Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Hivi ndivyo unavyoenda kuwafanya wateja waipende biashara yako

Watu wanaweza kuwa wanakaa sehemu moja lakini hawanunui kwao. Sio kwamba bidhaa hamna wala biashara kufunguliwa ila ni namna tu ya huduma wanayopewa.

Ikiwa wanahudumiwa vizuri ni rahisi kurudi kila mara tofauti na wanapohudumiwa vibaya. Pata picha umeenda kupata huduma fulani, ukaelezea unachotaka mhudumiaji anakutazama tu. Huku muda ukiwa unaenda, lakini wengine wanahudumiwa. Je, utafurahia biashara hiyo? Jibu ni hapana.

Ndugu, ni gharama kubwa kutafuta wateja wapya kuliko kuwafanya wale ulio nao tayari wabaki kwako. Hivyo, ni lazima uwathamini na uwajali wateja ulionao au unaoendelea kukutana nao.

Unahitaji kuwafanya wateja wako wawe na furaha. Unahitaji kuwafanya wawe wateja wanaokuja kwako kila mara na waweze kuleta marafiki zao. Kama utakuwa na wateja wasio na furaha, wanaweza wakasambaza maneno yasiyo mazuri kuhusu biashara yako kwa watu wengine.

Sasa unafanya nini kuhakikisha wana furaha na biashara yako? Njia hizi hapa za kuwafanya wateja wako wapende wanachopata kutoka kwako;

1. Jifunze huhusu wateja wako

Ili kufanya wateja wako kupenda biashara yako, kwanza unahitaji kujifunza kuhusu wao na kujua wanachotaka. Anza kwa kutafuta wateja wako wanataka nini kwa kuchunguza nini kipo sokoni na nini hakipo. Wakati wa kuchunguza kuhusu soko, unatakiwa kutafuta kujua juu ya mahitaji, matakwa, maslahi ya wateja wako.

Ukijua wateja wanachotaka, utaweza kuwapa wanachotaka. Mfano, kama umetafiti na kugundua sehemu fulani kuna uhaba wa nafaka, Hotel au spea za pikipiki na magari. Hiyo ni njia rahisi kuanzisha biashara na kupata watu. Wateja wakipata wanachotaka, lazima wafurahi, na wathamini biashara yako. Hivyo, endelea kuongea na kuwasikiliza wateja wako.

2. Kuwa na uvumilivu

Wateja hawatapenda unachofanya kila wakati. Ni kawaida na mara zote wateja kuwa na matatizo na bidhaa tofauti. Hata wote tumewahi kuwa wateja na tukalalamika sana kuhusu bidhaa fulani. Kitu cha muhimu wakati mteja atakapokuja kukulalamikia kitu, uwe mvumilivu.
Ni rahisi kutupilia mbali madai yake kuhusu bidhaa zako na hata kumfukuza. Lakini, chukua muda wa kumsikiliza mteja. Kuwa na subira nao na usikilize kila kitu wanachosema.

Hata kama wanalalamika kitu ambacho hakihusiani na wewe. Uvumilivu ni sehemu ya huduma nzuri kwa wateja. Hata wahenga waliwahi kusema “mvumilivu hula mbivu”. Baada ya mteja kumaliza kueleza malalamiko yake, basi unaweza kumjibu. Zingatia kuwa, usimfanye ajione kuwa mawazo yake hayana msingi. Kumbuka, mteja mara zote yuko sahihi.

3. Usiwachukulie kama wateja, wafanye marafiki.

Watu hununua kwa marafiki zao. Kwa maana hiyo, unahitaji kujuana na kuwa na uhusiano binafsi na wateja wako. Ongea na wateja wako kama wao ni marafiki wako. Hata kama hauna uhusiano wa moja kwa moja na wateja, bado unaweza kuongeza uhusiano wa kibinafsi kati ya biashara na wateja wako. Unaweza kutumia majina yao katika barua pepe. Pia, unaweza kushirikiana na wateja wako katika mitandao ya kijamii.

Unapokuwa umewafanya kama marafiki itakuwa rahisi wewe kuwajua kwa kina na wao kujua huduma unayotoa. Hali itakayokusaidia kuwapatia matokeo kugusa maumivu yao, kuwapa suluhu na matokeo wanayotaka. Hatimaye kuikuza biashara kama mipango yako ilivyo.

4. Toa ofa

Watu wengi wanapenda ofa kama vile punguzo la bei na ofa. Wateja wakiona wanapata thamani za pesa zao kutokana na ofa za bidhaa zako. Ukiwafanyia hivyo watakuwa na uwezekano mkubwa wa kurudi kwako au kuwa karibu yako.

Unaweza kutoa punguzo katika sherehe za msimu wa sikukuu, mwisho mwaka au unaweza kutoa bidhaa za bure kwa wateja wazijaribu. Au ile ya nunua moja upate moja bure. Uuzaji huo huhamasisha wateja kuendelea kurudi kwenye biashara yako. Wakinufaika na punguzo katika bidhaa zako, watapenda biashara yako zaidi.

Mambo haya ukiyazingatia na kuyafanya kwa muda mrefu bila kuacha utakuwa na wateja wengi wanaopenda biashara yako. Maana wateja wanaumizwa kila siku, hawasikilizwi wala kupewa ofa nzuri. Badala yake wanakandamizwa. Wajali wateja wako watajali na kuipenda biashara yako.

5. Kuwa na vipaumbele.
Maana ya vipaumbele ni kipi kianze kipi kifuatie. Kwenye kutoa huduma kuna watu huwa wanaofika mapema kabla ya wengine. Lakini baadhi yetu tumekuwa tunawaacha na kuwahudumia wengine.

Hii kibiashara sio sawa. Kwani humfanya mteja ajisikie vibaya. Haiwezekani mtu afike wa kwanza na kupata huduma akiwa wa mwisho. Hii inapaswa kutokea labda bidhaa anayotaka haipo. Inaenda kufuatwa mahali. Ila tofauti na hapo hapana. Kwenye huduma kipaumbele muhimu ni kumuhudumia mteja.

Ili kuwafanya wateja wajisikie vizuri na kupenda biashara yako, wape kipaumbele kulingana na ufikaji wao katika biashara eneo la biashara yako. Usiangalie ananunua vitu vya kiasi gani. Wewe mpe nafasi ya kumuhudumia atafurahia.

Je, kati ya haya mambo matano wewe unayatumiaje katika kuwafanya wateja kupenda biashara yako? Bonga nasi hapa hapa kwa maoni na ushauri.

Habari njema ni kuwa, kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo jikoni kinaandaliwa. Unavukaje mapingamizi, kuongeza ushawishi, kuwafuatilia wateja. Vyote vipo ndani ya kitabu hicho. Endelea kutufuatilia hapa hapa ili uwe wa kwanza kupata kitabu hicho pindi kitakapokuwa tayari.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi

Leave a comment