu anapopata ujumbe mfupi kutoka kwa mtu huwa anajisikia vizuri na kuona amethaminiwa.

Tatu; Wateja wanapenda kutumiwa SMS.
Wateja wanaweza kuona tangazo lako wasichukue hatua zaidi lakini wanapoona ujumbe mfupi huchukua hatua haraka sana.

Tafiti zinaonyesha asilimia 98% watu hufungua SMS.
Asilimia 55 % ya kampuni hutumia message kuwasiliana na wateja wao.

Baadhi ya wauzaji wamekuwa wanapata taabu sana hasa linapokuja suala la kutuma ujumbe mfupi. Haya ni baadhi ya maswali tunayojiuliza;

Moja; Naenda kuandika kuhusu nini kwa huyu mteja?

Mbili; Naanzaje kuandika ujumbe huu?

Tatu; Nitampa jibu gani kwa huyu mteja, ikiwa kauliza swali?

Nikuhakikishie hakuna jambo baya litajitokeza. Unachotakiwa ni kutuma ujumbe mfupi. Askari awapo vitani huwa hajiulizi mara mbili kuhusu adui. Anajipanga kadiri anavyoweza kisha kuingia msituni. Mengine ni majaliwa.

Unakumbuka enzi za utoto ulipoibiwa pesa uliyotumwa kununua mafuta. Ukaanza kuwaza namna gani utamwambia mama. Hii ni kutokana na ukali aliokuwa nao. Kila ukitafuta kitu cha kuongea unashindwa lakini ulipofika nyumbani ulipata kitu cha kumwambia na hakukupiga. Badala yake alikukanya na kukwambia uongeze umakini na upunguze michezo.

Ndivyo ilivyo kwa wateja wako. Wajibu wako kama mtu wa mauzo ni kuwasiliana na mteja. Unapokuwa unajiuliza zaidi kuhusu ujumbe upi unaoenda kumtumia mteja, tambua kuwa tayari tunazo aina kadhaa za watu unaoenda kuwatumia ujumbe.

Kuna wateja uliowatembelea, hawa unawashukuru kwa muda waliokupa kuongea na wewe.

Wateja waliofanya manunuzi au uliopata namba kutoka kwa watu uliowauzia (rufaa). Hawa pia, unawapigia kujitambulisha kwao, huku ukiwaelezea namna gani wanaweza kunufaika bidhaa zako.

Katika mchakato mzima hupaswi kuwa na wasiwasi kwenye kukosea tunajifunza kutokana na makosa.
Uzuri unaijua biashara yako, wewe ongea nao. Usiogope wewe andika. Utapata uzoefu kadiri utakavyokuwa unaongea na wateja wako. Unapopata nafasi ya kuongea na mteja jitahidi kuwa na shauku kubwa pamoja na ujasiri.

Itakusaidia sana kwenye kukuza ukaribu na wateja wako. Mara zote hakikisha ujumbe unakuwa mfupi unaoenda moja kwa moja kwenye mambo ya msingi.

Jinsi ya kutuma ujumbe mfupi;

Moja; Jitambulishe, weka jina la kampuni yako kama lipo.

Mbili; Weka kiini cha ujumbe. Hapa andika sentensi nzima.

Tatu; Nenda kwenye jambo la msingi. Epuka kuzunguka. Mwambie maana ya kumtumia ujumbe. Ndiyo maana unaitwa ujumbe mfupi. Hili sio gazeti wala makala au jarida.

Nne; Epuka vifupisho, mfano; BS, badala ya Bosi. Hbr, badala ya Habari. MJ, badala ya meneja. GR badala ya grupu pamoja na maneno mengine mengi. Wewe andika neno zima kama linavyotakiwa kuwa.

Tano; Tumia linki zinazoeleweka. Huna uhakika wa linki iache.

Sita; Hakiki ujumbe kabla ya kuutuma. Hii inapunguza makosa mbalimbali mfano, kisarufi, kimuundo au kimaana.

Saba; Jua namba zako, kisha watumie mara nyingi zaidi.

Tahadhari; Usiandike ujumbe unaendesha gari kasi au unakimbia kimbia. Unapokosea baadhi ya herufi mfano; badala ya neno sikia unaweza kukuta inaandika “skia”. “Inka” badala ya inuka. Hii hali inapoteza ladha ya maana kwa msomaji. Weka simu chini, simama au simamisha gari uandike ili kuepuka makosa. Andaa ujumbe wako na utume, Kisha uendelee na safari.

Nenda kafanyie kazi yale yote uliyojifunza katika makala hii. Chukua pia, vitabu vya Chuo Cha Mauzo, Mauzo NI RAHA, Mauzo Ni Huduma na Mauzo Ni Mahusiano.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Tanzania. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.

1 Comment

  • Faraji
    Posted December 1, 2023 at 5:26 am

    Ni njia rahisi na haina ghalama, tatizo ni nini hatuitumii kila siku

Leave a comment