Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Mchakato Wa Maisha Ya Kila Siku.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora.
Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Mafanikio kwenye maisha ni kama safari. Wakati watu wengi huwa wanasubiri mwisho wa safari ndiyo wafurahie, ni mpaka wanapofika mwisho ndiyo wanagundua furaha ilipaswa kuwa wakati wa safari na siyo mwisho.

Kumbuka kipindi unasoma shule, ulikuwa unatamani sana siku ya kuhitimu masomo yako. Ni siku ambayo uliisubiria kwa hamu kubwa. Uliona jinsi ambavyo maisha yako yatakuwa ya raha pale unapoamka asubuhi na hufikirii kuwahi shule.

Lakini nini kilitokea baada ya kuhitimu masomo yako? Siku chache za mwanzo ulifurahia hali ya kutokuhitajika kwenda shuleni. Lakini baadaye ulichoka maisha hayo ya kutokwenda shule. Ulianza kukumbuka matukio muhimu ya shule.

Kwa mfano huo halisi kabisa kwenye maisha yetu, tunajifunza jinsi ambavyo furaha haipo mwisho wa kitu, bali kwenye safari ya kukiendea kitu hicho.
Hiki ni kitu ambacho watu wengi hawajawahi kufundishwa na matokeo yake ni kuwa na maisha yasiyo na furaha.

Maisha ya wengi yanakosa furaha kwa sababu kila wakati kuna kitu wanakikimbiza, ambacho wanaamini wakikifikia ndiyo watafanikiwa na kufurahi. Lakini matokeo yake ni wanapofikia kitu hicho, wanaona kingine kikubwa zaidi, ambacho inabidi wakikimbize pia.

Kwa ufupi, hivi ndivyo wengi wanavyoishi maisha yao bila ya kuyafurahia.
Wanaanza wakiwa shuleni, ambapo wanaona wakihitimu masomo yao watakuwa na raha sana.
Wanahitimu masomo na wanaanza kufikiria kupata kazi au biashara inayowaingizia kipato.

Furaha yao inasogezwa mbele, wakijiambia wakishapata kazi au biashara itakayowaingizia kipato, watafurahi sana.
Wanapata kazi au biashara inayowaingizia kipato. Na hapo lengo la furaha linabadilika.
Sasa linakuwa ni kuwa na mahitaji ya msingi, kama makazi, usafiri n.k.

Mtu anakazana na kupata baadhi ya vile alivyokuwa anataka. Na hapo lengo la furaha linabadilika na kuwa kupata familia.
Alipata familia lengo la furaha linabadilika na kuwa kukuza familia mpaka ifikie kujitegemea.
Baada ya hapo lengo la furaha linakuwa ni kustaafu.

Hivyo ndivyo watu wanaenda wakihamisha lengo la furaha na kujikuta wakiishi maisha yao yote bila ya kufurahia hatua mbalimbali wanazokuwa wamepiga.

Na hapo ni kama wameweza kupata matokeo waliyokuwa wanataka. Hali huwa inakuwa mbaya zaidi pale wanapokosa matokeo waliyotaka.
Hapo ndipo wengi huvurugwa na kukata tamaa kabisa. Wanajiona ni watu wa kushindwa na wasioweza kufanya makubwa.

Njia pekee ya kuondokana na hali hiyo ya kutokuyafurahia maisha au kukata tamaa pale mambo yanapokwenda tofauti na matarajio ni kuwa na MCHAKATO WA MAISHA YA KILA SIKU.

Mchakato wa maisha ya kila siku ni utaratibu wa kuyaendesha maisha yako ambao unaufuata kila siku bila kuacha, hata itokee nini.
Hii inakuwa ndiyo ratiba kuu ya maisha yako ambayo unaifuata kila siku bila kuacha.

Mchakato huo unakuwa umeupangilia kwa namna ambayo ukifanyika kwa msimamo na kwa muda mrefu, matokeo unayoyataka yanakuwa ya uhakika.
Kwenye mchakato wako wa maisha ya kila siku, kila jambo linakuwa limepangiliwa muda wake na kufanywa kwenye muda huo kila siku.

Sasa kwa sababu huna udhibiti na matokeo, wewe unajidhibiti kwa kuhakikisha unafuata mchakato wako kila siku bila kuacha.
Ni ile hali ya kufuata mchakato wako kila siku ndiyo inayokupa furaha kwenye maisha.
Kwa sababu husubiri mpaka upate matokeo ndiyo ufurahie, badala yake unafurahia kila siku kwa kukamilisha  mchakato wako.

Mchakato wako wa maisha ya kila siku unapaswa kuutengeneza kwa namna ambayo utakupa kile unachotaka kupata kwenye maisha yako.
Yaani mchakato huo unakuwa ndiyo safari yako kuu ya mafanikio.
Lakini pia unapaswa kuendana na michakato ya wale waliofanikiwa kwenye  maeneo mbalimbali.

Uzuri wa mafanikio ni kitu cha wazi, wale wanaofanikiwa kuna mambo wanayafanya ambayo wengine pia wakiyafanya wanaweza kufanikiwa.
Moja ya vitu ambavyo waliofanikiwa wanafanya ni kuwa na mchakato wa maisha ya kila siku ambao wanaufuata mara zote bila kuuvunja.

Katika kuandaa na kuandaa mchakato utakaouishi kila siku, zingatia kuweka mambo haya 10 ambayo yapo kwenye michakato ya watu waliofanikiwa zaidi.

1. Amka asubuhi na mapema.
Kuamka asubuhi na mapema ni moja vitu vitakavyokutofautisha sana na wengine.
Unapata muda wa kujiandaa vizuri kwa siku inayokuwa mbele yako.
Ukiwahi kuamka unaweza kuwahi kwenye mengine yote ya muhimu.

2. Andaa orodha ya majukumu ya siku.
Ipangilie siku yako nzima kwa kuorodhesha majukumu unayotaka kukamilisha na muda wa kufanya majukumu yako.
Kuiendesha siku bila ya kuwa na orodha ni kuchagua kuipoteza siku hiyo.

3. Jifunze.
Kila siku jifunze ili kuendelea kupiga hatua kwenye maisha yako na tasnia yako pia. Muda mzuri wa kujifunza ni asubuhi na mapema kabla siku haijaanza na mambo ya kufanya yakawa mengi.
Kila siku tenga muda ambao utajifunza kwa kusoma, kusikiliza na kuangalia ili uendelee kuwa bora.

4. Masaa mawili ya dhahabu.
Kwenye muda wako wa kazi, masaa mawili ya kwanza yatenge kwa ajili ya kutekeleza majukumu yanayokamilisha lengo lako kuu.
Kwenye muda huo usiruhusu usumbufu wowote kukuingilia. Tekeleza majukumu yanayochangia kwenye kufikia lengo kuu ulilonalo.
Ukiweza kutenga masaa mawili na kuyatumia vizuri, utakamilisha makubwa kuliko siku nzima ya kufanya vitu huku ukiwa na usumbufu.

5. Jali afya yako.
Afya ndiyo mtaji wa kwanza kwenye kujenga mafanikio. Bila ya kuwa na afya imara, mengine yote yatashindwa.
Ni wajibu wako wa kila siku kuhakikisha unajali afya yako.
Na hapa unahitaji kula kwa afya, kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika.

6. Jali fedha zako.
Fedha ni kitu muhimu kwenye maisha, ukiondoa pumzi ambayo unaipata bure ukiwa mzima wa afya, kinachofuatia kwa umuhimu ni fedha.
Kwenye mchakato wako wa kila siku kuwa na muda wa kujali na kupitia hali yako ya kifedha.
Hapo unaangalia njia za kuongeza zaidi kipato chako, kudhibiti matumizi yako, kuweka akiba kwenye kila kipato na kuwekeza.
Kila unapopokea kipato chako binafsi, anza kwa kuweka akiba pembeni kabla ya matumizi. Kisha wekeza akiba hiyo mara moja ili usije ukaitumia.

7. Jali mahusiano yako.
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, mafanikio yetu yanatokana na ukubwa na uimara wa mahusiano yetu. Kila siku chukua hatua kujenga na kuimarisha mahusiano yako na watu wa karibu, washirika, wateja na wengine wanaohusika kwenye yale unayofanya.
Mahusiano yanajengwa na kuimarishwa kwa kutoa kabla ya kuomba. Angalia ni vitu gani unaweza kutoa kwa wengine ili baadaye unapowataka wakupe unachotaka, wanakuwa tayari kufanya hivyo.

8. Fanya kitu cha tofauti.
Pamoja na kwamba unao mchakato unaoufuata kila siku bila kuacha, unapaswa kuwa unafanya mambo ya tofauti ili kupata matokeo makubwa.
Kila siku fanya kitu kipya ambacho hujawahi kufanya au fanya kwa ukubwa na utofauti ambao hujawahi kufanya. Jisukume sana kutoka nje ya mazoea yako na hivyo ndivyo utakavyozalisha matokeo makubwa na ya tofauti.
Pia kwa yale unayohifia kufanya, jisukume kuyafanya. Hiyo ni kwa sababu dawa ya hofu ni kufanya kile unachokuwa unahofia kufanya.

9. Usiahirishe kinachoweza kufanyika.
Huwa ni rahisi kuahirisha kitu ulichopanga kufanya kwa kujiambia utafanya kesho. Lakini kesho ikifika, unajiambia tena utafanya kesho. Hivyo ndivyo unavyoishia kuwa na tabia ya kuahirisha mambo na kujinyima mafanikio.
Ukipanga kufanya kitu, panga na muda wa kukifanya kisha kwenye muda huo fanya kitu hicho. Hata kama hutamaliza kufanya, ni bora uanze, kwa sababu utakuwa umepiga hatua kuliko kutokufanya kabisa.
Jijengee sifa binafsi ya kukamilisha kila unachopanga na utaweza kufanya makubwa.

10. Itathmini siku yako.
Kila siku unayoimaliza, tenga muda wa kujifanyia tathmini ya jinsi siku hiyo ilivyokwenda kwako.
Kwenye tathmini yako ya kila siku angalia maeneo matatu; ukamilishaji wa majukumu uliyopanga, mapya uliyojifunza na maboresho ya kufanya kwenye siku inayofuata.
Kama utaitathmini kila siku yako na kuchukua hatua sahihi, huwezi kuyakosa mafanikio, kwa sababu utaviona na kuvivuka vikwazo mapema.

Mafanikio kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku nyingi ambazo mtu ameziishi kwa mafanikio.
Kwa kuwa na mchakato wa maisha ya kila siku ambao unaufuata bila kuacha, kila siku yako inakuwa ya mafanikio na hatimaye unakuwa na maisha ya mafanikio.

Kwenye mchakato wetu wa CHUO CHA MAUZO kila siku hakikisha unashiriki kipindi cha mafunzo na UNAGUSA WATEJA WASIOPUNGUA 100. Ukikamilisha hayo na mengine utakayoyaweka kwenye mchakato wako wa kila siku kama ulivyojifunza, mafanikio kwako yanakuwa ni ya uhakika.
Inakuwa ni swala la muda tu kuyafikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Tengeneza mchakato wako wa maisha ya kila siku na fuata mchakato huo kwa msimamo na kila siku bila kuacha.
Utakuwa mtu bora na hatimaye muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea.
Utauza kwa uhakika na kwa wingi na siyo kwa kubahatisha.
Anza kuyaendesha maisha yako kwa mpango huu na upate manufaa makubwa.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora.
Kocha Dr. Makirita Amani,
Mkuu wa CHUO CHA MAUZO
www.mauzo.tz

2 Comments

 • Faraji
  Posted December 4, 2023 at 5:41 am

  Faraha au hazuni ni kila siku unapofakiwa au kutofanikiwa katika siku yako na kusubiri matokeo au mwisho wa mchakato

 • Kizito bakwanye
  Posted December 4, 2023 at 5:48 am

  Asante kocha mimi nimependa sana hii ya jali fedha zako na kwa kweli usipo zipendant fedha zako nakuzijali
  Wengine watazipenda nakuzijali kwa nafasi yako watatumia mbinu yoyote ili wazitoe katika mfuko wako kwa hiyo hili nakwenda kulifanyia kazi pia kwasababu afia ndiyo mtaji namba moja nakwenda pia kujali afia yangu na kwasababu pia misingi yangu ni mi tatu yaani Utajiri,afia,na hekima kila asubuhi nitahuzuria vipindi ili kuendelea kujifunza zaidi. Asante

Leave a comment