Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Madaraja Ya Mafanikio Kwenye Maisha Na Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora.
Hiyo ni kwa sababu jinsi unavyofanya kitu chochote kwenye maisha, ndivyo unavyofanya kila kitu.
Huwezi kukazana kuwa bora kwenye mauzo kama kwenye maeneo mengine siyo bora.

Kwenye maisha, watu huwa hatulingani.
Huwa tuna madaraja tofauti ambayo yanatokana na vile tulivyo.
Watu wawili wanaweza kuzaliwa wakati mmoja, wakapata elimu sana na kufanya kazi au biashara ya aina moja kwa kipindi sawa, lakini bado wakatofautiana sana kwenye mafanikio.

Tofauti hiyo kwenye mafanikio haitokani na mmoja kupendelewa zaidi ya mwingine.
Au mmoja kukutana na vikwazo zaidi.
Bali tofauti zinatokana na madaraja ambayo watu hao wanakuwa.

Kwenye mfumo wa elimu, matokeo ya mtihani wa mwisho huwa yanatolewa kwa madaraja.
Kuanzia daraja la kwanza, la pili, la tatu, la nne na daraja sifuri.
Maisha pia huwa yana njia ya kuwapanga watu kwenye madaraja kupitia matokeo wanayozalisha kwenye maisha yao.

Watu wamekuwa wanalalamikia mfumo wa elimu kwamba unaweza usiwe sawa, kwa sababu unalinganisha watu wote kwa kipimo kimoja.
Lakini mfumo wa maisha umekuwa na usawa mkubwa, kwa sababu unampima mtu kwenye kile ambacho yeye mwenyewe amechagua au kukubali kufanya.

Kwenye safari ya mafanikio, kuna madaraja matano yanayotokana na hatua ambazo watu wanachukua na matokeo ambayo wanayapata.

Daraja la kwanza ni mafanikio ya juu kabisa.
Hili ni daraja linalofikiwa na wale ambao wana ari kubwa ya kufanya kile walichochagua kufanya.
Hawa ni wale ambao wanafanya kile kilicho sahihi kufanya bila hata ya kuambiwa wafanye.
Watu hawa hupata malipo makubwa na heshima kubwa pia.

Kwenye mauzo, daraja la kwanza ni la wauzaji ambao wanafanyia kazi mchakato wa mauzo kwa juhudi kubwa bila ya kusubiri kuambiwa.
Hawa mchakato wa mauzo ndiyo kipaumbele cha kwanza kwenye shughuli zao za kila siku na ndiyo wanaupa muda na umakini mwingi.
Kwenye vipaumbele, wanatumia kanuni ya 99/01, ambapo asilimia 99 wanaweka kwenye mauzo na asilimia 1 kwenye vitu vingine.
Matokeo wanayopata ni wanakuwa wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea, wanapata malipo makubwa na yasiyokuwa na ukomo na wanaishi maisha ya ndoto zao.

Hili ndiyo daraja unalopaswa kulipambania wewe kama muuzaji unayetaka kuwa bora kabisa.

Daraja la pili ni mafanikio makubwa.
Hili ni daraja la wale ambao wanafanya kitu sahihi baada ya kuambiwa mara moja.
Watu wa daraja hili hupata malipo mazuri na heshima ya wastani.
Hawa siyo watu wa kujiongeza wao wenyewe, lakini pia siyo watu wa kusukumwa.

Kwenye mauzo, watu wa daraja la pili ni wale wanafanya vizuri pale wanapopangiwa mchakato wa mauzo wa kufanyia kazi.
Wakishaambiwa wanachopaswa kufanya, wanakifanya kwa uhakika.
Kwenye vipaumbele, wanatumia kanuni ya 80/20, ambapo asilimia 80 wanatumia kwenye mauzo na 20 kwenye mambo mengine.

Hili bado ni daraja zuri kwenye mauzo, kwani linampa mtu matokeo ambayo ni makubwa na mazuri.
Ni daraja linalompa muuzaji kipato kizuri na maisha bora.
Kama utashindwa daraja la kwanza, basi hili ndiyo daraja unalopaswa kuhakikisha unakuwa.
Kama umeshindwa kujiongeza na kufanya kilicho sahihi, basi hakikisha kile unachoambiwa ufanye, unakifanya mara moja na kwa uhakika.

Madaraja ya chini yaliyobaki nitayataja kwa ufupi uyajue, ila sitayaelezea sana kwa sababu hupaswi kuwa kwenye madaraja hayo.
Lakini ni muhimu uyajue ili uyaepuke kama ukoma na kama upo kwenye daraja lolote kati ya hayo uondoke haraka.

Daraja la tatu ni mafanikio ya wastani.
Hili ni daraja ambalo watu wanafanya kitu baada ya kuambiwa zaidi ya mara moja.
Watu wa daraja hili ni wa kusukumwa ndiyo waweze kufanya.
Hilo linapelekea wapate malipo ya wastani na wasipate heshima kabisa.
Wauzaji walio kwenye daraja hili ni wale ambao mpaka wasukumwe sana ndiyo wanakaa kwenye mchakato sahihi wa mauzo.
Kama muuzaji, epuka daraja hili, halitakufikisha popote.

Daraja la nne ni mafanikio duni.
Hili ni daraja ambalo watu hawafanyi kitu mpaka wawe na mahitaji yao binafsi.
Hapa watu wanafanya kwa sababu hawana namna nyingine.
Watu kwenye daraja hili wanapata malipo ya chini na hakuna heshima kabisa.
Wauzaji walio kwenye daraja hili ni wale ambao wakifanya mauzo makubwa na kupata malipo mazuri, wanakuwa hawana tena msukumo wa kufanya mauzo makubwa, hata wasukumweje. Ni mpaka malipo mazuri waliyopata yaishe ndiyo wanakuwa tena na msukumo.
Hili ni daraja ambalo hupaswi kuwepo kabisa.

Daraja sifuri ni la kushindwa kabisa.
Hili ni daraja ambalo watu hawafanyi kitu hata waambiwe, wakumbushwe, wasisitizwe na hata kulazimishwa.
Hawa ni watu ambao hawana mbele wala nyuma na hivyo hawapati malipo yoyote wala heshima.
Hawa ni ambao wanaishi maisha ya kushindwa na yasiyo na mwelekeo.
Ukiwa kwenye daraja hili, habari yako inakuwa imesha, maana unakuwa hata hujitambui. Utapigiwa kila aina ya kelele lakini hakuna utakachosikia.

Hatua ya kuchukua;
Ujue mchakato sahihi wa mauzo tunaojifunza kwenye CHUO CHA MAUZO na ishi mchakato huo kila siku bila hata ya kusubiri kuambiwa.
Kuwa na msimamo kwenye kuishi mchakato sahihi wa mauzo mara zote bila kujali ni matokeo gani unayoyapata.
Kwa njia hiyo utaweza kutengeneza matokeo makubwa kwenye mauzo.

Na pale unapopitiwa na kushindwa kuzingatia mchakato, unapokumbushwa, tekeleza kwa uhakika bila kusubiri kukumbushwa mara kwa mara na kulazimishwa.
Huwezi kuwa muuzaji bora kwa kulazimishwa.
Utakuwa muuzaji bora kwa msukumo mkubwa unaoanzia ndani yako.
Ndiyo maana utaweza kuwa muuzaji bora kama upo kwenye daraja la kwanza au la pili pekee.
Chini ya hapo utaishia kuwa kawaida na kupata matokeo kidogo.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

6 Comments

  • Alex
    Posted November 6, 2023 at 4:36 pm

    Daraja la Kwanza na Daraja la pili ndipo pambano lilipo .

    • mauzo
      Posted November 7, 2023 at 1:48 pm

      Hakika,
      Tupambanie hapo.

  • Faraji
    Posted November 6, 2023 at 7:05 pm

    Ipo kazi kupata namba namba 1 na 2

    • mauzo
      Posted November 7, 2023 at 1:49 pm

      Ni kweli na ni kazi inayowezekana kabisa.

  • Miraji abdallah
    Posted November 6, 2023 at 10:00 pm

    Ni hakika, kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa Bora, utakuwa muuzaji bora kwa msukumo
    mkubwa unaozia ndani yako.
    Asante Sana

    • mauzo
      Posted November 7, 2023 at 1:50 pm

      Ndiyo, tuweke juhudi kuwa watu bora ili pia tuweze kuwa wauzaji bora.

Leave a comment