Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Zana Yenye Nguvu Katika Kukuza Mauzo Yako Mara Mbili na Zaidi

Umewahi kufikiria ni kwa namna gani simu yako inaweza kukunufaisha zaidi? Ndiyo! Simu yako inaweza kufanya mambo mengi zaidi unavyofikiria. Songa nami upate dondoo zinazoenda kukusaidia kukuza mauzo yako mara mbili zaidi na kuboresha maisha yako.

Ndugu, Simu ni zana bora na itaendelea kuwa zana bora na yenye nguvu zaidi kwenye mauzo. Ilianza kuwa na nguvu kwa muda mrefu na manufaa yake yamekuwa makubwa sana. Maana inaweza kuwafikia wateja wengi ndani ya muda mfupi, hasa ikitumika inavyotakiwa matokeo yake ni makubwa sana.

Weka akilini kuwa simu ndiyo zana ya kwanza na muhimu kabisa ambayo kila muuzaji anapaswa kuitumia vizuri kwenye mchakato wake wa mauzo. Tafiti zinaonyesha wastani kwa siku mtu hushika simu yake zaidi ya mara 100.

Tupo kwenye zama za sayansi na teknolojia. Kila mtu anayo simu ya mkononi na asilimia kubwa wanazo simu kubwa tunazoita simu janja (smartphones). Hilo linafanya kuwafikia wateja wengi kuwa rahisi. Iwe ni kwa njia ya kupiga kawaida au kutumia simu za kuonana (video calls).

Mtu wa mauzo lazima uwe na mkakati wa kuwasiliana na wateja wako kwa kuwapigia simu. Unapaswa kuwa na mpango wako wa kila siku ya mauzo wenye idadi ya wateja ambao unawapigia simu. Wateja unaowasiliana nao wanapaswa kuwa wapya hata kama kuna walionunua karibuni na walionunua muda mrefu. Sio mbaya kuwafikia kwa njia ya kupiga simu. Maana ukiweza kufanya hivyo kwa msimamo kuna nguvu kubwa ya kufanya mauzo makubwa na kuwafikia wengi.

Nisikilize mimi! Simu yako ni zana yenye nguvu katika mauzo yako. Mwisho wa simulizi. Usipoitumia vema jua inakunyonya.

Wauzaji wengi wanaogopa kupiga simu, wanatuma ujumbe mfupi au barua pepe hali inayopelekea baadhi ya wateja kushindwa kuwajibu wauzaji kwa wakati. Hapa naamini unaelewa vema ninachomaanisha huenda hali hii ilishawahi kukumba.

Nakusihi upige simu kadiri unavyoweza. Uzuri kupiga simu haichukui muda mrefu. Kama unatumia dakika moja hadi mbili kwa kila simu kwa muda wa saa moja na nusu utapiga simu zaidi ya 50. Hizi hapa sababu zinazofanya wauzaji wengi kuogopa kupiga simu:

(I). Hawajui nini waseme wanapoongea na wateja. Na wengine hawana skiripti ya mauzo.
(II). Wanaogopa majibizano na wateja.
(III). Wanaogopa kukataliwa.

Wakati naandika makala hii nilipigiwa simu na rafiki yangu akiomba ushauri. Alisema sikiliza Lackius, napata shida kuongea na simu ya kwanza ninayopiga kwa wateja wangu.

Ila mteja wa ana kwa ana sina shida naye. Wateja wa kwenye simu mambo yanakuwa tofauti. Naogopa wasije kukwamisha malengo yangu ya mwezi. Nifanyeje? Nilimwambia, pole sana Jacob kwa changamoto hiyo, zingatia mambo haya matatu utapiga simu zaidi;

Moja; Muda wa kupiga simu. Angalia muda unaoenda kupiga simu, uwe ni muda wa kazi. Isiwe asubuhi sana wala usiku sana. Kumbuka siyo mdeni wako.

Pili; Mada ya mazungumzo. Kama mteja alikuwa ana changamoto ya bei hukumuuzia mtafute umuombe mfikie hitimisho. Kama aliulizia bidhaa akaondoka, mpigie umwelezee namna anavyoweza kunufaika na bidhaa yako.

Tatu; Anza kwa kumsifia au kumpongeza. Katika mazungumzo yako jitahidi kutafuta kitu chochote cha kumsifia iwe upole, utulivu, uvumilivu wake au hatua anazoendelea kuchukua. Itakusaidia kuwa na mahali pa kuanzia. Ndiyo maana nakwambia usiache kupiga simu.

Endelea kupiga kupitia vikwazo, majibizano utajifunza kitu. Haupo peke yako unayekumbana na hali hiyo, kumbuka wauzaji wengi hawajafundishwa kupiga simu. Ni jambo unalopaswa kulijua. Wapo wengi waliokabiliwa na hali hiyo lakini wakaishinda. Unapokosea usiwe na wasi wasi, jifunze ni kupitia kujifunza unajiboresha zaidi. Haya hapa mambo matano kuzingatia ukiongea na simu;

Moja; Nasa Umakini. Taja jina lake; “Habari, Janeth”

Mbili; Jitambulishe; “Naitwa Lackius, natokea taasisi ya “Chuo Cha Mauzo”

Tatu; Lengo la kumpigia; “Naomba kupata miadi na wewe”, au kitu kingine ulichokuwa umejiandaa nacho.

Nne; Sababu; “Nimepata taarifa kuhusu mpango wa kuongeza mauzo kwenye kampuni yako.”

Tano; Nini unataka. Mwambie nadhani tuanzie hapa. Tukutane muda wa saa saba tuone namna ya kuelekezana juu ya fanikisha lengo hilo.

Sehemu muhimu sana ya mchakato wa mauzo ni kuweza kuwapata wateja tarajiwa wa kukutana nao na kufanya nao mazungumzo. Na hilo litahusisha kuwakatisha watu kwenye mambo yao wanayofanya na washawishike kukutana na wewe.

Kupiga simu ni sehemu muhimu ya kuanzia ili kuweza kupata wateja tarajiwa wa kukutana nao. Kupiga simu ndiyo kitu kitakachokutambulisha kwa wateja unaowalenga ila hawakujui na kuwashawishi wakutane na wewe.

Kupiga simu kwa watu ambao hawakujui ni zoezi ambalo wengi huwa hawalipendi, kwa sababu wanaogopa kukataliwa. Watu wanahofia kupiga simu kwa sababu zifuatazo;

Moja; Muda unaopiga simu unaweza usiwe sahihi kwa mteja. Jambo linalowafanya wasipokee simu. Mfano, saa moja asubuhi au saa nne usiku.

Mbili; Mteja anaweza asiwe na uhitaji wa kile unachouza kwa wakati huo. Hili ndilo huwakuta wauzaji wengi na kuwakatisha tamaa.

Tatu; Watu huwa hawapendi kupigiwa simu na watu wasiowajua. Hili ni suala la baadhi ya wenzetu, kwao simu mpya sio kipaumbele.

Nne; Simu yako inaweza kuwa inakatisha mambo muhimu kwenye siku yao.

Kwa sababu hizo hapo juu, ambazo ni za kweli kabisa, inamaanisha zoezi la kupiga simu kwa wateja tayari lina ugumu mkubwa kwako hivyo nafasi ya kufanikiwa ni ndogo.

Kila unapopiga simu na ukakataliwa, unapata hofu zaidi na kushindwa kuendelea na zoezi hilo.
Hivyo, unatakiwa kuweka mpango mzuri kupiga simu kwa wateja wako.

Umefika kwa mteja mahali pake pa kazi hujamkuta. Usimuache hivi hivi mpigie simu. Huenda alikuwa na changamoto ndiyo maana hajafika eneo lake la kazi. Unapofanya hivyo kwa muda mrefu bila kuacha unajikuta umewafikia wateja wengi zaidi.

Uwepo wa hizo sababu usikufanye ukaziabudu na kunyoosha mikono kwamba sasa basi mauzo kwa njia ya simu ni magumu. Nikukumbushe msemo wa “there is no free lunch” hakuna chakula cha bure. Unatakiwa kupiga simu bila kuacha wala kuchoka. Watu wanahitaji kuona simu yako mara nyingi zaidi na kwa muda mrefu.

Je, simu yako unaitumia katika matumizi yapi?

Habari njema ni kuwa, kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA kipo jikoni kinaandaliwa. Unawapigiaje wateja wako na maneno ya kuongea na mengine mengi. Vyote vipo ndani ya kitabu hicho. Endelea kutufuatilia hapa hapa ili uwe wa kwanza kupata kitabu hicho pindi kitakapokuwa tayari.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz ili uwe wa kwanza kupata makala na kitabu.

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi.

Leave a comment