Skip to content Skip to sidebar Skip to footer

Matumizi Bora Ya Akili Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.

Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Ili uweze kuwa muuzaji bora, lazima kwanza uwe mtu bora. Ni ubora wako kwenye kila eneo la maisha yako ndiyo utakaokuwa na mchango kwenye mafanikio yako kimauzo.

Kibaiolojia, sisi binadamu ni wanyama. Tupo kwenye kundi moja na wanyama wengine, ambao tunawafuga na hata wa mwituni. Hiyo ni kwa sababu kila ambacho kipo kwenye miili yetu, kipo kwenye miili ya wanyama pia.

Una moyo na mbuzi pia ana moyo, una ubongo na mbuzi pia ana ubongo. Kwa kila kiungo cha mwili ulichonacho, hata wanyama wengine pia wanacho.

Swali ni je, nini kinatutofautisha sisi binadamu na wanyama wengine? Kwa nini tunaweza kuwatawala wanyama wengine, licha ya kuwa wanaweza kutuzidi maumbo, ukali na hata sumu?

Na hapo jibu ni moja tu, kinachotutofautisha sisi binadamu ni akili zetu. Binadamu ndiyo viumbe pekee ambao wana akili zilizoendelezwa, zenye uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi.

Wanyama wengine wana ubongo na akili, lakini ni akili ambayo inafanya mambo kwa kufuata mazoea na mkumbo. Lakini akili ya binadamu ina uwezo wa kufikiri na kuja na njia mpya na bora za kufanya vitu mbalimbali.

Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa wanashindwa kutumia akili zao vizuri na kuishia kukosa mafanikio makubwa ambayo wangeweza kuyapata. Wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kama wanyama wengine kwa kuiga yale yanayofanywa na wengine bila hata ya kufikiri kwa kina.

Ili uweze kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kujijengea mafanikio makubwa, unapaswa kutumia vizuri akili yako. Kwenye somo hili unakwenda kujifunza mambo matatu ya kufanya ili kutumia akili yako kwa mafanikio makubwa.

Mambo matatu ya kufanya ili kutumia akili yako kwa mafanikio kwenye mauzo.

Moja; Ilishe maarifa sahihi.

Akili yako inajengwa na kile ambacho unailisha. Chakula cha akili huwa ni maarifa na taarifa ambazo zinaingia. Pale akili inapolishwa maarifa na taarifa hasi, inakuwa na mtazamo hasi na kuwa kikwazo kufanikiwa. Lakini akili ikilishwa maarifa na taarifa chanya, inakuwa na mtazamo chanya wa kuziona fursa nzuri za mafanikio.

Katika kuilisha akili yako maarifa sahihi, unapaswa kuzingatia yafuatayo;

1. Soma vitabu vyenye maarifa mazuri ya kukuwezesha kujenga mafanikio.

2. Sikiliza vitabu vilivyosomwa (Audio Books) ambavyo vinakujenga kimafanikio.

3. Angalia video za mafunzo mazuri ya mafanikio.

4. Epuka kufuatilia habari hasi za kwenye vyombo vya habari.

5. Epuka kushabikia maisha ya wengine ambayo hayana mchango kwenye mafanikio yako. Mfano kufuatilia udaku wa wasanii.

Hatua ya kuchukua; Kila unapokuwa, hakikisha kuna namna unailisha akili yako maarifa chanya na yanayokujenga ili kufanikiwa.

Mbili; Epuka raha rahisi.

Kwenye zama tunazoishi sasa, kuna mitego mingi sana ya raha rahisi kwa akili na ambayo imewafanya wengi kuwa walevi wa vitu vinavyotoa raha hizo.

Akili huwa ina mfumo wa kujipa raha pale mtu anapokamilisha kitu fulani. Raha hiyo huwa inatokana na kuachiliwa kwa kemikali ya Dopamine.

Kuna vitu ambavyo huwa vinaleta raha ya haraka, lakini huwa havijengi. Mfano kutumia mitandao ya kijamii, kutumia vilevi, kufanya mapenzi na mengine ya aina hiyo.

Kuna vitu ambavyo huwa vinaleta raha ambayo inachelewa, lakini vinajenga. Mfano kutimiza malengo uliyoweka, kukamilisha jukumu ambalo lilikuwa gumu na mengine.

Katika kuepuka raha rahisi, zingatia haya;

1. Acha matumizi ya mitandao ya kijamii yasiyo na tija.

2. Jidhibiti kwenye matumizi ya simu janja (smartphone).

3. Usitumie vilevi vyovyote kwenye muda wa kazi.

4. Weka malengo na yagawe kwenye vipande ambavyo unaweza kuvifanyia kazi na kuvikamilisha.

5. Kila siku andika orodha ya majukumu unayotaka kutekeleza (To do List) kisha kila unapotekeleza jukumu, weka alama ya vema mbele yake. Hiyo inakupa raha kuwa umekamilisha ulichopanga.

Hatua ya kuchukua; Epuka vitu vyote vinavyochechea raha rahisi (cheap dopamine) kwenye akili yako na fanya yale yanayoleta raha iliyo sahihi.

Tatu; Ipe akili yako mazoezi.

Ni kanuni ya asili kwamba kitu kinachotumiwa huwa kinakuwa imara na kile kisichotumiwa huwa kinakuwa dhaifu. Mfano mzuri ni misuli ya mwili, mtu anayenyanyua vitu vizito anakuwa na misuli mikubwa na imara kuliko asiyefanya hivyo.

Ili akili iwe imara inapaswa kupewa mazoezi mbalimbali. Kama ambavyo mtu anafanya mazoezi ya mwili, unapaswa pia kufanya mazoezi ya akili. Watu wengi sana wamekuwa na akili dhaifu kwa sababu ya kukimbilia mambo rahisi na kuachana na yaliyo magumu.

Ipe akili yako mazoezi kwa kufanya yafuatayo;

1. Unapokutana na ugumu kwenye kufanya jambo, usiache kufanya, bali endelea, akili yako itapata njia.

2. Shiriki michezo mbalimbali ya kutumia akili kung’amua mambo magumu.

3. Jifunze vitu vipya ambavyo hukuwa unavijua kabisa, mfano lugha mpya, ujuzi mpya n.k.

4. Epuka michezo ya kielektroniki (games) ambayo inakupa uraibu. Hii inaweza kuonekana kama inaipa akili mazoezi, lakini inatengeneza ulevi.

5. Epuka usumbufu unaofanya akili ihame hame kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

Hatua ya kuchukua; Kila siku ipe akili yako mazoezi yanayoifanya iwe imara zaidi.

Kwenye somo hili tumejifunza na kuona jinsi ambavyo akili ni rasilimali muhimu sana kwa mafanikio yako kwenye mauzo na maisha kwa ujumla. Akili tayari unayo, haijalishi umekuwa unaitumiaje huko nyuma, kwa kuwa bado upo hai, unaweza kufanya mabadiliko makubwa. Anza sasa kuyaweka kwenye matendo haya uliyojifunza hapa ili uweze kuitumia akili yako kwa manufaa makubwa.

Kwa kuutumia vizuri akili yako utaweza kuwa mtu bora na kisha muuzaji bora kuwahi kutokea. Huhitaji kuingia gharama zozote kubwa ili kutumia akili yako kwa manufaa, anza sasa kwa yale ambayo ni ya msingi kabisa na utaweza kuutumia akili yako kufanya makubwa sana.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

Leave a comment