Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Wateja Sio Wasumbufu, Wanahitaji Ufafanuzi Mzuri Kununua

Kuna siku nilikuwa nahitaji maziwa, nikatoka nyumbani kwenda kuyafuata. Wakati ninaenda, kwenye nyumba moja nikaona pamewekwa tangazo, tunauza maziwa. Nikasema safi sana, ngoja nigonge niulize.

Hazikupita dakika nyingi akaja mdada, tukasalimiana nikamuuliza kama maziwa yapo. Dada akaniambia maziwa yapo, na bei, nikatoa fedha kusubiria kuletewa maziwa. Dada akapokea fedha akaenda. Kwa furaha nikasubiria maziwa, maana eneo lile maziwa yalikuwa yanasumbua. Ukizingatia nilikuwa na wageni. Baada ya dakika kadhaa dada akarudi, akaniambia inabidi uwe na dumu lako la kubebea maziwa. Hapa hatutoi madumu ya bure. Je, dumu unalo?

Nikasema sina, kwani bei gani kuchukua na dumu? Akasema hatuna madumu hadi uje nayo. Nikasema sawa, ngoja nifuate. Akasema pesa yako hii hapa. Ukipata dumu njoo. Akarudi ndani na maziwa yake.

Nilitafakari tukio hili kwa dakika chache sikuelewa wazi nini kilipelekea yeye kunijibu vile awali. Nikaona labda wamezoea wateja wao wanakuja na madumu yao, na hivyo kutokutoa huduma ya madumu ni gharama kubwa kwao. Hayo nilitafakari nikiwa nimepanda Boda boda kufuata dumu.

Baada ya dakika chache nikifika kwangu na kuchukua dumu la lita tano na kurudi kwa dada kuchukua maziwa maana nilikuwa na shida nayo. Nilifika na kugonga mlango, dada akafungua na kuniambia samahani kaka maziwa yameisha labda usubirie kesho.

Nikamuuliza kwanini hukunitunzia maziwa wakati uliona ninafuata dumu?

Je, kwanini hamjaweka madumu pembeni kuwa mnauza?

Na kwanini kwenye tangazo hakuna maelezo ya kwamba mtu aje na kifaa chake?

Dada akasema wewe kaka unaonekana msumbufu. Unauliza maswali mengi. Nikamwambia je, si niliita boda boda mbele yako na kukwambia nafuata dumu nitunzie maziwa. Ulifanya hivyo? Dada kimya. Kiujumla niliumia mno. Nimepoteza muda na pesa niliyomlipa boda boda.

Je, ungekuwa ni wewe ungefanya nini?

Hali iliyonikuta ni moja kati ya hali wanazokutana nazo wateja wakati wa huduma. Wanapokutana nazo wanaanza kuuliza maswali mengi. Wanapata hasira kwa sababu maslahi yao na maumivu hayajazingatiwa.

Unaweza kuona hata baada ya kutopata maziwa lakini bado dada hakuwa tayari kunisaidia kupata maziwa sehemu nyingine. Badala yake anaanza kuniambia mimi ni msumbufu. Unafikiri kama mteja nilijisikiaje? Lazima uumie.

Kwa hiyo, unapokuwa kwenye biashara ukakutana na hali kama hizi. Kuzikabili unahitaji kuwa na mtazamo sahihi kuhusiana na wateja. Sio wateja wote watakuelewa vile unavyotaka iwe lazima uwe na mtazamo sahihi namna ya kuendana nao. Bila kuwa na mtazamo mzuri kwamba sio wasumbufu hutoweza kwenda nao vema.

Sababu kubwa inayowafanya wauzaji wengi kuwaona wateja kama wasumbufu ni kutokana na mtazamo mbaya kuhusu wao. Mteja anapouliza swali unaona kama anakusumbua wakati anataka kujua zaidi. Kuna hofu anayo juu ya bidhaa yako, anahitaji kupata uelewa zaidi. Na wewe unapomchukulia hivyo, utampoteza na utaanza kuongea vibaya nao maana tayari kuna dhana umeijenga kwao.

Kutoa pesa kunauma, hiki ni kitu unachopaswa kujua kama muuzaji bora kuwahi kutokea. Wateja wanatafuta pesa katika mazingira magumu, wakati mwingine wanachomwa na jua, wanalala wamechelewa, wanafanya kazi hatarishi kuipata hiyo pesa. Hivyo, wanapokuwa wamepata hiyo pesa wanahitaji kufanya manunuzi yanayoenda kutatua changamoto zao.

Ipo hivi, mteja anapokuja katika biashara yako au unapokua unaongea naye kuna hitaji analo au kuna namna anaelewa jambo. Ikiwa na maana anapokuwa anakupatia maelezo ili baadaye umhudumie anachotarajia kutoka kwako ni kumsikiliza na kumpatia hitaji au huduma yake.

Kujaribu kupingana na anachosema mteja ni ugomvi mkubwa unataka kuanzisha. Maana hakuna mtu anayekubali kushindwa huku akitoa pesa yake. Atakachoweza kufanya ni kuendelea kukupinga ili kudhihirisha kuwa kipo kitu anakijua kuhusu bidhaa fulani. Mjadala huo lazima uwe mkubwa na ikiwa mmoja wapo hatoshuka basi hitimisho halitaweza kufikiwa mwishowe hakuna utamkosa mteja.

Mambo ya kutoka nayo;
Moja; Mpe nafasi ya kujielezea mteja.
Mbili; Mpe maelezo kuendana na mazungumzo yake.
Tatu; Msaidie kupata huduma yako.
Nne; Usimuingize gharama za ziada yasiyo na ulazima.
Tano; Kuwa na mtazamo chanya, amini mteja sio msumbufu bali anahitaji maelekezo.

Fanyia kazi yote uliyojifunza hapa ili uwahudumie vizuri wateja wako. Bonga nasi kwa chochote hapa hapa.

Kwa mafundisho zaidi pata kitabu Cha MAUZO NI HUDUMA ndani yake kimeelezea mengi kuhusu kushughulika na wateja kwa njia rafiki, kuwahudumia vizuri, kuwauzia, kuwafuatilia kisha kuwabakiza katika biashara yako milele.

Makala imeandaliwa na Lackius Robert, Mwandishi wa vitabu na Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Karibu tuwasiliane kupitia 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz

Hakika, mauzo ni huduma.
Karibu tujifunze na kuuza zaidi
Karibuni.

1 Comment

  • Miraji abdallah
    Posted November 16, 2023 at 3:22 pm

    Nimesoma makala kwa uturivu mkubwa . Ninaunga mkono hoja
    1. Mpe nafasi mteja ajieleze
    2. Mpe mteja maelezo kuendaa na nale aliyoeleza
    3. Msaidie kupata huduma bora na pia
    usimsababishia gharama zisizo za lazima.

Leave a comment